CURRENT NEWS

Saturday, August 5, 2017

MWANAUME MVAA MADERA NA KUDAIWA KUFANYA UHALIFU AKAMATWA PWANI-RPC SHANNA

Tokeo la picha la duka la madera
Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
JESHI la Polisi Mkoani Pwani, limemtia nguvuni kijana wa kiume mkazi wa Mbagala Jijini Dar es Salaam ambaye huvalia mavazi ya kike ikiwemo madera /hijabu na kuficha sura yake kwa kuvaa nikabu kisha kufanya matukio ya kiuhalifu.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Pwani (ACP)Jonathan Shanna alisema kijana huyo (jina limehifadhiwa)amekamatwa maeneo ya Picha ya Ndege barabara ya kuelekea Magereza akiwa amevaa mavazi hayo.

Kwa sasa jeshi hilo bado linaendelea na mahojiano ili kubaini mtandao anaoshirikiana nao kwenye matukio ya uhalifu.

Kamanda Shanna alieleza kwamba,wamemkamata baada ya kumwekea mtego uliowekwa na makachero waliokuwa wamepata taarifa kutoka kwa wasiri waliokuwa wanamtilia mashaka na kufanikiwa kumkamata akiwa kwenye bodaboda akielekea maeneo ya Magereza-Kibaha.

“Tunaendelea kumhoji kujua ni kwanini avae mavazi ya kike na tunawashukuru wananchi na wasiri wetu kwa kuendelea kutoa ushirikiano,” alisema Shanna.
Hivi karibuni kijana huyo alisababisha taharuki kwa wakazi wa Picha ya Ndege,baada ya kumuona akiwa anawasiliana na mtu mwingine huku yeye akijifanya ni mwanamke. 
Mwenyekiti wa mtaa wa Picha ya Ndege Joseph Zambo alisema kijana huyo alimfuata mtu waliokuwa wakiwasiliana naye kwa njia ya simu ambaye inadaiwa kuwa ni dereva bodaboda.

“Watu hawa walikuwa wakiwasiliana kwa njia ya simu na kijana huyo alikuwa akiigiza sauti ya kike na dereva bodaboda alijua fika kuwa aliyekuwa anawasiliana naye ni mwanamke,” alisema Zambo.

Alisema dereva bodaboda huyo alimwona kijana huyo kupitia ukurasa wake wa facebook ambapo ulipambwa na picha za msichana hali ambayo ilimfanya avutiwe naye.

“Mawasiliano yalianza kama siku tatu zilizopita na walikubaliana na ndipo bodaboda huyo alimwambia njoo Picha ya Ndege Kibaha lakini kijana huyo alipitiliza hadi Kongowe na ilibidi arudi ashukie Picha ya Ndege na alimwelekeza akishuka apande bodaboda ili aende kwake eneo la Sofu,” alisema Zambo.

Aidha Zambo alieleza,aliposhuka waendesha pikipiki walikuwa wakimfuatilia na walimwona amevaa dira na usoni kajifunga kitambaa ambacho kiliacha wazi macho akapandishwa kwenye pikipiki na kuanza safari ya kwenda kwa mtu wake.

“Wakiwa njiani upepo ulipuliza na dereva wa bodaboda akashangaa kuona miguu ya kiume lakini amevaa viatu vya kike akashtuka na kugeuza pikipiki kule alikotoka "
"Ndipo madereva bodaboda walipojaa na kuanza kumzonga hali iliyowabidi wamlete ofisini kwangu na ilikuwa tafrani kubwa ,wengine wakitaka kumpiga wakidai ni mwizi wa pikipiki,” alisema Zambo.

Alibainisha,baada ya kumfikisha walimfunua na kukuta kuwa ni mwanaume akiwa ameweka maziwa ya bandia .
Zambo alifafanua walianza kumhoji ndipo aliposema kuwa alikuja Kibaha kuja kuchukua hela na haikujulikana alikuja kuzichukua hizo fedha kwa njia gani.

Alisema zogo lilizidi ,bodaboda wakitaka kumpiga ndipo ikabidi wachukue gari na kumpeleka polisi kwa ajili ya usalama wake.

Wakati huo huo mkazi wa Mlandizi wilayani Kibaha Abdallah Chakame (25) amekufa akiwa anapatiwa matibabu kwenye hospitali Teule ya Rufaa ya mkoa wa Pwani ya Tumbi baada ya kupigwa na wananchi wenye hasira kali kwa tuhuma za wizi.

Kamanda Shanna, alisema kuwa marehemu alishambuliwa na watu wenye hasira kali kwenye kituo cha Daladala cha Kongowe.

Kabla ya kukutwa na mauti marehemu alikiri kujihusisha na matukio ya uvunjaji wa nyumba katika maeneo mbalimbali pia alitaja mahali alipohifadhi vitu alivyoiba.

“Baada ya ufuatiliaji tuliweza kufanikiwa kupata tv flati nchi 32 aina ya sharp, cd za aina mbalimbali, deki, meza ya tv moja, spika mbili za redio, feni moja, mashine ya kupimia mapigo ya moyo na mkasi wa kukatia makufuli,” alisema Shanna.

Aliwataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi pale wanapowakamata wahalifu badala yake wawafikishe katika vyombo vya dola ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.


 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania