CURRENT NEWS

Wednesday, September 13, 2017

DC NJWAYO ATEMBELEA ZAHANATI KUFUATILIA FEDHA ZA MPANGO WA KUBORESHA SEKTA YA AFYA( RBF )


 MKUU wa wilaya ya Rufiji ,Juma Njwayo wa kwanza kulia akizungumza jambo na kaimu mganga mkuu wa wilaya ya Rufiji, Didas Asenga .
Dc Njwayo atembelea zahanati kufuatilia fedha za mpango wa kuboresha sekta ya afya( RBF ) 
Na Mwamvua Mwinyi,Rufiji
MKUU wa wilaya ya Rufiji ,Juma Njwayo amewaagiza waganga wafawidhi wa zahanati na vituo vya afya wilayani hapo ,kufuata miongozo na kusimamia fedha za mpango wa malipo ya matokeo ya ufanisi wa kazi kwenye maeneo yao (RBF)ili kuboresha huduma za afya.
Aidha amewaasa watumishi hao kuachana na tabia ya kuingiza siasa kwenye majukumu yao hali inayosababisha kukwama kwa jitihada za kuleta mabadiliko katika sekta hiyo.
Njwayo ,amekemea baadhi ya wauguzi hasa wodi ya uzazi ambao wamekuwa wakiwatolea lugha zisizoridhisha na maneno machafu akinamama wanaokwenda kujifungua.
Mkuu huyo wa wilaya ,amemtaka na kaimu mganga mkuu wa wilaya ya Rufiji Didas Asenga,kusimamia maagizo  na maelekezo hayo aliyoyatoa pamoja na kuhakikisha afisa afya anaongeza kasi ya kuweka mazingira safi kwani maeneo mengi hususan baadhi ya zahanati,usafi hauridhishi.
Aliyasema hayo wakati wa ziara yake aliyoianza kutembelea  vituo vya afya na zahanati 28 zilizopo wilayani Rufiji ,kufuatilia fedha za awali zilizotolewa katika mpango wa RBF kiasi cha sh .mil.10 kila zahanati .
Njwayo alisema, wizara imeleta mpango huo kwa dhamira njema lakini amegundua kuna changamoto kubwa kwa baadhi ya zahanati kushindwa kufuata maelekezo na miongozo waliyopatiwa.
“Lipo tatizo la kutofuata maelekezo ya mradi suala litakalosababisha kukosa fedha nyingi kwa ajili ya mradi endapo asilimia zao hazijafikia, wanajipotezea point.”alisema
Hata hivyo alisema,hatua inayofuata baada ya kutolewa mil.10 ni kuongezwa fedha kila zahanati kulingana na kiwango cha malipo ya ufanisi zilizoonekana .
“Nimeanza ziara yangu leo,na nimepitia zahanati ya Tapika ambayo katika ukaguzi uliofanywa na maofisa wa mradi wametoa asilimia 49,Ngarambe asilimia 29,Kingupira 24,Utunge 20 na zahanati ya Chumbi imejitahidi imepata asilimia 75”alifafanua Njwayo.
Njwayo alieleza ,atakaezembea atachukuliwa hatua kwani mradi ulipoanza walipewa miongozo na maelekezo kama hawayafuatilii ina maana wanakiuka kwa makusudi.
Aliwataka wafanyakazi wa zahanati na vituo vya afya kujenga umoja na ushirikiano na kamati za afya ili kamati ziache kujisahau  kushirikisha na jamii kwa kuitisha mikutano kuwaeleza masuala ya afya na umuhimu wa  bima za afya .


Akizungumzia maadili kwa watumishi wa afya,Njwayo alisema,lazima kuheshimu wagonjwa na kutoa kauli za staha na kuwa wasiri pasipo kutoa aibu za wagonjwa mitaani.


Alisema sio utaratibu wa namna ya kutibia wagonjwa na kama kuna mtumishi atabainika kukiuka hayo atamchukulia hatua za kimaadili.


Kwa upande wake kaimu mganga mkuu wilaya ya Rufiji,Didas Asenga ,alisema amepokea maagizo na maelekezo yote aliyopatiwa.
Anasema mpango wa malipo kwa ufanisi umeleta matokeo chanya kwani awali zahanati nyingi zilikuwa na miundombinu chakavu,nyingine zilikuwa hazina vyoo,uhaba wa madawa,kukosekana vichomea taka lakini kwa sasa baada ya kupatiwa mil.10 kwa kila zahanati imeweza kuboresha huduma hizo.
Asenga alielezea,zipo changamoto zinazojitokeza ikiwemo baadhi ya zahanati kukosa uelewa wa hatua za manunuzi na mahesabu .
Alisema ,kunahitajika wahasibu wasaidizi katika kila zahanati ili kusimamia fedha zijazo na kuweka kumbukumbu kitaalamu na hatimae kuondokana na mapungufu yaliyopo.
Asenga alibainisha,mafunzo na elimu ya kutosha inahitajika kwa wakuu wa vituo vya afya ili kupunguza matatizo hayo.

Nae mwenyekiti wa kijiji cha Nyamwage ,Ibrahim Said alisema mpango huo ni mzuri kwakuwa umeweza kuimarisha huduma ya afya kwa jamii.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania