CURRENT NEWS

Saturday, November 4, 2017

JAFO AKOROMEA WAKANDARASI WA UJENZI WA BARABARA KITETO

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali(Tamisemi), Selemani Jafo akiwa na viongozi mbalimbali wa wilaya ya Kiteto wakikagua barabara ya Namelock-Sunya.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali(Tamisemi), Selemani Jafo akiwa na viongozi mbalimbali wa wilaya ya Kiteto wakikagua barabara ya Namelock-Sunya.

 Wananchi wa Engusero wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali(Tamisemi), Selemani Jafo kwenye mkutano wa hadhara.
Wananchi wa Engusero wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali(Tamisemi), Selemani Jafo kwenye mkutano wa hadhara.

 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali(Tamisemi), Selemani Jafo akiwa kwenye picha ya pamoja na wanafunzi wa shule ya sekondari Engusero.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali(Tamisemi), Selemani Jafo akiwa kwenye mkutano wa hadhara katika kijiji cha Engusero.
...................................................................
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali(Tamisemi), Selemani Jafo amefanya ziara leo wilayani Kiteto mkoani Manyara na kumuagiza Meneja wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini(Tarura) kuhakikisha ifikapo Novemba 17 mwaka huu utekelezaji wa barabara ya Namelock-Sunya yenye urefu wa kilomita 88.1 uwe wa kuridhisha.

Jafo amefikia hatua hiyo baada ya kukagua barabara hiyo na kutoridhishwa na utekelezaji wake wakati ni miongoni mwa barabara za kimkakati za wilaya hiyo.

Amesema kama utekelezaji huo utakuwa wa kusuasua hadi tarehe hiyo na Meneja huyo akashindwa kumchukulia hatua mkandarasi wa ujenzi wa barabara hiyo basi ataondolewa katika nafasi hiyo meneja huyo.

“Serikali imetoa zaidi ya Sh.Bilioni 6 kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii lakini utekelezaji wake unasuasua nikwambie tu Meneja nikija tena Novemba 17 nikakuta hali hii na wewe ukawa hujamchukulia hatua mkandarasi basi nitakunyofoa wewe,”amesema Jafo

Mbali na hilo, Jafo amekagua kituo cha Afya Engusero na kuwaahidi kuwa serikali itaendelea kuboresha huduma za afya kwenye eneo hilo ili wananchi waweze kupata huduma bora.

“Tutaleta fedha za kujenga chumba cha upasuaji, chumba cha kuhifadhia maiti, wodi ya kinamama na watoto pia, nimeshuhudia changamoto zilizopo tunawahakikishia wananchi serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuhakikisha zinatolewa huduma bora za afya,”amesema.

Kadhalika, Jafo ametembelea shule ya sekondari Engusero na kuzungumza na walimu na wanafunzi ambapo amewaahidi serikali itaboresha miundombinu ya shule hiyo ili kuhakikisha wanasoma katika mazingira mazuri.

Mara baada ya ziara hiyo, Jafo amezungumza na wananchi wa Engusero katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye eneo hilo ambapo amezungumzia dhamira ya serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk.John Magufuli katika kulinda rasilimali za Taifa hasa madini kuwa imesaidia kuongezeka kwa mgao kwenye madini ambapo awali Tanzania ilikuwa haipati.

Amesema serikali inaendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi na kuwataka kufanya kazi kwa bidii na kuanzisha kwa viwanda vya usindikaji mazao ikiwemo alizeti.

Kwa upande wake, Mbunge wa Kiteto Emmanuel Papian ameishukuru serikali kwa kuendelea kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wake huku akiomba serikali kuwapatia fedha za ujenzi wa uzio katika shule ya sekondari Engusero ili kuwalinda wanafunzi.

Aidha amesema wilaya hiyo inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa watumishi mbalimbali ikiwemo madaktari na kuiomba serikali kutupia jicho na kushughulikia changamoto hizo.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania