CURRENT NEWS

Saturday, September 2, 2017

DEREVA AKUTWA NA MISOKOTO MITANO YA BANGI NA POMBE AINA YA SAFARI-RPC SHANNA

Kamanda wa Polisi Mkoani Pwani (ACP)Jonathan Shanna ,akionekana akizungumza jambo (picha na Mwamvua Mwinyi) 
Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
JESHI la polisi mkoani Pwani,linamshikilia dereva wa gari lenye namba za usajili T .235 DET aina ya Mitsubishi Fuso,Yusuph Saidi,ambae amesababisha ajali kutokana na kudaiwa kutumia kilevi kilichofikia kiwango cha 105 kinyume na sheria.
Dereva huyo ,amesababisha kutokea kwa ajali ,na kupoteza maisha ya mtu mmoja na wengine 14 kujeruhiwa.
Ajali hiyo imetokea ,eneo la Ujenzi Kibaha barabara kuu ya Morogoro baada ya gari hiyo kugonga basi dogo la abiria aina ya Toyota Coaster lenye namba za usajili T. 198 BMG lililokuwa likiendeshwa na Masumbuko Zakaria na kusababisha kifo cha abiria wa coaster.
Akizungumzia kuhusiana na tukio hilo,mjini Kibaha kamanda wa Polisi mkoani Pwani (ACP)Jonathan Shanna alimtaja abiria aliyefariki dunia ni Janeth Jackson (40) mkazi wa Mlandizi .
Alisema kuwa, majeruhi wamelazwa kwenye hospitali ya rufaa ya mkoa wa Pwani Tumbi.
Alieleza, baada ya kutokea ajali hiyo dereva huyo alikamatwa na kukutwa na misokoto ya bangi mitano katika gari lake.
Kwa mujibu wa kamanda Shanna, walikuta pia chupa ya maji iliyowekwa pombe aina ya safari na alipopimwa alikutwa na kilevi 105 tofauti na kilevi cha kawaida 20.

Alisema kuwa kilevi zaidi ya 20 dereva haruhusiwi kuendesha gari kwani usalama unakuwa ni mdogo na inaonekana dereva Saidi alitumia vilevi vyote hivyo ikiwemo bangi na pombe aina ya safari.

Kamanda Shanna ,alibainisha ,wanamfikisha mahakamani na ameomba mahakama imchukulie hatua kali dereva huyo ikiwa ni pamoja na kumfutia leseni yake .
Alisema hatotakiwa aendeshe magari kutokana na matumizi makubwa ya ulevi na itakuwa fundisho kwa madereva wengine wasiofuata sheria.
Kamanda huyo alitoa rai kwa madereva kufuata sheria za usalama barabarani bila ya kushurutishwa kwani jukumu la usalama wa abiria liko mikononi mwao.
Kwa mujibu wa sheria nchini Tanzania kiwango cha ulevi kwa dereva kinachoruhusiwa ni 0.08,wakati kwa nchi ya Zambia ni 0.2 na duniani ni 0.05 .


Kiwango kinachoruhusiwa kwa dereva wa Tanzania bado ni kikubwa hivyo kuna kila sababu ya kufanyiwa marekebisho ili kupunguza ajali zembe.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania