CURRENT NEWS

Wednesday, September 13, 2017

NHIF YAWAPIGA MSASA WAANDISHI WA HABARI PWANI /WATAKIWA KUJIUNGA NA MFUKO HUO

 Baadhi ya waandishi wa habari mkoani Pwani wakiwa kwenye picha ya pamoja na wafanyakazi kutoka mfuko wa taifa wa bima ya afya mkoani humo.
 Katibu tawala wa Mkoa wa Pwani ,Zuberi Samataba wa kwanza kulia ,akizungumza katika mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari mkoani hapo yaliyoandaliwa na NHIF Mkoa wa Pwani, wa kwanza kushoto ni Meneja wa mfuko huo mkoani humo Fortunata Raymond 
MENEJA wa mfuko wa taifa wa bima ya afya (NHIF) mkoani Pwani ,Fortunata Raymond  ,akionekana kuzungumza jambo katika mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari mkoani hapo yaliyoandaliwa na mfuko huo  .(picha na Mwamvua Mwinyi)


Na Mwamvua Mwinyi ,Pwani
WAANDISHI wa habari ,hasa wasio na mikataba maalum katika vyombo vyao mbalimbali vya habari ,wametakiwa kujiunga na mfuko wa taifa wa Bima ya afya ili kujihakikishia usalama wa afya zao wawapo kazini .
Aidha endapo wakitumia kalamu zao kuelimisha makundi ya wajasiriamali ,wanafunzi wa vyuo ,watoto chini ya miaka 18,wafanyakazi viwandani,viongozi wa dini ,umuhimu wa kujiunga na bima ya afya itaongeza wigo wa watu kujiunga na huduma hiyo.
Rai hiyo ,imetolewa na katibu tawala wa mkoa wa Pwani ,Zuberi Samataba ,wakati akifungua warsha fupi kwa waandishi wa habari iliyoandaliwa na NHIF mkoani hapo .
Alisema tasnia hiyo inakumbana na hatari na kufanya kazi katika mazingira magumu ambayo yanahitaji kuwa na Bima .
Samataba alieleza ,wapo waandishi wa habari ambao ni vinara wa kuandika makala na kuelimisha kuhusu NHIF na CHF lakini wao wenyewe hawajajiunga .
Alibainisha ,mafunzo hayo yawe chachu cha mabadiliko kwao kuona Bima ya afya ni sehemu ya vitu muhimu katika maisha na kazi zao .

“Majukumu yenu yamezungukwa na mazingira magumu na hatarishi hivyo ni muhimu mjiunge na mfuko wa taifa wa bima ya afya ili kuwa na uhakika wa kutibiwa mahala popote pindi mnapopata tatizo”alisema Samataba.

Hata hivyo Samataba ,alieleza kutokana na mkoa wa Pwani kuendelea kutoa fursa nyingi za ajira kupitia sekta ya viwanda ni vema wafanyakazi hao wakajiunga na mfuko huo.


“Watumishi wa sekta binafsi nao wana fursa ya kujiunga ,inasaidia kuwa na uhakika wa kugharimia matibabu pale wanapoumwa na hata kama hawana fedha za matibabu ,” alisema .


Aliwahakikishia , serikali inazidi kuuboresha mfuko wa taifa wa bima ya afya ili wanachama wake wanapokwenda kutibiwa katika zahanati na vituo vya afya wasisumbuliwe wala kukosa dawa.
Samataba alisema kwa sasa serikali inafikiria kuwa na huduma ya afya kwa wote ambao kila mwananchi atalazimika kujiunga na huduma hizo.
Nae meneja wa mfuko wa taifa bima ya afya mkoa wa Pwani,Fortunata Raymond ,alisema warsha hiyo itawajengea uwezo waandishi wa habari hao kujua faida na manufaa ya bima za afya.
Alisema, wameanza utaratibu wa kuwaunganisha watoto walio chini ya umri wa miaka 18 kupitia mpango wa TOTO KADI.

Fortunata alielezea ,mpango huo ni wa gharama nafuu kiasi cha sh.50,400 pekee na mtoto huyo ataweza kupata huduma kokote nchini.

Pamoja na hayo ,alibainisha kwamba, sekta isiyo rasmi ikiwemo vibindo, saccos, amcos, vikoba na vikundi maalumu vya wajasiriamali vilivyosajiliwa nayo itanufaika .


“Utaratibu wa vikundi hivi unaitwa VIKOA ambapo vikundi vyenye mwelekeo wa kiuchumi vitapata fursa ya kujiunga ,hawatatumia fedha za mitaji yao kwa ajili ya kujitibia “alieleza Fortunata.

Fortunata alisema , mfuko huo zamani ulikuwa ukitoa huduma kwa watumishi wa serikali pekee lakini sasa wanategemea maboresho makubwa ili kufikia watanzania wengi.

Alisema wanatarajia kuongeza elimu kwa wadau ,kuboresha kitita cha mafao,usambazaji na utoaji huduma vijijini,kuimarisha usajili wa maduka ya dawa muhimu na utoaji wa vitambulisho vipya kwa wanachama.
Meneja huyo wa NHIF mkoani humo,alifafanua tangu waanze kutoa huduma hizo ndani ya jamii ni miaka 15 sasa na tayari kuna mafanikio makubwa hapa nchini.
Mwandishi wa habari wa gazeti la habari leo mkoani Pwani,John Gagarini ,alisema waandishi ambao hawana ajira za kudumu wamekuwa wakishindwa kujiunga tofauti na wale walioajiriwa wanaonufaika kwenye mikataba yao moja kwa moja.
Alisema utaratibu mpya wa VIKOA utawezesha waandishi ambao hawajajiunga na huduma hizo kujiunga kupitia vyama  vyao vya mikoa kwa gharama y ash.76,800 kwa kila mwanachama.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania