CURRENT NEWS

Wednesday, August 16, 2017

STENDI YA KISASA YAJENGWA MJI WA KIBAHA AMBAPO ITAGHARIMU BIL.3.478-BYARUGABA


Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
HALMASHAURI ya Mji Kibaha mkoani Pwani, imeanza mradi wa ujenzi wa stendi ya kisasa utakaogharimu kiasi cha sh.billion 3.478.5.

Stendi hiyo inajengwa kwa ufadhili wa bank ya dunia kupitia fedha za ruzuku kwenye mradi wa uendelezaji wa miji (ULGSP) unaoendeshwa kwenye miji 18 hapa nchini ikiwemo Mji wa Kibaha.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha ofisa habari wa halmashauri hiyo ,Innocent Byarugaba alisema ujenzi wa stendi hiyo unajengwa kwa miezi sita hivyo unatarajia kukamilika januari 2018 .
Alisema kuwa ,halmashauri ya Mji wa Kibaha ndio makao makuu ya mkoa wa Pwani kwa zaidi ya miaka 40 iliyopita lakini ulikuwa hauna stendi kubwa inayokidhi mahitaji .
"Mji huu ni sebule ya popote unapokwenda ,hivyo inastahili na utapendeza ukijengwa stendi ya kisasa inayolingana na hadhi yake na itakuwa ni moja ya stendi kubwa hapa nchini kwetu" alielezea Byarugaba .
Aidha Byarugaba ,alieleza kwamba,itaondoa tatizo la mji huo kutokuwa na stendi ya uhakika kwa kipindi chote hicho .

Alisema stendi ambayo inatumika kwa sasa ni ndogo na imejengwa kwenye hifadhi ya barabara ambapo iko ndani ya mita 60 ikitakiwa kuondolewa na ina hudumia mabasi ya mikoa 24.

“Stendi mpya mara itakapokamilika inatarajiwa kuwa na uwezo wa kuhudumia mabasi 60 kwa wakati mmoja ,” alisema Byarugaba.

Byarugaba alifafanua ,stendi hiyo itakuwa na miundombinu mbalimbali ikiwa ni sanjali na kituo cha polisi, ofisi za mabasi, sehemu ya texi, Bajaji, pikipiki, huduma ya vyoo na  vibanda vya kupumzikia abiria.

Miundombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu, ATMs, kituo cha mafuta,gereji, hoteli na kizimba cha kuhifadhia takataka na huduma nyingine muhimu.

Aliwataka watu wenye viwanja vinavyozunguka eneo hilo na walioko kwenye eneo la kitovu cha mji wajenge kama ramani inavyojieleza kujenga ghorofa kuanzia moja na kuendelea kama sheria zinavyowataka.

Ujenzi huo unafanywa na kampuni ya Group Six International Ltd ambayo ilijenga stendi ya kisasa ya Msamvu mkoani Morogoro chini ya wataalamu washauri Ace Consult, Lupta Consult na Mhandisi.

 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania