CURRENT NEWS

Sunday, August 6, 2017

WAHAMIAJI HARAMU 72 NA WAKALA WAO WAKAMATWA PWANI


Na Mwamvua Mwinyi,Pwani 

JESHI la Polisi Mkoani Pwani ,linamshikilia mfanyabiashara anaedaiwa kuwasafirisha wahamiaji haramu 72 raia kutoka nchini Ethiopia,Rajabu Hitaji (30)mkazi wa Vigwaza ,Bagamoyo .
Aidha jeshi hilo linawashikilia pia wahamiaji haramu hao kwa kosa la kuingia nchini bila kibali . 

Akitolea ufafanuzi juu ya tukio hilo ,kamanda wa Polisi mkoani Pwani(ACP) Jonathan Shanna ,alisema uchunguzi unaendelea na watafikishwa ofisi za uhamiaji kwa hatua nyingine stahiki. 

Alieleza ,mtuhumiwa Hitaji ambae ni mfanyabiashara alikamatwa jana, saa 3.30 asubuhi huko maeneo ya pori la ranchi ya Taifa Narco ,Vigwaza wilaya ya kipolisi Chalinze . 

“Kufuatia msako mkali ulioendeshwa na makachero wetu baada ya kupata taarifa juu ya uwepo wa raia walioingia nchini pasipo kufuata taratibu za uhamiaji na raia hao baada ya kugundua kuna gari la polisi linawafuatilia “
“Waliingia kwenye hifadhi hiyo kwa lengo la kujificha lakini askari wetu waliweza kubaini mahali walipo kufuatia msako mkali uliokuwa ukiendeshwa katika ranchi hiyo ” alisema kamanda Shanna . 

Alisema askari hao walifanikiwa kuwakamata kundi la kwanza la wahamiaji haramu 63 wakiwa mahali ambapo gari halifikiki . 

Kamanda Shanna ,alielezea kwamba ,licha ya kukamatwa kundi hilo askari waliendelea na msako na kufanikiwa kukamata kundi jingine la wahamiaji haramu Tisa ,waliokuwa wakitafuta njia ya kutoroka katika ranchi ya taifa ya Narco . 

Wakati huo huo ,MTU mmoja na watoto wawili wamefariki dunia baada ya mtumbwi waliokuwa wakitumia kuvuka mto Ruvu kuzama.
Mtumbwi huo walikuwa wakiutumia kutoka upande wa Vigwaza kwenda upande wa Mlandizi katika mto huo wilaya ya kipolisi Chalinze Mkoani Pwani. 

Kamanda Shanna alisema ,tukio hilo limetokea majira ya saa kumi alfariji usiku wa kuamkia agost 6. 

Aliwataja waliopoteza maisha kuwa ni Sikuzani Mussa(41)ambae mwili wake bado haujapatikana na jitihada za kuutafuta zinaendelea.
Kamanda Shanna, alisema watoto waliopoteza maisha kwenye tukio hilo ni pamoja na Nusurat Haji mwenye miezi minne na Fesali Hamza mwenye mwaka mmoja . 

Aidha katika tukio hilo watu wawili waliweza kuokolewa wakiwa hai ambao ni Zuwena Ramadhani (29)na Tero Mziray (20).
“Dereva wa mtumbwi huo haijajulikana alipo na inaaminika ya kwamba yeye hajafa maji .”alisema . 


Kamanda Shanna, alieleza chanzo cha mtumbwi huo kuzama maji bado kinachunguzwa na miili ya marehemu imeshafanyiwa uchunguzi na kukabidhiwa kwa ndugu zao kwa ajili ya mazishi . 
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania