CURRENT NEWS

Wednesday, November 8, 2017

RC MAHENGE AKUTANA NA WAKUU WA VYUO VIKUU NA ELIMU YA JUU MKOANI DODOMA KUJADILI MASUALA YA MAENDELEO

        
Mkuu wa Mkoa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge (wa kwanza kushoto) akizungumza na Wakuu wa Vyuo Vikuu na Elimu ya Juu Mkoani Dodoma  kuhusu masuala ya Maendeleo ya Mkoa wa Dodoma.

Mkuu wa Mkoa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge (wa kwanza kushoto) akizungumza na Wakuu wa Vyuo Vikuu na Elimu ya Juu Mkoani Dodoma  kuhusu masuala ya Maendeleo ya Mkoa wa Dodoma.

Picha ya pamoja kati ya Mkuu wa Mkoa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge (wa tano kutoka kushoto) na Wakuu wa Vyuo Vikuu na Elimu ya Juu Mkoani Dodoma mara baada ya kumalizika kwa kikao baina ya viongozi hao kuhusu masuala ya Maendeleo ya Mkoa wa Dodoma.

.........................................................................................................................
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge katikati ya wiki  amekutana na kufanya mazungumzo na Viongozi wa Vyuo Vikuu, Elimu ya Juu na Ufundi Stadi Mkoani Dodoma na kwa pamoja wamejadili masuala mbalimbali ya Maendeleo ya Mkoa wa Dodoma Makao Makuu ya Nchi.
Katika Mkutano huo, Dkt. Mahenge amepongeza mchango wa Vyuo Vikuu, Elimu ya Juu na Ufundi Stadi Mkoani Dodoma na kubainisha kuwa ipo haja ya kukuza zaidi ushirikiano kati ya Serikali ya Mkoa na Taasisi hizo za Elimu ambapo amezitaka zijikite katika kufanya tafiti za kitalaamu juu  ya namna ya kutatua changamoto za wananchi na kuboresha zaidi shughuli mbalimbali za uchumi, uzalishaji na uwekezaji kwa lengo la kuufanya Mkoa wa Dodoma uwe na kasi kubwa ya maendeleo zaidi ya ilivyo sasa.
Ametaja maeneo makuu ya ushirikiano ni pamoja na eneo zima la ujio wa Serikali Mkoani Dodoma Makao Makuu ya nchi na kuzitaka Taasisi hizo za Elimu kusaidia kuwaandaa wananchi wa Dodoma juu ya namna bora za kuchangamkia fursa hiyo ya ujio na kuainisha bayana maeneo ya fursa zinazoambatana na ujio wa Serikali.
Aidha, ametaja eneo jingine muhimu linalohitaji mchango mkubwa wa Taasisi hizo za Elimu ni Eneo la kuelekea Tanzania ya Viwanda ambapo Mkoa unahitaji kuandaa nguvu kazi ya kutosha na yenye ujuzi kwenye fani mbalimbali zinazohitajika kwenye viwanda vilivyopo na vinavyoendelea kujengwa na kutaja Taasisi kama ya VETA inaweza kutoa mchango mkubwa kuwaandaa vijana ili watafutiwe mitaji waweze kujiajiri kwa kuanzisha viwanda vidogo, vya kati na hatimaye vikubwa.
Amebainisha kuwa Mkoa pia unahitaji ushirikiano  na Taasisi hizo kwenye eneo la Elimu hususani suala la kuinua kiwango cha ufaulu kwa kusaidia ufundishaji kwenye shule za Dodoma na mafunzo kwa walimu wa Mkoa wa Dodoma. Amesema kwa hali ya sasa bado kiwango cha Ufaulu cha Mkoa wa Dodoma hakiridhishi akitolea mfano kuwa wastani wa kiwango cha ufaulu cha Mkoa wa Dodoma kwenye mtihani wa kumaliza Elimu ya msingi kwa mwaka huu 2017 ni asilimia 63.68% hivyo kuufanya Mkoa kushika nafasi ya 24 kati ya mikoa 26.
Dkt. Mahenge pia ameziomba Taasisi hizo za Elimu kuona namna ya kubuni programu mbalimbali za utunzanji Mazingira ya Mkoa wa Dodoma kwa kuwashirikisha wanafunzi wake katika utekelezaji kama moja ya njia ya kufanyia kazi kwa vitendo elimu wanayopewa darasani na kubainisha kuwa utunzaji wa mazingira utapunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kuboresha hali ya hewa.
Akipongeza jitihada za Serikali ya awamu ya Tano, Kaimu Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo vijijini (IRDP) Profesa Hozen Mayaya  amemweleza Mkuu wa Mkoa kuwa, Chuo chake kitajikita zaidi katika suala zima la Tafiti na kuziwezesha Halmashauri za Wilaya za Mkoa wa Dodoma  katika uandaaji wa mipango ya Maendeleo ambayo itagusa hadi wananchi kwenye ngazi za msingi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Mafunzo na Ufundi Stadi (VETA) Dodoma Ndugu Ramadhani Mataka amesema tayari chuo chake kilishaanza programu za kuwaandaa vijana kwa kuwapa ujuzi kwenye fani mbalimbali ambapo tayari Vijana zaidi ya 800 waliokuwa kwenye soko la uzalishaji mtaani kwenye fani mbalimbali walipatiwa mafunzo rasmi na kusajiliwa, Amesema kuwa programu hiyo itaendelea ili kuwafikia vijana wengi zaidi hapa Mkoani Dodoma.
Aidha, Mkurugenzi wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Kampasi ya Dodoma Ndugu Omary Ally amesema kuwa tayari chuo chake kilishaanza utaratibu wa kuandaa makongamano ya Biashara, Uchumi na Uwekezaji yakiangazia fursa mbalimbali zinazokuja na ujio wa Serikali Mkoani Dodoma na kubainisha kuwa mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka huu kongamano lingine litafanyika lenye lengo la kuangazia Dhana ya Tanzania ya Viwanda kwa maendeleo endelevu ya kiuchumi ambapo wataalamu wa chuo chake watawasilisha matokeo ya tafiti mbalimbali walizozifanya.
Pia amesema ili kusaidia eneo la elimu na kiwango cha ufaulu Mkoani Dodoma chuo chake kitaandaa programu za kutoa wataalamu wake na wanafunzi wake wakati wa mazoezi ya vitendo kwenda kufundisha kwenye shule za Dodoma, lakini pia wataandaa programu maalumu za kuwajengea uwezo walimu wa Dodoma na kuwa kwa sasa tayari chuo hicho kimeanzisha kozi ya shahada ya kwanza ya ualimu wa masomo ya biashara. 
             Imeandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania