CURRENT NEWS

Tuesday, October 3, 2017

MAKAMU WA RAIS AFUNGUA MAKUMBUSHO MAPYA OLDUVAI

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akikata utepe kuashiria ufunguzi wa Makumbusho mapya ya mambo ya kale katika bonde la Olduvai ndani ya hifadhi ya Ngorongoro, wengine pichani  ni Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Profesa Jumanne Maghembe (kushoto) pamoja na Mkuu wa mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo (kulia).
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akipata maelezo mbali mbali kuhusu maisha ya binadamu na wanyama wa kale kutoka kwa Mhifadhi wa Mambo ya Kale kutoka Makumbusho ya Taifa Dkt. Agness Gidna mara baada ya kufungua Makumbusho mapya ya mambo ya kale katika bonde la Olduvai ndani ya hifadhi ya Ngorongoro.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akiangalia mchoro wa Mambo ya Kale mara baada ya kufungua Makumbusho mapya ya mambo ya kale katika bonde la Olduvai ndani ya hifadhi ya Ngorongoro.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akiangalia uzinduzi wa tovuti na mtanzao wa bure wa Hifadhi ya Ngorongoro mara baada ya kufungua Makumbusho mapya ya mambo ya kale katika bonde la Olduvai ndani ya hifadhi ya Ngorongoro.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akihutubia mara baada ya kufungua kufungua Makumbusho mapya ya mambo ya kale katika bonde la Olduvai ndani ya hifadhi ya Ngorongoro.

                                  ............................................................ 
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi wanaoishi kwenye bonde la Ngorongoro kuwa mstari wa mbele katika kuhifadhi na kutunza mazingira ya bonde hilo ili liwe na manufaa kwa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.

Makamu wa Rais aliyasema hayo leo wakati wa ufunguzi rasmi wa Makumbusho mapya ya Olduvai - Ngorongoro.  Katika ufunguzi huo Makamu wa Rais pia alipata nafasi ya kuzindua tovuti maalum kuhusu masuala ya utalii katika bonde la Ngorongoro. “Ufunguzi huu ninaoufanya leo unaendana na malengo tuliyojiwekea ya kuongeza na kukuza vivutio vya utalii ili kuvutia wageni (watalii) wengi zaidi kutembelea nchi yetu” alisema Makamu wa Rais.

Akihutubia mamia ya wananchi waliojitokeza katika tukio la ufunguzi wa Makumbusho hayo, Mheshimiwa Makamu wa Rais alisema anatamani kuona kinachofanyika Ngorongoro kinafanyika pia katika maeneo mengine  yenye rasilimali za kihistoria kama vile mapango ya Amboni (Tanga), Michoro ya Miambani ya Kondoa (Dodoma), miji mikongwe ya Zanzibar, Bagamoyo, Kilwa Kisiwani na Songo Mnara.

Pia Mheshimwa Makamu wa Rais aliwaagiza viongozi wa Serikali, hususani Wizara ya Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii kutambua, kulinda, kuhifadhi na kuendeleza vivutio vyote vya kiutamaduni na kijiolojia vilivyopo nchini. “Nataka kuona shughuli za kiutalii zikiibuka katika ngazi ya wilaya kupitia Halmashauri zetu na ofisi za Wakuu wa Wilaya ili kuongeza ajira za vijana nchini” alisisitiza Makamu wa Rais.

Makamu wa Rais alitoa rai kwa wananchi wote wanaoshi pembezoni au karibu na rasilimali za kitamaduni kutunza rasilimali hizo muhimu kwa kufuata sheria na taratibu zilizopo. Makamu wa Rais alisema ”ninyi ni mashuhuda wazuri wa namna rasilimali hizi zilivyo muhimu kwa ustawi wa uchumi wenu, ajira mnazopata, heshima ya kutambuliwa utamaduni wenu kimataifa pamoja na fedha za kigeni zinazopatikana kupitia utalii unaotokana na rasilimali hizi ambazo husaidia kujenga huduma za kijamii kama vile mahospitali, mashule, barabara na miundombinu ya maji”.  Aidha alisisitiza kuwa serikali haitasita kuchukua hatua kali kwa viongozi wa serikali, wataalam na wananchi watakaosababisha uharibifu wa rasilimali muhimu kwa kutotekeleza majukumu yao sawasawa au kuvunja sheria na taratibu za uhifadhi wa rasilimali hizo.
Mwisho, Makamu wa Rais aliwashukuru wote waliohusika katika ujenzi wa Makaumbusho hii mpya na ya kipekee duniani hususan Umoja wa Ulaya ambao wamechangia kiasi kikubwa cha fedha za kukamilisha ujenzi huo.

Ufunguzi wa Makumbusho ya Olduvai uliohudhuriwa na Waziri wa Maliasili na Utalii Profesa Jumanne Maghembe(MB), Mkuu wa Mkoa wa Arusha  Mhe. Mrisho Gambo, Naibu Waziri wa Kilimo na Mifugo Mhe. Ole Nasha (MB), Balozi wa Umoja wa Ulaya na Balozi wa Hispania pamoja na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali. 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania