CURRENT NEWS

Wednesday, September 27, 2017

JAFO AELEKEZA KAMPENI YA ONDOA ‘ZERO’ KISARAWE


Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo akizungumza katika Mahafali ya kidato cha nne katika shule ya sekondari Maneromango wilayani Kisarawe.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo akiwa na baadhi ya madiwani katika ukaguzi wa vyumba vya hoteli ya kisasa iliyojengwa kwenye shule ya sekondari Maneromango.

Wanafunzi wa kidato cha nne katika sekondari ya Maneromango wakiimba katika mahafali ya kuwaaga walimu na wanafunzi wenzao.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo akikagua bweni la wasichana wa kidato cha tano lililojengwa katika sekondari ya Maneromango.

Wanafunzi wa kidato cha tano waliojiunga mwaka huu katika sekondari ya Maneromango.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo akiwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kisarawe Hamisi Dikupite na Katibu wa Mbunge Halfani Sika wakikagua maktaba mpya ya kisasa iliyojengwa katika sekondari ya Maneromango.

Baadhi ya walimu wakuu wa sekondari mbalimbali katika wilaya ya Kisarawe wakisikiliza maelekezo yaliyokuwa yakitolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo.
.........................................................................
MBUNGE wa Jimbo la Kisarawe ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Mhe. Selemani Jafo amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kisarawe kuanza mchakato wa kuwaweka wanafunzi wa kidato cha nne katika kambi maalum ya masomo kwa ajili ya kujiandaa na mitihani.

Kambi hizo zinatakiwa kuwekwa katika shule zao kuanzia Oktoba mosi mwaka huu hadi pale watakapomaliza mitihani yao ya kidato cha nne mnamo Novemba 19, 2017.

Jafo ameazimia Kampeni hiyo leo alipokuwa mgeni rasmi katika sherehe ya mahafari ya  kidato cha nne katika sekondari ya Maneromango iliyopo wilayani kisarawe. 

Amesema lengo la kufanya hivyo ni kupata muda wa kutosha kujisomea ili kuondoa tatizo la ufaulu usio ridhisha jimboni humo. 

Naibu Waziri Jafo ameipa Kampeni hiyo jina la Ondoa ZERO Kisarawe ambapo itagusa shule zote za kata zilizomo wilayani humo ambapo wanafunzi watakula na kulala, na  kufanya mazoezi mbalimbali ya masomo ili kuwajengea uwezo wanafunzi hao kabla ya kuanza mitihani yao.


Katika kufanikisha zoezi hilo, Jafo amewaagiza viongozi wote wa wilaya ya Kisarawe kuandaa harambee maalum kwa kuwashirikisha ya wadau mbalimbali wa maendeleo wa Kisarawe.

kampeni hiyo inahitaji wastani wa shilingi milioni 50 kwa ajili ya wanafunzi 669 wa kidato cha nne watakaokuwa kambini.

Kadhalika, Harambee maalum ya wadau inatarajiwa kufanyika Oktoba 7, mwaka huu.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Jafo amewapongeza viongozi wote wa kisarawe pamoja na wananchi wa Maneromango kwa kufanikisha ujenzi wa mabweni mapya mawili, maktaba, madarasa, pamoja na matundu ya vyoo kumi shule hapo baada ya serikali kupeleka kiasi cha shilingi milioni 259.


 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania