CURRENT NEWS

Monday, October 23, 2017

MWENYEKITI WA KITONGOJI AVULIWA UONGOZI NA WANANCHI MWINGINE AJIUZULU MBELE YA DC MTATURU


Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu akizungumza na wananchi wakati wa Mkutano wa hadhara uliofanyika katika eneo la Ofisi za serikali za kijiji cha Mtavira.


Na Mathias Canal, Singida


Mwenyekiti wa Kitongoji Cha Kazizi Ndg Kurwa Maduka amevuliwa uongozini na Wananchi Wakati wa Mkutano wa hadhara kutokana na tuhuma za kuruhusu na kuingiza wavamizi katika hifadhi ya msitu zinazomkabili huku wananchi hao wakipendekeza Aliyekuwa Kaimu Mwenyekiti wa Kitongoji hicho Ndg Mussa Mkumbo kuendelea Kuhudumu katika nafasi hiyo.

Mkutano huo uliofanyika katika eneo la Ofisi ya Kijiji Cha Mtavira na kuhudhuriwa na wananchi 353 kutoka Kijiji Cha Makilawa, Mtavira na Mteva Kata ya Makilawa umepelekea pia Mwenyekiti wa Kijiji Cha Mtavira Ndg Jilala Lutelemula kujiuzulu kutokana na tuhuma mbalimbali zinazomkabili ikiwemo tuhuma za kuchukua Rushwa ili kuwaacha wafugaji waendelee kuishi na kuharibu msitu.

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu akizungumza na wananchi wakati wa Mkutano wa hadhara uliofanyika katika eneo la Ofisi za serikali za kijiji cha Mtavira.


Mara Baada ya Mwenyekiti huyo kujiuzulu katika Mkutano huo Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu Aliagiza kuitishwa Mkutano wa wananchi haraka iwezekanavyo ili kuchagua Mwenyekiti mpya ambapo pia ameagiza Mwenyekiti huyo kutiwa nguvuni ili kulisaidia Jeshi la polisi kubaini wahujumu wa msitu huo.

Mhe Mtaturu pia aliliamuru Jeshi la polisi kumtafuta popote alipo aliyekuwa Mwenyekiti wa Kitongoji Cha Kazizi Ndg Kurwa Maduka kutokana na tuhuma zinazomkabili ikiwemo kuzuia wananchi kuhama katika msitu huo Jambo ambalo Ni kosa kisheria.

Usiku wa kuamkia Octoba 17, 2017 Mhe Mtaturu aliongoza Kamati ya ulinzi na usalama Wilaya ya Ikungi kuwasaka na kuwakamata wavamizi wa msitu wa Minyughe wanaoendesha shughuli za kibinadamu ikiwemo Makazi, kilimo na Ufugaji kinyume na Tangazo la serikali (GN) ya kuanzisha hifadhi ya msitu wa Minyughe ya Mwaka 2007.
Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Mtavira, Makilawa na Mteva wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu wakati wa Mkutano wa hadhara uliofanyika katika eneo la Ofisi za serikali za kijiji cha Mtavira.


Katika Oparesheni hiyo Kamati ya ulinzi na usalama pamoja na mambo mengine pia iliyobaini ukiukwaji wa taratibu unaofanywa na baadhi ya viongozi wa Vijiji na Vitongoji ikiwemo kuwauzia mavamizi maeneo kwa kutoa Rushwa ya fedha au Mifugo.

Mhe Mtaturu ameiagiza Taasisi ya kupambana na kuzuia Rushwa (TAKUKURU) Kuwahoji wote wanaotuhumiwa katika sakata la kuruhusu wavamizi wa hifadhi ya msitu.

Alisema kuwa Ni aibu kubwa kwa viongozi kujihusisha na tuhuma mbalimbali zinazoichafua serikali, Kuvunja heshima na Uaminifu wa wananchi kwa serikali yao.

"Dhambi ya viongozi kuwaacha kwa makusudi wananchi waharibu misitu itaendelea kuwatafuna viongozi hao kwani wamewasababishia wananchi kuingia hasara ya kuchomewa nyumba zao ambazo walidhani Ni makazi ya kudumu, Ni dhahiri kuwa hatuwezi kuvumilia Nchi ikawa inaongozwa ovyo ovyo ilihali Kuna sheria, taratibu na kanuni" Alikaririwa Mhe Mtaturu

Mhe Mtaturu pia alisema kuwa ili kunusuru misitu kuharibiwa na wavamizi itaundwa Bodi ya Misitu ambayo itashirikisha Wajumbe kutoka kila Kijiji katika Vijiji 24 vlivyopo katika Kata 8 zilizopitiwa na msitu huo wa hifadhi.

Pia aliwataka viongozi wa Vijiji, Kata na Kamati zote za misitu kushirikiana kwa karibu na serikali ili kutunza misiti kwani ndio Msingi wa uimarishaji wa Mazingira na uoto wa asili.

Mhe Mtaturu alisema kuwa dhamira ya kuhifadhi misitu Ni kutunza Mazingira na uoto wa asili hivyo wananchi kufanya shughuli za kibinadamu Ni kinyume na sheria ya misitu namba 14 ya mwaka 2002.

Sambamba na hayo pia Mhe Mtaturu aliwasihi wananchi kuanza kuandaa mashamba kwani msimu wa Kilimo umekaribia huku akiwasisitiza kuendelea kumuunga Mkono Rais wa Awamu ya Tano wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli kutokana na kazi kubwa ya kusimamia Rasilimali za Nchi anayoifanya.

Mhe Mtaturu alichangia shilingi milioni mbili kwa ajili ya ukarabati wa jengo litakalotumika kwa ajili ya kituo cha polisi cha muda huku Akielekeza wananchi, serikali ya kijiji na Kata kusaidia ukarabati wa kituo hicho sambamba na ujenzi wa kituo kipya cha Polisi cha Kata ya Makilawa.

Hifadhi ya msitu wa Minyughe ilianzishwa kwa Tangazo la serikali (GN) Mwaka 2007 ina jumla ya hekta 264,600 ina manufaa makubwa katika utunzaji wa mazingira na uoto wa asili kwa urahisi wa upatikanaji wa mvua na urahisi katika uimarishaji wa sekta ya kilimo sambamba na ushoroba (Njia ya Tembo).


Mwenyekiti wa Kijiji Cha Mtavira aliyejiuzuru Ndg Jilala Lutelemula akizungumza mbele ya wananchi wakati wa Mkutano wa hadhara kabla ya kujiuzuru.
Mkazi wa Kijiji cha Mtavira Wilayani Ikungi Ndg Nchambi Kadawi akieleza changamoto inayowakabili wakati wa mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu. 
Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Mtavira, Makilawa na Mteva wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu wakati wa Mkutano wa hadhara uliofanyika katika eneo la Ofisi za serikali za kijiji cha Mtavira.
Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Mtavira, Makilawa na Mteva wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu wakati wa Mkutano wa hadhara uliofanyika katika eneo la Ofisi za serikali za kijiji cha Mtavira.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania