CURRENT NEWS

Tuesday, September 5, 2017

MADEREVA WANAOKATISHA RUTI (KULA CHAPATI)KUKIONA -RPC SHANNA

Na Mwamvua Mwinyi ,Pwani

MADEREVA wa mabasi ya abiria ,yanayotumia barabara kuu ya Morogoro na kupitia wilaya za mkoa wa Pwani wameonywa kuacha tabia ya kukatisha ruti maarufu "KULA CHAPATI".

Aidha katika kupambana na ajali za barabarani ,jeshi la polisi mkoani Pwani limeongeza wakaguzi wa magari ili kuhakikisha hakuna gari linaloweza kupita mkoani hapo bila kukaguliwa .

Kamanda wa Polisi mkoani humo kamishna msaidizi wa polisi ,Jonathan Shanna alitoa onyo hilo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu masuala ya usalama barabarani na kupewa taarifa ya kuwepo kwa baadhi ya madereva ambao hukatisha ruti hasa eneo la Kongowe .

Alisema kitendo cha madereva hao kukatisha ruti ,ni kosa kisheria kwani atakaebainika anaweza kunyang'anywa leseni yake.

"Mabasi yote yanajulikana lipi linakwenda eneo gani na kuishia safari yake wapi ,kuna yanayotoka Mbezi -Mlandizi ,Mbezi -Tumbi ,Mbezi -Kongowe lakini unakuta yanayokwenda Mlandizi hayafiki na kuishia Kongowe "

"Eneo la Kongowe limekubuhu kwa madereva kugeuza magari yao na kushindwa kuwafikisha abiria eneo husika ,naagiza waache mara moja,"alisema kamanda Shanna.

Kamanda Shanna ,aliwataka abiria kuwa na ushirikiano wa kutoa taarifa polisi mara wanapoona wanawashushwa kubadilishwa kwenda kwenye bus jingine ili gari walilopanda ligeuze kabla ya kufika safari .

Alieleza hata yeye mwenyewe ataweza kwenda eneo ambalo litatajwa kuna katabia hako ili kuwachukulia hatua madereva wazembe .

Alitoa rai kwa madereva wenye tabia hiyo kuacha mara moja kusumbua abiria kwa kuwabadili kwenye mabus mengine njiani .

Hata hivyo ,kamanda Shanna alisema wameongeza pia idadi ya askari wa usalama barabarani kwenye barabara zote zinazounganisha mkoa huo na mikoa jirani ,;" Kutoa elimu kwa madereva bodaboda kuhusu kuchukua tahadhari lengo likiwa ni kuufanya mkoa uwe eneo salama kwa watumiaji barabara.

Alifafanua kwamba ,Pwani bila ajali za barabarani inawezekana ikiwa wote kwa ushirikiano watapaza sauti kufichua madereva wanaokiuka sheria .

Kamanda wa usalama barabarani mkoani Pwani,Abdi Issango ,alisema ,wanaimarisha matumizi ya speed radar ,vipima ulevi ,na kuhakikisha madereva wanaopatikana na makosa hayo wanafikishwa mahakamani .

Issango alibainisha kwasasa ,wanaendelea kusimamia kwa karibu mfumo wa utoaji leseni ili kila atakayepata leseni awe amepitia chuo cha udereva na kufaulu .

 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania