CURRENT NEWS

Thursday, September 7, 2017

MAKAMU WA RAIS AZINDUA KONGAMANO LA KIMATAIFA LA KISWAHILI NA MIRADI YA KUIMARISHA ELIMU MKOA WA KUSINI

unnamed


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia wakati wa uzinduzi wa Kongamano la kwanza la Kimataifa la Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki lililobeba mada isemayo Kuleta Mabadiliko katika jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kutumia Kiswahili lilianza leo mjini Unguja, Zanzibar.
5
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akikata utepe kuashiria kuzinduliwa kwa ofisi ya Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki mjini Zanzibar
16
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Balozi wa Japan nchini Mhe. Masaharu Yoshida wakipeana ishara ya kushukuru mara baada ya Balozi wa Japan kukabidhi miradi miwili mikubwa,mmoja ukiwa ni ujenzi wa uzio wa shule ya Msingi ya Muyuni na wa pili ni mradi wa uboreshaji  wa mazingira ya elimu katika wilaya ya ya kusini uliojumuisha ujenzi wa shule ya awali katika kijiji cha Kajengwa na Ukumbi wa Skuli ya Sekondari Kizimkazi.
17
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Balozi wa Japan nchini Mhe. Masaharu Yoshida wakikata utepe kama ishara ya kufungua Ukumbi wa Skuli ya Sekondari ya Kizimkazi.
24
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimuelezea  Balozi wa Japan nchini Mhe. Masaharu Yoshida namna Pomboo wanavyovutia utalii katika mkoa wa kusini wakati akimkabidhi zawadi ya sanamu ya Pomboo mara baada ya ufunguzi wa Ukumbi wa Skuli ya Sekondari ya Kizimkazi.
Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais
…………………………..
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi wa mkoa wa Kusini Unguja kutunza miradi na kuitumia kwa manufaa ya wote.
Makamu wa Rais aliyasema hayo leo wakati wa Ufunguzi wa Ukumbi wa Skuli ya Sekondari ya Kizimkazi ambao umefadhiliwa na Ubalozi wa Japan.
Mhe. Samia aliwashukuru Ubalozi wa Japan kwa kufadhili ujenzi wa Uboreshaji wa Mazingira ya Elimu katika Wilaya ya Kusini ambao umegharimu dola za kimarekani  laki moja na elfu kumi na mbili  na mia nane na arobaini na tano (112,845) ambazo ni sawa na takribani ya shilingi milioni mia mbili arobaini na saba (247) .Awali Ubalozi wa Japan ulitoa dola za Kimarekani elfu ishirini na nane mia nane na sitini (28,860) takribani shilingi milioni sitini na moja za kitanzania kujenga uzio wa shule  ya Msingi Muyuni .
Makamu wa Rais alimshukuru sana Balozi wa Japan kwa ufadhili huo ambao umeendelea kuimarisha urafiki na mahusiano kati ya nchi mbili hizi, aliwataka wananchi wa Wilaya ya Kusini kutilia mkazo masuala ya elimu na  kutunza miradi yote ili inufaishe na vizazi vijavyo.
Makamu wa Rais pia aliwapongeza viongozi wa halmashauri ya wilaya ya kusini kwa kusimamia vizuri fedha za ufadhili na kufanikisha kukamika kwa ujenzi wa miradi kama ilivyopangwa na kukamilika mapema zaidi .
Kwa Upande wake Balozi wa Japan nchini Mhe. Masaharu Yoshida alisema amefurahishwa  na Ushirikiano  alioupata kutoka kwa Makamu wa Rais na wakazi wa Wilaya ya Kusini Unguja na kuahidi kwamba Japan itaendelea kusaidia maendeleo ya Tanzania ambapo alisema ufunguzi wa miradi ya leo ni hatua nyingine kubwa ya kuimarisha  ushirikiano mzuri uliopo baina ya nchi mbili hizi, Japan na Tanzania.

Wakati huo huoMakamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan leo amezindua Mpango Mkakati wa Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki 2017-2022 wakati wa Kongamano la Kwanza la Kimataifa  la Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki ambapo aliwataka Viongozi wan chi za jumuiya hiyo kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha matumizi ya lugha ya Kiswahili kwani lugha hii inatuunganisha watu wa Afrika Mashariki, pamoja na kuzindua rasmi pia Makamu wa Rais alifungua Ofisi ya Kamisheni ya Kiswahili  ya Afrika Mashariki mjini Unguja, Zanzibar.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania