CURRENT NEWS

Wednesday, October 11, 2017

MGOMBEA EKURU AUKOT ARUHUSIWA KUWANIA URAIS KENYAMahakama Kuu nchini Kenya imeamuru mgombea urais wa chama cha Thirdway Alliance Ekuru Aukot aliyekuwa ameshiriki uchaguzi mkuu tarehe 8 Agosti ashirikishwe kwenye uchaguzi mkuu mpya unaopangiwa kufanyika tarehe 26 Oktoba.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi IEBC ilikuwa imetangaza kwamba ni wagombea wawili pekee, Rais Uhuru Kenyatta wa chama cha Jubilee na Raila Odinga wa muungano wa National Super Alliance (Nasa) wangewania kwenye uchaguzi huo.
Bw Odinga alijiondoa kwenye uchaguzi huo Jumanne.
Dkt Aukot amesema amefurahia uamuzi huo na kwamba sasa watakuwa kwenye uchaguzi kwani mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alikuwa amejaribu kuwafungia nje
Hata hivyo, amesema chama chake bado kina masuala ambayo kilitaka yashughulikiwe na tume hiyo ya uchaguzi tangu mwezi Agosti na bado hayajashughulikiwa.
Amesema kukubaliwa kwao kuwania kutawafungulia mlango kufanya mashauriano na viongozi wa IEBC.
Dkt Aukot amesema chama chake kitatoa maelezo ya kina kuhusu msimamo wao katika kipindi cha siku mbili hivi baada ya mashauriano zaidi.
Maafisa wakuu wa IEBC walikutana jana kutafakari kuhusu hatua za kuchukua baada ya hatua ya Bw Odinga lakini kufikia sasa bado hawajatoa tamko.
Kujumuishwa kwa mgombea huyo kuna maana kwamba IEBC haiwezi kumtangaza Bw Kenyatta kuwa mshindi wa moja kwa moja hata baada ya kujiondoa kwa Bw Raila.


 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania