CURRENT NEWS

Friday, September 8, 2017

MFUMUKO WA BEI WA TAIFA KWA MWEZI AGOSTI 2017 UMEPUNGUA HADI KUFIKIA ASILIMIA 5.0


 Mkurugenzi wa Takwimu za Jamii na Sensa ya Watu na Makazi Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Ephraim Kwesigabo, akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo kuhusu kupungua kwa mfumuko wa bei. Kulia ni Kaimu Meneja wa Ajira na Takwimu za Bei Ruth Minja 


Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali wakichukua taarifa hiyo.

Na Dotto Mwaibale

MFUMUKO wa Bei wa Taifa kwa mwezi Agosti 2017 umepungua zaidi hadi kufikia asilimia 5.0 ikilinganishwa na asilimia 5.2 ilivyokuwa mwezi Julai2017.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Takwimu za Jamii na Sensa ya Watu na Makazi Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Ephraim Kwesigabo wakati akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo.

Alisema hii inamanisha kuwa kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti ,2017 imepungua zaidi ikilinganishwa na kasi ilivyokuwa kwa mwaka ulioishia mwezi Julai,2017.

"Fahirisi za Bei zimeongezeka hadi 108.46 mwezi Agosti, 2017 kutoka 103.28 mwezi Agosti, 2016" alisema Kwesigabo.

Kwesigabo alisema Mfumuko wa Bei wa Bidhaa za Vyakula na vinywaji baridi kwa mwezi Agosti, 2017 umepungua hadi asilimia 8.6 kutoka asilimia 8.9 ilivyokuwa mwezi Julai, 2017.

Akizungumzia mfumuko wa bei kwa kipimo cha mwaka kwa bidhaa za vyakula nyumbani na migahawani kwa mwezi Agosti,2017 umepungua hadi asimilia 9.1 kutoka asilimia 9.3 mwezi Julai 2017. Ambapo badiliko la Fahirisi za bei zisizo za vyakula umebaki kuwa asilimia 3.1 mwezi Agosti, 2017 kama ilivyokuwa mwezi Julai, 2017.

Kwesigabo aliongeza kuwa mfumuko wa bei ambao haujumuishi vyakula na nishati kwa mwezi Agosti, 2017 umepungua hadi asilimia 1.8 kutoka asilimia 2.2 Julai, 2017.

Alisema Fahirisi inayotumika kukokota aina hii ya mfumuko wa bei haijumuishi vyakula vinavyoliwa nyumbani na migahawani, vinywaji baridi, petroli, dizeli, gesi ya kupikia, mafuta ya taa, mkaa kuni na umeme.

Alisema vyakula na bidhaa za nishati vinasifa ya kuwa na bei ambazo hubadilika mara kwa mara, hivyo vikiondolewa kwenye fahirisi ya bidhaa na huduma zote hubakia fahirisi ambayo ina mwelekeo imara kwa watunga sera.


 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania