CURRENT NEWS

Monday, October 30, 2017

SAKALAWE AMPIGA RISASI MWANAE WAKATI AKIJARIBU KUKWEPA MAKACHERO-CHATANDA


Na Mwamvua Mwinyi,Pwani

ALLY Sakalawe (43)mkazi wa Lukenge, Magindu ,mkoani Pwani anadaiwa kupiga risasi ovyo baada ya kukaidi kujisalimisha kwa makachero waliokwenda kufanya upekuzi nyumbani kwake ,ambapo kati ya risasi hizo ilimpata mwanawe Mekwere Ally ambae alifariki dunia .

Mbali ya kusababisha kifo cha mwanawe mtuhumiwa anadaiwa kumjeruhi askari F 3438 D/CPL Leonard katika mkono wake wa kushoto .

Aidha kufuatia msako uliofanywa na makachero hao,jeshi la polisi mkoani hilo ,linawashikilia watu wawili akiwemo Ally Sakalawe kwa kosa la kumiliki silaha bila kibali .

Kaimu kamanda wa polisi mkoani humo ,Blasilus Chatanda alikiri kutokea kwa matukio hayo.

Alielezea watu hao wamekamatwa Oct 28 majira ya saa 5.30 katika kitongoji cha Kilungule kijiji cha Lukenge kata ya Magindu ,wilaya ya kipolisi Mlandizi.

Chatanda alisema ,watuhimiwa wanadaiwa pia kujihusisha na matukio ya ujambazi na uwindaji haramu .

Alifafanua,siku hiyo mkuu wa upelelezi Mkoa wa Pwani SSP Kingai akiwa na timu ya makachero walimkamata Sakalawe,akiwa na bunduki mbili aina ya gobore,risasi mark4 na kipande kimoja cha gamba la kakakuona.

Alitaja vitu vingine kuwa ni sanjali na vipande 10 vya nondo vilivyokatwa mithili ya risasi ,goroli 249 za baiskeli alizokuwa anatumia kama risasi na vifurushi saba vya nyuzi ya katani alizokuwa akitumia kwenye mtutu wa bunduki kuzuia baruti.

Chatanda alielezea ,katika upekuzi huo askari walijitambulisha kwa watu waliokuwa ndani ya nyumba hiyo kwa kuwataka wajisalimishe lakini mtuhumiwa huyo alikaidi na kuamua kufyatua risasi ovyo .

"Kati ya risasi hizo alizokuwa akifyatua alimjeruhi tumboni mtoto wake anaeitwa Mekwere Ally ambae alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu kituo cha afya Chalinze" 

"Mtuhumiwa  alimjeruhi askari F 3438 D/CPL Leonard katika mkono wake wa kushoto ambae amepatiwa matibabu katika kituo cha afya Chalinze na amesharuhusiwa " alisema Chatanda .

Katika tukio jingine, Robison Almas (37)alikamatwa akiwa na bunduki aina ya gobore ambazo alikuwa akizimiliki kinyume na utaratibu .

Kaimu kamanda huyo Mkoani Pwani ,Chatanda alisema mtuhumiwa huyo anahusishwa kutumia silaha hizo kwenye matukio ya ujambazi na uwindaji haramu .

Chatanda, alitoa rai kwa wananchi ambao wanatumia silaha kinyume na utaratibu kwenda kujisalimisha katika jeshi la polisi .
a
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania