CURRENT NEWS

Saturday, October 28, 2017

DC MTATURU AZINDUA MSIMU WA KILIMO 2017/2018

Na Mathias Canal, Singida

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida Mheshimiwa Miraji Jumanne Mtaturu amezindua msimu wa kilimo 2017/18 ikiwa ni Sehemu ya kuwasihi wananchi kuanza kujiandaa kwani tayari wakati wa kuanza kilimo umekaribia.

Katika uzinduzi huo uliofanyika katika kijiji na kata ya Ihanja wilayani Ikungi Mhe Mtaturu pamoja na  mambo mengine lakini amewasihi kutumia vizuri mvua za mwanzo kupandia.

Katika mkutano huo wa uzinduzi  Mhe Mtaturu pia ameanzisha utaratibu huo wa kuzindua msimu wa kilimo kila mwaka ili kuwaandaa wakulima kuingia msimu mpya mapema ikiwemo kuyakumbusha makampuni ya mbegu kuwafikishia wakulima mbegu kabla mvua kuanza kunyesha.

Sambamba na utaratibu huo wa kuzindua msimu wa kilimo kila mwaka  pia kutakuwa na zoezi la kufanya maonesho ya zana na teknolojia mbalimbali za kilimo ili wakulima wapate muda wa kujifunza mbinu mpya za kilimo ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.

Mhe Mtaturu aliwaagiza maafisa ugani kuwa na mashaba darasa na madaftari ya wakulima sambamba na  kuwaunganisha wakulima hao na makampuni ya mbegu ili waweze kupanda mbegu bora zikiwemo zile zinazokomaa kwa muda mfupi.

Aliwakumbusha wakulima wote kulima mazao ya chakula ili kuwa na usalama wa chakula ambapo aliyataja mazao hayo ambayo yanastahili hali ya ukame kuwa ni pamoja na Mtama, uwele, Mpunga, viazi lishe,viazi vitamu na mihogo.

Pia aliwataka wakulima kulima mazao ya biashara ili kuwa na uchumi imara huku akitikisa msisitizo  zaidi katika mazao ya kipaumbele katika wilaya hiyo ambayo ni Korosho, Pamba na Alizeti.

Mhe Mtaturu aliwahakikishia wananchi kupanda mbegu mapema za korosho na dawa za kupulizia ili kuua vijijidudu vinavyoshambulia.

Alisma kuwa tayari Wilaya ya Ikungi imepokea Mbegu Tani 20 za Pamba ambazo zitaanza kusambazwa wiki ijayo kwa wakulima waliojiandikisha.

Akisoma taarifa ya idara ya kilimo kwa Mkuu wa Wilaya, Kaimu afisa kilimo Wilaya  ya Ikungi Ndg Teendwa Senkoro alieleza lengo la wilaya hiyo ku ni kulima hekta 124,038 za mazao mbalimbali katika msimu wa mwaka 2017/18 na kuvuna tani 208,700 za mazao mbalimbali.

Mhe Mtaturu ametimiza ahadi yake ya kuanzisha msimu wa kilimo aliyoahidi hivi karibuni wakati alipofanya kikao kazi na wakuu wa Idara na Vitengo

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Mhe Ally Mwanga alimpongeza Mhe Mtaturu kwa juhudi zake mbalimbali za kimaendeleo anazozifanya katika Wilaya hiyo tangu ateuliwe kuhudumu katika nafasi hiyo. 

Alisema kuwa waheshimiwa Madiwani na Halmashauri wataendelea kumuunga mkono katika jitihada hozo ili kuwasaidia wananchi kujiletea maendeleo.

 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania