CURRENT NEWS

Saturday, November 4, 2017

AWESO AWAPA KIBARUA WAKANDARASI WA MAJI NCHINI

Naibu waziri wa maji na umwagiliaji Jumaa Aweso akimsikiliza mwananchi wa wilaya ya Bahi Esther Matonya aliyesimamisha msafara wake akiwa katika ziara wilayani humo na kueleza adha ya maji wanayoipata.

 Naibu waziri wa maji na umwagiliaji Jumaa Aweso akipanda ngazi za tanki la kuhifadhia maji lililopo wilayani Bahi na ili kulikagua.
Mhandisi wa Maji wa wilaya ya Bahi Deus Mchele akitoa maelezo ya mradi wa kijiji cha Mchito mbele ya naibu waziri wa maji na umwagiliaji Jumaa Aweso.

Naibu waziri wa maji na umwagiliaji Jumaa Aweso akipanda ngazi za tanki la kuhifadhia maji lililopo wilayani Bahi na ili kulikagua. 
Naibu waziri Wa Maji na Umwagiliaji Jumaa Aweso akiwa katika picha ya pamoja na wananchi wa Kijiji cha Mchito alipokuwa katika ziara yake wilayani Bahi pamoja nae yupo makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo Sosthenes Mpandu.
.....................................................................................................
NAIBU waziri wa Maji na Umwagiliaji Jumaa Aweso amewataka wakandarasi wa maji katika halmashauri nchini kufanya kazi kwa bidii ili majisafi na salama yapatikane na kuweza kufikia azma ya serikali ya awamu ya tano ya kumtua mama ndoo ya maji kichwani kwa kuhakikisha maji mijini yanapatikana kwa asilimia 95 na vijijini asilimia 85 ifikapo 2020.

Akizungumza  na wananchi wa kijiji cha Mchito wilayani  Bahi ikiwa ni siku ya tatu toka aanze ziara yake mkoani Dodoma Aweso amesema uhandisi wa maji maana yake ni maji yapatikane na sio vinginevyo.

"Uhandisi wa maji maana yake maji yapatikane, wananchi hawataki kusikia mambo ya dizaini,upembuzi wala usanifu wanataka maji, fanyeni kazi watu wapate maji na sio vinginevyo,

"Ndugu zanguni mi unaibu waziri bado nautaka hivyo sitokubali kutumbuliwa,kabla sijatumbuliwa mimi nitakutumbua wewe timizeni majukumu yenu,"alisisitiza Naibu huyo.

Alisema serikali ina dhamira ya dhati ya kuhakikisha wilaya ya Bahi inapata maji ambapo katika mwaka wa fedha wa 2017/2018 jumla ya shilingi  bilioni moja zimetengwa.

"Katika kuhakikisha mkoa wa Dodoma unakuwa na maji ya uhakika tumeamua kutumia bwawa la Farkwa kwa ajili ya kusambaza maji katika wilaya ya Chemba,Bahi na Dodoma mjini,ndugu zangu unapobebwa kiuno kikaze,ukikilegeza utaanguka,nawaomba mtunze miradi ya maji,"alisema Aweso.

Alisisitiza suala la miradi kutopewa mtu kwa dhana ya ushemeji au undugu kwa kuwa mara nyingi wamekuwa wanakwamisha utendaji kwa kukosa uwezo.

"Kuna baadhi ya miradi mnapeana kwa ushemeji tabia hiyo inakwamisha wananchi,wapeni watu miradi wenye uwezo wa kusaidia wananchi,lakini vijana wa hapa muwape kazi wanazoweza kufanya,haipendezi mtu anatoka Arusha kwa kazi ya kuchimba mfereji,"alisisitiza Aweso.

Wakizungumza baadhi ya wanachi wamempongeza rais John Magufuli na serikali yake kwa kuonyesha dhamira ya kutatua shida ya maji iliyokuwa inawafanya waamke alfajiri na kulala usiku sana hali iliyoleta changamoto katika ndoa zao.

Kwa upande wake makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo  Sosthenes Mpandu alimshukuru naibu waziri kwa ziara yake inayolenga kutatua tatizo la maji ambapo kwa sasa wananchi wa Bahi wananunua dumu moja shilingi mia tano hadi mia sita.

"Mh Aweso ziara yako imeleta manufaa,umetuonyesha na kudhihirisha kuwa rais hakufanya makosa katika kukuteua unaendana na kauli mbiu yake ya hapa kazi tu,,tunashukuru na kukuomba tena utukumbuke wilaya ya Bahi,"alisema makamu mwenyekiti.


Katika ziara yake mkoani Dodoma Aweso ametembelea wilaya ya Dodoma mjini,Mpwapwa na Bahi ambapo wilayani Bahi ametembelea chanzo cha maji cha Mkakatika,eneo la tanki la maji,kituo cha kuchota maji cha wananchi,mradi wa maji wa kijiji cha Mchito ambapo kukamilika kwake kutafanya upatikanaji wa maji ufikie asilimia 48.73 kutoka asilimia 16 iliyopo sasa.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania