CURRENT NEWS

Thursday, October 5, 2017

JAFO AZIAGIZA HALMASHAURI KUZUIA UVUJAJI MAPATO.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo akisisitiza jambo alipokuwa akikagua mfumo wa kielektroniki katika Kituo cha Afya Makole Manispaa ya Dodoma.

Wagonjwa wakiwa katika dirisha la malipo kwenye kituo cha Afya Makole Manispaa ya Dodoma.

Wagonjwa wakiwa katika dirisha la malipo kwenye kituo cha Afya Makole Manispaa ya Dodoma.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo akisalimia wagonjwa alipokuwa akikagua kituo cha Afya Makole Manispaa ya Dodoma. 
..................................................................................
NAIBU Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi) Selemani Jafo amefanya ziara leo ya kukagua utekeleza wa maagizo ya serikali aliyoyatoa hivi karibuni katika Kituo cha Afya Makole Manispaa ya Dodoma.

Pamoja na maagizo mengine, Jafo aliagiza kuhakikisha kituo hicho kinafunga mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji mapato.

Akiwa katika ziara yake leo, Jafo amepongeza ufungaji wa mfumo huo huku akiwataka kuhakikisha wanaziba mianya ya upotevu wa mapato kwa kuwa hali ya ukusanyaji bado hairidhishi.

Amesema kwa mujibu wa taarifa aliyoipata kituo hicho kabla ya mfumo kilikuwa kikikusanya Sh.Milioni nne lakini kwasasa kinakusanya hadi Sh.Milioni 9.9 kwa mwezi jambo ambalo linaonesha bado kuna mianya ya upotevu wa mapato.

“Nawapongeza kwa kutekeleza maagizo ya serikali kwa kufunga huu mfumo lakini sijaridhishwa na ukusanyaji mapato wa kiwango hichi, kuna vituo vinakusanya hadi Sh.Milioni 24 nyie mnakusanya hivi bado haitoshi hakikisheni mnaziba mianya,”amesema Jafo

Ameongeza  “Kuwepo na mfumo ni jambo moja na kuutumia mfumo ni jambo jingine jambo la msingi ni uaminifu kuna watu katika vituo vyetu uaminifu ni mdogo kwenye kukusanya fedha ndio ugomvi huwa unazuka na wakati mwingine watu wanatolewa kwa maslahi yao binafsi,”.

Amewataka kuhakikisha kunakuwepo na matumizi sahihi ya mfumo huo ili kuongeza mapato.

Akizungumzia kuhusu ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya nchini, Jafo amesisitiza Mamlaka za serikali za mitaa kuhakikisha zinasimamia kikamilifu ujenzi huo na ifikapo Desemba 30 mwaka huu uwe umekamilika.

Amesema hivi karibuni serikali imetoa Sh.Milioni 500 kwa kila kituo kimoja kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo jengo la upasuaji,maabara ya kisasa na wodi ya akina mama na watoto.

Naibu Waziri huyo amesema serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk.John Magufuli imedhamiria kuboresha huduma za afya na kwamba utoaji wa fedha huo umetokana na hali ya vituo vya afya kuwa si ya kuridhisha.

Amebainisha Dodoma ni eneo mkakati kutokana na wingi wa watu hivyo ni  lazima huduma za afya ziboreshwe ili kuondoa msongamano katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

Kwa upande wake, Katibu wa Afya wa kituo hicho, Habiba Thabiti amesema kabla ya kufungwa mfumo huo walikuwa wanakusanya Sh.Milioni nne kwa mwezi lakini kwasasa wamefikia Sh.Milioni 9.9.


Naye, Mganga Mfawidhi wa kituo hicho, Dk.George Matiko amesema kwa siku kituo kinahudumia wagonjwa kati ya 400-800 na akina mama wanaojifungua kwa mwezi ni 400.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania