CURRENT NEWS

Tuesday, October 24, 2017

WATAKAOTOA AMA KUPATIWA STIKA ZA MAGARI KIMAGUMASHI KUKIONA -RPC SHANNA


Na Mwamvua Mwinyi,Pwani

JESHI la polisi mkoani Pwani ,limeanza kufanya zoezi la ukaguzi wa magari aina yote ikiwa ni pamoja na utoaji wa stika za usalama barabarani kwa magari yatakayokuwa ni mazima .

Pamoja na hilo ,kamanda wa polisi mkoani Pwani (ACP) Jonathan Shanna ,amemuagiza kamanda wa usalama barabarani mkoani humo ,Edward Gontako ,kuhakikisha wale wote wanaogawiwa stika waweze kufahamika.

Aidha magari yanayobeba wanafunzi katika shule binafsi yatakaguliwa na wamiliki wa shule wameombwa kuzingatia kuwa na magari yenye mikanda kwa ajili ya wanafunzi na kuyakodi ama kumiliki magari yaliyo mazima na kuyakagua mara kwa mara .

Katika ukaguzi huo pia utahusisha kuwapima madereva ulevi na watakaobainika kujihusisha na utumiaji wa vileo wanapoendesha vyombo vya moto hatua za kisheria zitachukuliwa.

Akizungumzia kuhusiana na ukaguzi huo na mkakati waliojiwekea kupambana na madereva na wamiliki wa magari wasiofuata sheria za usalama barabarani, alisema mkoa huo umegawa stika kwa serial namba ili kuwabaini watakaopewa kimagumashi .

Kamanda Shanna ,alieleza kwamba watakaotoa stika hizo kwa magari yaliyo mabovu na pasipo kuyakagua hatua kali zitachukuliwa dhidi yao .

Alieleza katika kuhakikisha wanafanikisha kauli mbiu ya mwaka huu Zuia Ajali ,Tii Sheria Okoa Maisha,;" jeshi la polisi mkoani hapo watakahahakisha magari yote yanayopita kwenye mkoa huo yanakaguliwa.

"Tunakagua magari aina yote yakiwemo magari yanayobeba wanafunzi,tax,magari ya abiria,binafsi na yanayobeba mizigo"

Kamanda Shanna alifafanua kuwa ,kaguzi hizo ni endelevu kwani itasaidia kupunguza ajali zembe zinazosababishwa na madereva walevi ama madereva na wamiliki wanaoingiza magari yao barabarani yakiwa mabovu .

Hata hivyo kamanda huyo ,alisema watathubutu kuingilia kati mahakama iweze kutoa adhabu kali kwa madereva na wamiliki wazembe .

Nae kaimu kamanda wa kikosi cha usalama barabarani mkoani Pwani Edward Gontako ,alisema wametoa muda maalum wa kuangalia stika baada ya hapo wale ambao hawajapeleka magari yao kukaguliwa kwa hiari na kupewa stika kwa mujibu wa sheria watakamatwa na kushtakiwa .

Alisema endapo kunabainika gari ni bovu halitaruhusiwa kuingia barabarani ambapo mmiliki husika atatakiwa kulipeleka kwenye matengenezo kisha litakaguliwa upya .

Gontako alibainisha ,baada ya hapo ndipo litaruhusiwa kuingia barabarani kwa uthibitisho wa askari wa usalama barabarani.

Alisema zoezi la ukaguzi wa magari mbalimbali mkoani hapa sio la masihala na aliwataka madereva ikiwemo wa Pikipiki kuwa makini ili kuokoa maisha ya abiria wao .

 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania