CURRENT NEWS

Sunday, November 19, 2017

NDIKILO-MAKAMPUNI 30 KUTOKA CHINA YATARAJIA KUJA KUWEKEZA MKOANI PWANI

Mkuu Wa Mkoa Wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo,akipokea taarifa kutoka Kwa timu ya Mkoa huo ilitoka safari nchini China , kujifunza masuala mbalimbali ya uwekezaji na kuhamasisha wawekezaji.(picha na Mwamvua Mwinyi)
  Katibu tawala Mkoani Pwani (RAS)Zuberi Samataba akitoa taarifa kwa mkuu wa mkoa huo,kuhusiana na mafanikio waliyoyapata katika safari yao ,ambapo waliambatana baadhi ya wataalamu na viongozi Mkoani hapo kwenda nchini China kwa ajili ya kujifunza masuala mbalimbali ya uwekezaji na kuhamasisha wawekezaji.(picha na Mwamvua Mwinyi)

Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
MAKAMPUNI 30 kutoka nchini China yanatarajia kuja Mkoa wa Pwani -Tanzania ,kwa ajili ya kuangalia namna ya kuwekeza kwenye sekta ya mbalimbali za kiuchumi.
Ujio wa makampuni hayo ,ni matunda ya safari  ya timu ya baadhi ya viongozi na wataalamu wa mkoa huo waliokwenda nchini China hivi karibuni kujifunza masuala mbalimbali ya uwekezaji.
Aidha halmashauri zilizopo mkoani humo,zinapaswa kutenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji ikishirikiana na taasisi wezeshi ikiwemo TANESCO, DAWASCO, CHALIWASA, TARURA, TRA, Jeshi la Polisi na Jeshi la Zimamoto kwa ajili ya utoaji huduma.
Mkuu wa mkoa wa Pwani,Mhandisi Evarist Ndikilo aliyasema hayo wakati akipokea taarifa kutoka kwa maofisa hao.
Alisema safari hiyo imewafunza namna ya kuvutia na kuhamasisha wawekezaji na uzalishaji pamoja na uendelezaji wa viwanda.

Mhandisi Ndikilo alieleza, kupatikana kwa wawekezaji hao kuja mkoani Pwani ni mwendelezo wa uwekezaji mkubwa uliowekwa na makampuni mengi kutoka nchi ya China.
Alisema mkoa huo ni moja ya mikoa ambayo ina wawekezaji kwenye sekta ya viwanda ikiwemo cha kuchakata betri kilichopo Kibaha kinachoitwa Anhui Boda Power Co Ltd.
Kingine ni kiwanda cha vigae kilichojengwa Pingo Chalinze cha Twyford Ceramic T Ltd na kiwanda cha Chuma kilichopo Mlandizi Kibaha cha Kiluwa Steel Group Co Ltd.

"Ziara hiyo imepata mafanikio makubwa ambapo makampuni hayo yatakuja kuwekeza kwenye sekta za Kilimo, Madini, Madawa ya viwandani, utalii, ujenzi viwanda vya juisi, bia, ujenzi wa majengo ya ofisi, chuma na mabomba ya chuma" alifafanua.
Mhandisi Ndikilo alibainisha, viongozi na wataalamu hao wa ngazi ya mkoa na Halmashauri ya Kibaha wakiongozwa na katibu tawala wa mkoa(RAS) Zuberi Samataba walitembelea China kuona shughuli zinazofanywa na makampuni mbalimbali.

“Timu hiyo ikiwa nchini China ilitembelea majimbo ya Jiangsu, Anhui, Guangdong na Majiji ya Shanghai na Beijing waliweza kuona shughuli zinazofanywa na wawekezaji na kushiriki kongamano la wawekezaji na wafanyabiashara lillofanyika Beijing,” alisema Ndikilo.

Hata hivyo alisema kutokana na wimbi kubwa la wawekezaji kwenye mkoa, Halmashauri zinapaswa kutenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji ikishirikiana na taasisi wezeshi kama vile TANESCO, DAWASCO, CHALIWASA, TARURA, TRA, Jeshi la Polisi na Jeshi la Zimamoto kwa ajili ya utoaji huduma.

Aliwataka viongozi mbalimbali katika kutekeleza agizo la kujenga viwanda 100 vidogo na vya kati kila mkoa chini ya kampeni ya Mkoa , suala la ujezni wa viwanda  linafanikiwa kwa kila wilaya kuwa na mikakati ambayo inatekelezeka.
Katibu Tawala wa mkoa Zuber Samataba ambaye aliongoza timu hiyo alisema waliweza kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo nchini hususani mkoa wa Pwani na kushawishi wawekezaji kuja mkoani hapo kwa ajili ya kuwekeza.

Samataba alifafanua wakiwa kule walikutana na balozi wa Tanzania nchini China Mbelwa Kairuki ambaye alitoa ushauri wa kukabiliana na changamoto zinazowakabili wawekezaji hao wa China wanapokuja nchini ili kuongeza kasi ya uwekezaji.

“Baadhi ya mambo wanayoyaona kuwa ni changamoto kwao ni pamoja na miundombinu ya barabara, umeme, maji, vibali vya kazi, vibali vya ukazi, ucheleweshaji wa vibali ya ardhi na kupewa maeneo ambayo bado ni pori,” alisema Samataba.

Timu hiyo kutoka Mkoani Pwani ilitembelea nchi ya China na kufanya ziara ya wiki mbili ,kuanzia Oktoba 13 hadi oktoba 27 mwaka huu.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania