CURRENT NEWS

Saturday, September 23, 2017

DC SHINYANGA AANZISHA KAMPENI YA UPANDAJI MITI 'SHINYANGA MPYA,MTI KWANZA'


Mkuu wa mkoa wa Shinyanga,Zainab Telack akizindua kampeni ya upandaji miti ya ‘Shinyanga Mpya,Mti Kwanza’ leo Septemba 23,2017-Picha na Kadama Malunde - Malunde1 blog
*****
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Josephine Matiro ameanzisha kampeni ya upandaji miti yenye kauli mbiu ya ‘Shinyanga Mpya,Mti Kwanza’ ili kuboresha mazingira na kupambana na mabadiliko ya tabia nchi yanayosababisha jangwa katika wilaya hiyo. 
Kampeni hiyo imezinduliwa leo Jumamosi Septemba 23,2017 katika manispaa ya Shinyanga na Mkuu wa mkoa wa Shinyanga,Zainab Telack kwa lengo la kuboresha mazingira ya mji wa Shinyanga,maeneo ya taasisi,maeneo ya wazi,maeneo yanayozunguka kaya,kandokando ya barabara na sehemu zingine ambazo hazina miti. 
Akizindua kampeni hiyo,Telack alisema kutokana na mvua haba katika mkoa wa Shinyanga, kumekuwepo na mabadiliko ya tabia nchi hali inayosababisha kuwepo na hali ya jangwa. 
Telack aliwataka wananchi na wadau wote kuhakikisha wanatunza miti hiyo na kuzuia mifugo kuzurura ovyo mitaani. 
“Tutakuwa wakali,kuanzia sasa ni marufuku kwa mifugo kuzurura mitaani,ikikamatwa kwa kila mfugo faini ni kati ya shilingi 50,000/= na 100,000/=,iwe ng’ombe,mbuzi,kondoo au punda, tukikuta mti umekauka faini ni shilingi 50,000/=”,alieleza mkuu huyo wa mkoa. 
Naye Mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Josephine Matiro alisema uzinduzi wa kampeni hiyo umeanza na barabara 25 za mji wa Shinyanga ambapo jumla ya miti 3000 imepandwa na ofisi zote kata 17 za manispaa ya Shinyanga zitaendelea kutekeleza zoezi hilo. 
“Kampeni hii ni kwa wilaya ya Shinyanga,leo tumeanza katika manispaa ya Shinyanga,tunataka wilaya yetu iwe na mandhari nzuri ya kuvutia,ardhi iboreke,tuzuie upepo mkali katika majengo,tuhifadhi vyanzo vya maji,kuongeza vivuli katika maeneo ya kupumzikia,kujinasua na athari za mabadiliko ya tabia nchi lakini pia jamii itanufaika na miti ya matunda itakayopandwa”,alifafanua Matiro. Alibainisha kuwa ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi,sasa wilaya hiyo imekuja na teknolojia rahisi ya kumwagilia miti kwa njia ya matone,teknolojia ambayo inatumia maji kidogo lakini inaweza kumwagilia miti mingi na kwa muda wote.
“Tumekuwa tukipanda miti kila mwaka lakini miti hii ilikumbwa na changamoto nyingi wakati wa usimamizi na kusababisha miti mingi kufa,kwa sasa tumekuja na mpango huu mpya wa kupanda miti itayosimamiwa na wananchi na wadau wote”,alieleza Matiro. 
Alisema kauli mbiu hiyo ya Upandaji miti ya ‘Shinyanga Mpya,Mti Kwanza’ ina maana ya kuwaasa watu wote wa Shinyanga kuachana na tabia ya kuharibu miti na hivyo wahifadhi miti. 
“Tutatekeleza kampeni hii katika halmashauri zote,kila halmashauri itaanzisha kitalu na kuzalisha miche isiyopungua 25,000,kila kata ipande miti isiyopungua 1000 na iwe na kitalu cha kudumu,ofisi za mitaa na vijiji miti 100,vitongoji miti 50,kila mwananchi miti isiyopungua mitatu na taasisi zote zipande miti”,alifafanua Matiro.
Aliongeza kuwa ili kufanikisha kampeni hiyo,taasisi mbalimbali zitachangia mbegu,miche na kupanda miti ili kufikia lengo la kupanda miti isiyopungua milioni 1,500,000 kwa mwaka.
ANGALIA PICHA ZA MATUKIO HAPA CHINI
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga,Zainab Telack akizungumza wakati wa kuzindua kampeni ya upandaji miti ‘Shinyanga Mpya,Mti Kwanza’ leo katika ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Shinyanga.Kushoto ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga,Geofrey Mwangulumbi.
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga,Zainab Telack akiteta jambo na Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Josephine Matiro wakati wa uzinduzi huo. 
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Josephine Matiro akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo ya upandaji miti ambapo alisema miongoni mwa malengo yake ni kuhifadhi ardhi na kuiongezea thamani,kuzuia mmomonyoko wa adhi na kuboresha mazingira
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Josephine Matiro akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo.Alieleza kuwa kila kiongozi akialikwa kwenye tukio lolote,kabla ya shughuli ni vyema kwanza apande mti.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Josephine Matiro akisisitiza kuwa kampeni hiyo inalenga kujinasua na athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Wananchi wakiwa wameshikilia vijiti vinavyotumika katika zoezi la upandaji miti.
Uzinduzi unaendelea
Mdau wa Mazingira Ezra Manjerenga akieleza namna ya kupanda miti hiyo.
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga,Zainab Telack akipanda mti nje ya ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Shinyanga.
Wananchi wakishuhudia mkuu wa mkoa wa Shinyanga,Zainab Telack akipanda mti.
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga,Zainab Telack akichomeka vijiti kwenye mti aliopanda.
Meneja wa Benki ya CRDB,Said Pamui akipanda mti nje ya ofisi ya mkuu wa wilaya ya Shinyanga wakati wa uzinduzi wa kampeni ya upandaji miti 'Shinyanga mpya,mti kwanza'.
Wafanyakazi wa benki ya CRDB na wananchi wakishuhudia Meneja wa Benki ya CRDB,Said Pamui akipanda mti.
Meneja wa Benki ya CRDB,Said Pamui akishindilia udongo kwenye mti alioupanda.
Wananchi wakitoka katika ofisi ya mkuu wa wilaya ya Shinyanga wakielekea kwenye barabara mbalimbali mjini Shinyanga kwa ajili ya kupanda miti.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Josephine Matiro akiweka udongo kwenye mti alioupanda nje ya ofisi ya CCM wilaya ya Shinyanga Mjini.
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga,Zainab Telack akiwa katika ofisi ya CCM wilaya ya Shinyanga mjini.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Josephine Matiro akichimba shimo kwa ajili ya kupanda mti katika barabara ya Hospitali ya mkoa wa Shinyanga.
Mwananchi akifurahia baada ya kumaliza kupanda mti katika Barabara ya Shinyanga - Mwanza.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania