CURRENT NEWS

Thursday, November 16, 2017

RC WA TANGA MARTINE SHIGELLA AZINDUA RASMI TAWI LA BENKI YA NMB MKATA WILAYANI HANDENI


Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mh.Martine Shigella leo amezindua rasmi tawi la NMB benki lililopo Kata ya Mkata Wilayani Handeni na kuwataka wakazi wa maeneo ya jirani kuacha kuhifadhi fedha nyumbani. 

Mkuu wa Mkoa amesema kuwa ufunguzi wa tawi hilo la kibenki ni fursa kubwa kwa wakazi wa Mkata na maeneo ya jirani kwani huduma za kifedha zimesogezwa karibu na ni chachu ya ukuaji wa maendeleo na uchumi wa Mkata.

Aliongeza kuwa Mkata ni eneo lenye mzunguko mkubwa wa kifedha kutokana na kuwa na wafanyabiashara mbalimbali, wakulima, wafugaji,wafanyabiashara wa matunda na biashara nyingine hivyo wanategemea kwa kiasi kikubwa huduma ya benki katika utunzaji wa fedha na usalama wao.

Mh. Shigella alisema kuwa NMB Benki imesaidia sana wananchi kwa kutoa mikopo na misaaada mingine ya kijamii hivyo ni vyema kuitumia benki hiyo kwani kwa kufanya biashara na NMB ni kufanya biashara na serikali kwa sababu kwa upande mwingine NMB ni Serikali ambapo fedha zinazowekwa ndizo zinazorudi kwenye jamii kwa mtindo wa mishahara, ujenzi wa miundo mbinu na huduma nyingine za kijamii.

”wananchi muweke utaratibu wa kuhifadhi fedha zenu kwenye benki badala ya kuzikumbatia ndani hali inayopelekea kuhatarisha usalma wa maisha yenu, NMB imefungua tawi kuwapunguzia kufuata huduma za benki mbali, tumieni fursa hii kupata mikopo ili kukuza uchumi wenu na Taifa kwa ujumla” Alisema Mkuu wa Mkoa.

Aidha amewataka NMB Benki kujiandaa na fursa za miradi mikubwa ya Bomba la mafuta,Viwanda,Madini, Kilimo na Ufugaji iliyopo Wilayani Handeni na Mkoa wa Tanga ili kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi wote kwa kuongeza matawi mengi ili kuepusha wananachi kuzunguka na fedha mifukoni.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh. Godwin Gondwe ameshukuru uongozi wa NMB kwa kuona umuhimu wa kufungua tawi eneo la Mkata ambalo litawasaidia wakazi wa eneo hilo na jirani kutotembea urefu wa KM54 kufuata huduma za benki kwa kuzingatia kwamba eneo la Mkata linawafanayabiashara wengi na mzunguko wa fedha ni mkubwa.

Wakati huohuo Meneja wa NMB kanda ya Kaskazini Bw.Salie Mlai ameahidi kuwa Benki yao itatoa msaada wa vifaa vya afya kwenye kituo cha afya cha Mkata vyenye thamani ya Milioni 10 ikiwa ni sehemu ya kurudisha faida waliyoipata kwa jamii wanayoihudumia.

Benki ya NMB yenye kauli mbiu ya “Karibu Yako” yenye maana ya kuweka ukaribu wa huduma za fedha kwa wananchi na kutoa bidhaa inayoendana na mahitaji ya maeneo husika ili iweze kuwa karibu,rahisi na yenye mafanikio katika mambo ya ujenzi wa Taifa.

NMB Benki imesambaa nchi nzima kwa asilimia 97 ambapo ina ATM zaidi ya 800, Matawi 213 na mawakala 4500 ambao wanarahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha.Mikopo ya wafanyabiashara wadogo, wa kati na wakubwa inatolewa ikiwa ni pamoja na kutoa mikopo kuendana na aina ya mradi mfano Mikopo ya pembejeo za kilimo kwa wakulima.

Imetolewa na:
Kitengo cha Teknolojia, Habari na Mawasiliano
Halmashauri ya Wilaya ya Handeni. 
 Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh Godwin Gondwe akishukuru uongozi wa NMB kwa kuona umuhimu na kufungua Tawi eneo la Mkata.


Mkuu wa Mkoa Tanga,Mh. Martin Shigela akizungumza na wananchi wa Mkata wakati wa ufunguzi wa Tawi la NMB
​Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mh. Martine Shigella kushoto na Mkurugenzi wa NMB Benki Bi. Ineke Bismeka wakifungua kibaon cha ufunguzi wa Tawi hilo​
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania