CURRENT NEWS

Tuesday, November 7, 2017

MAKAMU WA RAIS AFUNGUA MKUTANO WA KIMATAIFA WA WADAU WA ELIMU YA UFUNDI NA MAFUNZO JIJINI DAR ES SALAAM

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia wakati wa Ufunguzi wa mkutano wa Kimataifa wa Wadau wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ulioanza leo tarehe 6 na unatarajiwa kumalizika tarehe 8 november, katika ukumbi wa APC Bunju, Jijini Dar es Salaam. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipata maelezo ya namna ya mashine ya kuchora kadi za mifumo ya umeme inavyofanya kazi na Mhandisi Vedastus Sichilima kutoka D.I.T (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)​


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungani wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, leo amefungua Mkutano wa Kimataifa wa wadau wa elimu na mafunzo ya ufundi. Mkutano huo unaofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Hotel ya APC Bunju wilayani Kinondoni, umeandaliwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) kwa kushirikianana Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima ya nchini Finland. 

Akihutubia washiriki katika Mkutano huo wenye kaulimbiu isemayo “wekeza katika elimu ya ufundi na mafunzo kwa Tanzania kuwa ya uchumi wa viwanda” Makamu wa Rais alisema kaulimbiu hiyo inaenda sambamba na agenda ya serikali ya kutekeleza dira ya kuwa nchi ya viwanda na uchumi wa kati ifikapo 2025. “Ni dhahiri kuwa elimu ya ufundi ni nguzo muhimu ya kufikia agenda ya serikali ya kuwa Tanzania ya viwanda na kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025” alisisitiza Makamu wa Rais

Makamu wa Rais alisema amefarijika kuona kuwa Mkutano huo umepambwa na magwiji wote kutoka taasisi na vyuo vya elimu ya ufundi pamoja na wadau wote wa utoaji wa elimu ya ufundi na mafunzo. Aidha, alisisitiza kuwa anatambua kuwa kutoa elimu ya ufundi ni mkakati muhimu sana utakaosaidia kubadili fikra na mitazamo ya raia walioelimika na kuwa mahiri katika stadi na maarifa ya kutosha kusaidia kukabiliana na changamoto za maendeleo ya nchi yetu.

Sambamba na hilo, Makamu wa Rais aliwapongeza waajiri waliojitokeza katika mkutano huo na kuwaasa kwamba wao ni kiungo muhimu sana katika kuleta maana halisi ya mkutano huo. Makamu wa Rais alisema ili kuzalisha na kuendeleza rasilimali watu bora katika kada ya kati ni lazima kuwepo mahusiano mazuri baina ya taasisi zinazotoa mafunzo ya ufundi na waajiri. Mahusiano hayo ndiyo yatakayozalisha wataalam bora kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu.

Akizitaja changamoto zinazoikabili sekta ya elimu hapa nchini, Makamu wa Rais alisema ni pamoja na kutokuwepo kwa muunganiko wa kutosha kati ya taasisi zinazotoa elimu na mafunzo ya ufundi na waajiri kama vile viwanda, mabenki, taasisi za afya na vyombo vya habari. Aidha, upo uelewa mdogo miongoni mwa wadau na jamii kwamba elimu ya ufundi inahusu masuala ya useremala, uashi, ufundi makenika, kushona nguo na mambo yanayofanana na hayo. Pamoja na hayo upungufu wa miundombinu stahiki katika vyuo vya ufundi ili kutoa mafunzo yenye viwango vya ubora wa hali ya juu nayo ni changamoto.

Makamu wa Rais alisema wakati nchi inaelekea kwenye uchumi wa Viwanda, hatuna budi kujipana kuandaa wataalamu wa kutosha hivyo Serikali imeelekeza Baraza kuanda, kupitia upya na kuboresha Mitaala kwenye maeneo muhimu ili kuendana na mahitaji ya soko la ajira.

Makamu wa Rais alisisitiza kuwa utoaji wa Elimu ya Ufundi inayojibu matatizo ya jamii, inayoandaa vijana wenye umahiri wa kuweza kupambana na changamoto za maendeleo katika ulimwengu wa sasa wa Sayansi na Teknolojia.

Mwisho Makamu wa Rais alisema kuwa ni matarajio yake Mkutano huu utatoa maazimio na ufumbuzi wa namna ya kukabiliana na changamoto za utoaji wa Elimu ya ufundi na kuishauri Serikali ipasavyo juu ya hatua za kuchukua ili elimu itolewayo iendane na mahitaji ya Soko la ajira.

Makamu wa Rais aliwashukuru na kuwapongeza Taasisi ya Elimu ya watu Wazima ya Finland kwa kushirikiana na NACTE katika kuandaa mkutano huo .

Aidha aliwapongeza Jamhuri ya Watu wa Finland kwa kuadhimisha miaka 100 ya uhuru.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania