CURRENT NEWS

Thursday, November 9, 2017

RC MAHENGE AMEKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA VIONGOZI NA WAJUMBE WA CHAMA CHA WAFANYABIASHARA, WAKULIMA NA WENYE VIWANDA - TCCIA

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mheshimiwa Dkt. Binilith Mahenge akisisitiza jambo wakati wa mkutano kati yake na Viongozi wa Wafanyabiashara wa Mkoa wa Dodoma. 


Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mheshimiwa Dkt. Binilith Mahenge akisisitiza jambo wakati wa mkutano kati yake na Viongozi wa Wafanyabiashara wa Mkoa wa Dodoma.Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mheshimiwa Dkt. Binilith Mahenge akisisitiza jambo wakati wa mkutano kati yake na Viongozi wa Wafanyabiashara wa Mkoa wa Dodoma.Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Mkoa wa Dodoma Bwana Deusi Nyabiri (kushoto) akiwasilisha salamu za wafanyabiashara wakati wa mkutano baina yao na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge (kulia).

    .........................................................................................................................
Na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dodoma
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mheshimiwa Dkt. Binilith Mahenge ameendelea na ratiba ya kukutana na Kuzungumza na Viongozi wa makundi mbalimbali muhimu kwenye Mkoa wa Dodoma na awamu hii amekutana na Viongozi na Wajumbe wa Chama cha Wafanyabiashara, Wakulima na Wenyeviwanda - TCCIA Mkoa wa Dodoma kwa lengo la kuendelea kujitambulisha na kushauriana masuala ya maendeleo kwenye Mkoa wa Dodoma.

Katika Mazungumzo yao Dkt. Mahenge amewataka wafanyabiashara na wadau wa sekta binafsi kuchukua nafasi yao ipasavyo kwenye maeneo makuu mawili akiyataja kuwa ni eneo la Ujio wa Serikali Mkoani Dodoma Makao Makuu ya Nchi na Utekelezaji wa azma ya kuelekea Tanzania ya Viwanda.
Amesema Ujio wa Serikali Mkoani Dodoma unakuja na fursa nyingi na mahitaji mengi ambayo kimsingi Serikali pekee haiwezi kuyatekeleza yote na hivyo inahitaji Sekta binafsi kuchukua nafasi yake kwenye maeneo yanayoruhusu sekta binafsi, amesema kuwa uwepo wa serikali hapa Mkoani Dodoma na Jiografia ya Dodoma kuwa katikati ya nchi ni fursa ya kuhudumia mikoa ya kanda nyingine zote za nchi na hata baadhi ya nchi jirani.
Katika suala la Kuelekea Tanzania ya Viwanda Dkt. Mahenge amewataka Wafanyabiashara hao kutoogopa kutafuta mitaji kwenye Taasisi za Fedha kwa ajili ya kuwekeza kwenye sekta ya Viwanda kwa kuwa ujio wa serikali utaambatana na mahitaji ya huduma na bidhaa za aina nyingi hivyo soko la bidhaa za viwandani litakuwa la kutosha kikubwa ni kutatua changamoto zinazokabili masuala ya uwekezaji wa viwanda.
Dkt. Mahenge amewataka wafanyabiashara wa Mkoa wa Dodoma kuhakikisha wanaboresha huduma zao na kuwa za kiwango cha hali ya juu wakitambua kuwa Dodoma ni Makao Makuu ya Nchi hivyo inatakiwa kuwa na huduma zenye kiwango cha ubora ambacho kinafikia hadhi ya kimataifa. Amewataka wasiogope kuchukua mikopo na kuboresha biashara zao.

Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Bwana Deusi Nyabiri, amesema kuwa tatizo linalokabili sekta ya biashara ni sheria zinazosimamia sekta hiyo, lakini pia akamuomba Mkuu wa Mkoa kama kiongozi Mkuu wa Serikali kwenye Mkoa ahakikishe anaweka mfumo mzuri zaidi wa mawasiliano na Mahusiano kati ya Taasisi za Serikali zinazosimamia masuala ya biashara na uwekezaji na Wafanyabiashara na Sekta binafsi na kubadili mfumo wa sasa ambao umejikita katika kuwatoza adhabu wafanyabiashara badala ya kuwaelimisha.
Amezitaja taasisi hizo za serikali kama Baraza la Taifa la Usimamizi Mazingira - NEMC, Mamlaka ya Mapato - TRA, Mamlaka ya Chakula na Dawa - TFDA, Wakala wa Usalama Mahala pa Kazi - OSHA na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Amesema pia ili kuiunga zaidi mkono Serikali katika utekelezaji wa Ujio wa Serikali Mkoani Dodoma na uwekezaji muhimu unaohitajika kufanyika, ipo haja kwa Mamlaka za Serikali zinazosimamia jambo hili la ujio kuweka wazi zaidi mipango ya mahitaji ya uwekezaji na huduma mbalimbali ili Wafanyabiashara waone ni eneo lipi ambalo wao wanaweza kushiriki na kuisaidia Serikali.
Pia amemtaka Dkt. Mahenge akiwa kama Mwenyekiti wa Baraza la Biashara la Mkoa wa Dodoma kuhakikisha Mabaraza ya biashara ya Wilaya zote Mkoani Dodoma na balaza la Mkoa kuimarishwa na kuboreshwa zaidi ili yaweze kutekeleza majukumu yake ya kuwa jukwaa la majadiliano kati ya Serikali na Sekta binafsi ili kubaini na kuzitafutia majibu changamoto zinazokabili sekta ya biashara na uwekezaji kwenye Mkoa wa Dodoma.
Kikao hiko kimetumika pia kuainisha changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyabiashara na wawekezaji wa sekta binafsi ndani ya Manispaa ya Dodoma na Wilaya za Mkoa wa Dodoma na tayari Uongozi wa Mkoa umekubaliana na Wafanyabiashara hao kupitia vyama vyao kuweka mkakati wa pamoja wa kuzimaliza kero  na changamoto zote ili kukuza kasi ya biashara na uwekezaji Mkoani Dodoma.

 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania