CURRENT NEWS

Tuesday, October 3, 2017

MSANII IZZO BIZNESS WA TANZANIA NA AVRIL WA KENYA WAPAMBA ONYESHO LA COKE STUDIO

Wapenzi wa muziki wa kizazi kipya nchini wanaendelea kupata burudani ya muziki kutoka wasanii nguli kutoka nchi za Afrika kupitia onyesho la Coke Studio kupitia luninga ya clouds ambapo mwishoni mwa wiki Kolabo ya mwanamuziki kutoka nchini Izzo Business na Avril kutoka Kenya imeacha gumzo kubwa. Wanamuziki wengine waliopagawisha washabiki wa muziki katika onyesho hilo ni Mafizikolo kutoka Afrika ya Kusini kwa kushirikiana na msanii Nyashinski kutoka nchini Kenya na wasanii waalikwa Bill Nas (Tanzania),Sheebab (Uganda) na Asgeg Ashko (Ethiopia). Akiongea juu ya kolabo hili,Izzo Business alisema amefurahi kushirikiana na Avril kimuziki hususani wimbo walioimba pamoja unaojulikana kama 'Kanyonyi Kanja' na 'mabata mabata yanaogelea' ambao umeimbwa kwa lugha ya Kiswahili ukiwa na vionjo vya muziki wa bongofleva. Kupitia onyesho hili la Coke Studio linaloandaliwa na kampuni ya Coca Cola muziki wa Tanzania unazidi kutangazwa ikiwemo vipaji vya wanamuziki kutoka hapa nchini ambao wanashirikiana na wenzao kutoka Afrika na linarushwa kwenye luninga kwenye nchi zaidi ya 50. Wasanii wa Tanzania waliopo katika onyesho la Coke Studio msimu huu ni Ali Kiba, Rayvanny, Izzo Bizness, Nandy na mtengenezaji wa muziki wa studio nguli Nahreel. Wakitoa maoni yao kuhusiana na onyesho hili,baadhi ya wapenzi wa muziki kutoka mikoa mbalimbali wanaolifuatilia walisema kuwa burudani za Coke Studio msimu huu ni moto wa kuotea mbali kwa kuwa kolabo za wanamuziki zimetengenezwa kwa ustadi mkubwa kiasi kwamba zikionyeshwa zinaleta furaha na kumfanya mtazamaji kujiona anaangalia onyesho la wanamuziki hao mubashara (Live).
Mbali na wasanii wa Tanzania,wasanii msimu huu wa tano wa Coke Studio unawajumuisha wasanii kutoka katika nchi za Kenya, Uganda, Rwanda, Ethiopia, Nigeria, Ghana, Angola, Zimbabwe, Afrika Kusini, Togo, Cote d’Ivoire, Madagascar, Mauritius, Mozambique, DRC na Cameroon Baadhi ya wasanii hao ni Khaligraph Jones na Band Becca (Kenya), Sami Dan (Ethiopia), Bebe Cool, Eddy Kenzo, Sheebah, Ykee Benda ( Uganda). Wengine ni Nasty C, Busiswa, Mashayabhuqe kutoka Afrika ya Kusini, Youssoupha kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Runtown na Yemi kutoka Nigeria, Dji Tafinha kutoka Angola, Laura Beg kutoka Mauritius, Jah Prayzah na Slapdee kutoka Central Africa Republic, Bisa Kdei na Worlasi kutoka Ghana. Tangia onyesho hili lianzishwe limekuwa kiungo kikubwa cha kuwakutanisha wanamuziki wa Afrika kufanya kazi kwa pamoja na kupiga muziki wenye vionjo kutoka sehemu mbalimbali za Afrika ikiwemo kuleta burudani kubwa kwa washabiki wa muziki wa kiafrika na kuwaunganisha waafrika hususani vijana kupitia muziki.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania