CURRENT NEWS

Friday, September 1, 2017

POLEPOLE: TUPO TAYARI KWA UCHAGUZI MDOGO JIMBO LA LONGIDO

Katibu Wa Halmashauri Kuu Ya Chama Cha Mapinduzi (NEC), Itikadi na Uenezi Ndg Humphrey Polepole akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Sekretarieti, Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam.
Waandishi wa habari wakimsikiliza kwa makini Katibu Wa Halmashauri Kuu Ya Chama Cha Mapinduzi (NEC), Itikadi na Uenezi Ndg Humphrey Polepole katika Ukumbi wa Sekretarieti, Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam.


Aliyekuwa mgombea Ubunge wa Jimbo la Longido kupitia Chama Cha Mapinduzi Dkt Steven Kiruswa akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Sekretarieti, Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam. Kushoto kwake ni Katibu Wa Halmashauri Kuu Ya Chama Cha Mapinduzi (NEC), Itikadi na Uenezi Ndg Humphrey Polepole

Na Mathias Canal, Dar es salaam

Chama cha Mapinduzi kimesema kuwa kipo tayari kuingia katika uchaguzi mdogo wa Ubunge Jimbo la Longido Mkoani Arusha mara baada ya kutangazwa kuwa jimbo hilo lipo wazi kutokana na maamuzi ya mahakama ya Rufaa iliyobainisha kuwa uchaguzi wa mwaka 2015 haukuwa huru na haki hivyo kufuta matokeo ya uchaguzi huo.

CCM imeeleza kuwa kulikuwa na matumizi yasiyostahili kutumika kujazwa matokeo ya Ubunge, kwa kutumia fomu namba 21c za kujaza matokeo ya Udiwani na kujaza matokeo ya Ubunge, badala ya kutumia fomu namba 21b jambo lililopelekea kufungua kesi ya kupinga ushindi wa Ubunge katika Jimbo hilo.

Kauli ya CCM imetolewa na Katibu Wa Halmashauri Kuu Ya Chama Cha Mapinduzi (NEC), Itikadi na Uenezi Ndg Humphrey Polepole wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Sekretarieti, Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam.

Polepole alisema kuwa vipo vyama vya siasa ambavyo kwa kawaida hulalamika kila vinaposikia kushindwa na mahakama kwa madai kuwa hakuna haki lakini vyama hivyo kila vinaposhinda vyenyewe husema mahakama imetenda haki.

Alisema kuwa kazi ya mahakama ni kutumia sheria zilizopo na kuamua juu ya malalamiko ya wananchi kwa kuhakikisha usawa mbele ya sheria kwa watu wote unatendeka hivyo maamuzi yaliyotolewa juu ya kuwa wazi kwa Jimbo la longido ni sehemu ya maamuzi huru na haki kwa mahakama ya Rufaa nchini.

Polepole alitoa Rai kwa mahakama zote nchini kuendelea kufanya kazi yake vizuri kwa uhuru na haki pasina kusikiliza kelele za watu wanaotaka mahakama kutekeleza matakwa yao kinyume na sheria za nchi.

Kwa upande wake aliyekuwa mgombea Ubunge wa Jimbo la Longido kupitia Chama Cha Mapinduzi Dkt Steven Kiruswa akizungumza katika mkutano huo na waandishi wa habari alisema kuwa pamoja na mapingamizi ya mara kwa mara katika kipindi chote tangu rufaa ilipoanza kusikilizwa aliamua kuwa mtulivu kwa kusubiri maamuzi yatakayotolewa na mahakama kama chombo huru nchini cha maamuzi.

Alisema kuwa kwa mara ya nne mahakama ya Tanzania imethibitisha kuwa inaongozwa kwa mujibu wa sheria na kujali haki ya mwenye haki ili isipotee bure.

Alisema CCM ilifungua kesi mwanzoni mwa mwezi Novemba 2015 ikiwa ni wiki mbili tangu kumalizika uchaguzi mkuu uliofanyika Octoba 25, 2015 ambapo mahakama kuu ya Arusha ilibaini kwamba uchaguzi haukuwa huru na haki na kufikia June 29, 2016 hukumu ikatolewa na ubunge kutenguliwa jambo ambalo liliwafanya Chadema kukata rufaa zaidi ya mara tatu.

Dkt Kiruswa alisema kuwa wananchi wa Longido wamenyanyasika katika kipindi cha miaka miwili pasina kuwa na muwakilishi wa kuwasemea bungeni hivyo maamuzi ya mahakama yataifanya Tume ya Uchaguzi kutangaza rasmi uchaguzi mdogo na hatimaye muwakilishi kupatikana kwa kura za haki.

Aidha, Polepole alisema kuwa Chama Cha Mapinduzi katika muktadha wa CCM mpya Tanzania Mpya kinaendelea kusisitiza siasa safi na kutoa uongozi bora.

Alisema siasa za kutumia lugha isiyofaa, na Siasa za aina yoyote zenye mtazamo wa fitina hazina nafasi ndani ya Chama Cha Mapinduzi katika kipindi hiki ambacho Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM Mhe Dkt John Pombe Magufuli anaongoza kwani amedhamiria CCM kuwa chama cha wananchi wote chenye mtazamo chanya katika uwajibikaji.

Alitoa Rai kwa vyama vingine nchini kufanya siasa za weledi pasina kutumia lugha za kuudhi dhidi ya serikali na wananchi wake huku akiahidi kuwa chama chake hakiwezi kupoteza muda kujibu porojo za hila kwani kitakuwa hakitendi haki katika kuisimamia ilani ya uchaguzi ya mwaka 2015-2020 kwa kuwaletea maendeleo endelevu wananchi.

Polepole alisema kuwa CCM inaamini katika majibizano ya hoja kwani chama hicho kina deni kubwa kwa wananchi la kuwaletea maendeleo hivyo viongozi wote wa chama na wale wenye dhamana katika dola kuendelea kuishi misingi ya CCM Mpya ya Uadilifu, Uaminifu, Uchapakazi, Vita dhidi ya Rushwa, Vita dhidi ya ubadhilifu wa mali za chama na mali za Umma, Unyenyekevu na kusikiliza watu.

MWISHO
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania