CURRENT NEWS

Tuesday, October 3, 2017

DK.KIKWETE -NILIGUNDUA NA KIPAJI CHA KUCHEZA MPIRA WA KIKAPU NIKIWA SEKONDARI

Rais Mstaafu wa awamu ya nne  ,Dk.Jakaya Kikwete, akionekana pichani ,wakati akizungumza na viongozi mbalimbali wilayani Kibaha na Mkoa wa Pwani,walimu,wanafunzi na wazazi wa wanafunzi wa shule ya sekondari Kibaha,huko shirika la elimu Kibaha.(picha na Mwamvua Mwinyi)

Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha

RAIS mstaafu wa awamu ya nne ,Dk.Jakaya Kikwete ,amesema uwepo wa walimu maalum wa kufundisha  somo la michezo katika shule mbalimbali itasaidia kuibua vipaji kwa wanafunzi na kujenga afya zao .

Ameeleza vipo vipaji vingi vya michezo tofauti tofauti vilivyojificha mashuleni ambapo endapo vitaibuliwa vitawezesha kupata wana michezo bora watakaotumika kuliletea sifa Taifa .

Dk Kikwete aliyasema hayo shirika la Elimu Kibaha ,wakati akizungumza na wazazi ,wanafunzi ,walimu na viongozi mbalimbali ,katika shule ya sekondari Kibaha.

Alieleza ,shule ya sekondari Kibaha ndipo alipogundua na kuibua kipaji chake cha kucheza mpira wa kikapu .

"Nilikuwa nikitumainiwa na walimu wangu wa michezo ,ndio waligundua kipaji changu kipo kwenye mpira huo,nilikuwa nikitumainiwa na walimu wangu "

"Kama kuna mechi nje ya shule,sekondari ya Pugu ,Azania ilikuwa lazima niende ,nikiugua mwalimu wangu anasema haikubaliki ilikuwa lazima niende na tushinde ." alisema Dk.Kikwete .

Dk Kikwete alifafanua pia alikuwa bingwa wa riadha shuleni licha ya yeye kupenda mchezo wa mpira wa miguu .

"Nilikuwa nikipenda sana mpira wa miguu lakini kumbe kipaji changu kilikuwa kwenye basketball "; Hapa nachotaka kusema ni kwamba somo la michezo katika shule zetu litasaidia kuibua vipaji kwa watoto wetu" alisema .

Alielezea kwamba ,shule ya sekondari Kibaha ilikuwa ikiwika na kuongoza kwa michezo nchini .

Dk.Kikwete alisema ,shule hiyo ilikuwa ikitumika viwanja vyake vya michezo mbalimbali ,na kuwa na walimu maalum wa somo la michezo .

Alifurahi kusikia bado viwanja hivyo vinaendelea kutumika na kuwepo na walimu wa somo hilo lakini aliusihi uongozi wa shirika kusimamia suala la michezo shuleni humo .

Hata hivyo ,rais huyo mstaafu hajafurahishwa kusikia kuna upungufu wa vifaa vya michezo shule ya sekondari Kibaha jambo ambalo aliahidi kuangalia namna ya kusaidia vifaa hivyo  ili kurejesha sifa iliyokuwepo awali shuleni hapo .

Dk.Kikwete alisema ,mamlaka husika pia imesikia ,na itatatua changamoto hiyo .

Awali mwalimu mkuu wa shule ya sekondari Kibaha ,Chrisdom Ambilikile ,alisema shule inakabiliwa na upungufu wa vifaa vya kimichezo ikiwemo mipira ya michezo mbalimbali na sare .

 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania