CURRENT NEWS

Wednesday, August 9, 2017

WATOTO WALIO NA ULEMAVU WAFICHULIWE KUPATA HAKI YA ELIMU-IDAMA

Walimu 24 kutoka halmashauri ya Mji wa Kibaha na Kibaha Vijijini Mkoani Pwani, walioshiriki katika mafunzo ya siku moja ya utambuzi wa mradi wa elimu jumuishi.
 Afisa program uhamasishaji wa shirika la kimataifa linalotetea na kuhudumia watu wenye ulemavu nchini (ADD)Isack Idama ,akizungumza katika mafunzo ya siku moja ya utambuzi wa mradi wa elimu jumuishi kwa walimu 24 wa shule za msingi kutoka halmashauri ya Kibaha mjini na Vijijini.
Afisa elimu ya watu wazima mkoani Pwani ,Hildelgade Makundi,akifungua mafunzo ya siku moja ya utambuzi wa mradi wa elimu jumuishi kwa walimu 24 wa shule za msingi kutoka halmashauri ya Kibaha mjini na Kibaha Vijijini
Picha na story Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
WAZAZI na walezi walio na watoto wenye ulemavu ,wametakiwa kuwafichua watoto wao walio na sifa ya kuanza elimu ya awali badala ya kuwaficha na kusababisha kukosa haki ya kupata elimu.
Akizungumza katika mafunzo ya siku moja ya utambuzi wa mradi wa elimu jumuishi kwa walimu 24 wa shule za msingi kutoka wilaya ya Kibaha mjini na Vijijini,afisa program uhamasishaji wa shirika la kimataifa linalotetea na kuhudumia watu wenye ulemavu nchini (ADD)Isack Idama ,aliomba jamii ihamasike na kuibua watoto hao.
Alieleza ,endapo tabia ya kuficha watoto wenye ulemavu itaachwa itasaidia kupunguza idadi kubwa ya watoto walio na ulemavu mbalimbali ambao hawajaandikishwa shule.
Kwa mujibu wa Idama,katika sensa ya mwaka 2012 karibu asimilia 9.3 /10 ya watanzania milioni . 3.15 wanaishi na ulemavu mbalimbali.
Alisema kwamba,utambuzi wa watu wenye ulemavu wa mwaka 2008 kati ya watoto 10 watoto wenye ulemavu wanaopelekwa shule ni wanne pekee.
“Na kati ya watoto 10 wasio na ulemavu 8-9 wanapelekwa shule hivyo kuna kila sababu ya kuibua idadi kubwa ya watoto wenye ulemavu iliyopo majumbani ili idadi iwe sawa na watoto wengine ”alisema Idama.
Idama alielezea kuwa,jamii itambue umuhimu wa elimu kwa watoto wote bila kuwabagua wala kuwanyanyapaa ,na kuwapeleka katika shule hasa za kawaida.
Aliiomba serikali kuwajengea miundombinu rafiki ,kupeleka walimu wenye ujuzi maalum na vifaa lengwa mashuleni  kwa watoto wenye mahitaji hayo ili waweze kupata elimu bora.
Akizungumzia malengo ya mafunzo hayo,alisema wamewapatia mafunzo walimu wa shule za msingi ambapo kila kata wamechukua mwalimu mmoja ambao wataenda kufanya zoezi la utambuzi wa watoto wenye ulemavu kuanzia miaka 3-6 kwa ajili ya kuanza elimu ya awali.
Idama alibainisha,elimu jumuishi itawezesha watoto hao  kupata fursa ya kupata elimu sawa na kupatiwa stadi na maarifa itakayowaandaa kwenda elimu msingi.


Awali akifungua warsha hiyo,kwa niaba ya afisa elimu mkoani Pwani,afisa elimu ya watu wazima mkoani hapo,Hildelgade Makundi alisema elimu jumuishi itawezesha kuondoa hali ya kuwatenga watoto .
Hildelgade alieleza ,jitihada za makusudi zifanyike kufichua watoto wanaofichwa ndani ya jamii ,Ushiriki wa jamii uwepo ndipo mradi utakapofanikiwa na kuweza kuwatambua watoto lengwa.
Kiongozi wa mradi wa elimu jumuishi kutoka ADD,Victoria Lihiru alifafanua ,wanatekeleza miradi ya elimu jumuishi kwa kufanyakazi na wizara ya elimu na TAMISEMI kuboresha elimu .
Alisema wanafunzi wa shule za awali 252 (chekechea)katika halmashauri nne ikiwa ni sanjali Mji wa Kibaha,Mkuranga,Kibaha Vijijini na Kisarawe mkoani Pwani,wanatarajia kunufaika na mradi wa kuongeza udahili wa watoto wenye ulemavu.

Victoria alisema kati ya shule hizo,shule 20 zitakuwa za mfano ambapo mradi utatekelezwa  kuanzia mwaka 2017-2021.

Akitoa mada iliyohusu sheria namba 9 ya mwaka 2010 inayotoa msukumo wa upatikanaji wa haki kwa watu wenye ulemavu ,mweka hazina wa shirikisho la vyama vya walemavu Tanzania(SHIVYAWATA),Elias Masamaki alisema mtu mwenye ulemavu
anastahili kupata haki sawa ikiwemo afya na elimu .

Mmoja wa walimu walioshiriki warsha hiyo,Winfrida Mkala kutoka shule ya msingi Mwendapole ,alisema mradi wa ADD ikishirikiana na serikali utafanikiwa kama serikali itaondoa changamoto za miundombinu ,walimu maalum na vifaa ikiwemo vya kusikia na kusomea watoto walio na ulemavu.

Shirika la kimataifa la ADD ,lipo nchini kwa takriban  miaka 20 kwa ajili ya kutetea,fursa na usawa kwa watu wenye ulemavu  huku  likifanya kazi na SHIVYAWATA.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania