CURRENT NEWS

Tuesday, November 21, 2017

SERIKALI YAWATAKA WANAZUONI KUSAIDIA KUFANIKISHA DIRA YA UCHUMI WA VIWANDA

  
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo akiteta jambo na Waziri Mkuu mstaafu Jaji Joseph Warioba kwenye ufunguzi wa Kongamano la Mwaka la Kitaifa Kuhusu “Uchumi wa Viwanda: Kufikiria Upya Sera ya Elimu ya Ujamaa na Kujitegemea”.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo akifungua Kongamano la Mwaka la Kitaifa Kuhusu “Uchumi wa Viwanda: Kufikiria Upya Sera ya Elimu ya Ujamaa na Kujitegemea”.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo akitembelea mabanda ya maonesho katika Kongamano la Mwaka la Kitaifa Kuhusu “Uchumi wa Viwanda: Kufikiria Upya Sera ya Elimu ya Ujamaa na Kujitegemea”.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo akitembelea mabanda ya maonesho katika Kongamano la Mwaka la Kitaifa Kuhusu “Uchumi wa Viwanda: Kufikiria Upya Sera ya Elimu ya Ujamaa na Kujitegemea”.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo akitembelea mabanda ya maonesho katika Kongamano la Mwaka la Kitaifa Kuhusu “Uchumi wa Viwanda: Kufikiria Upya Sera ya Elimu ya Ujamaa na Kujitegemea”.

    ...............................................................................................................................................................

Rafael Kilapilp,Tamisemi –Dar es Salaam

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa Majaliwa  amewataka wanazuoni kujadili, kutafakari na kutathmini upya ubora wa elimu itolewayo mashuleni na vyuoni na kutoa mapendekezo yatakoyoisaidia Serikali kuboresha Sera hiyo ili iendane na  Dira ya Taifa ya Uchumi wa Viwanda ifikapo 2025.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo alipomuwakilisha Waziri Mkuu kwenye ufunguzi wa Kongamano la Mwaka la Kitaifa Kuhusu “Uchumi wa Viwanda: Kufikiria Upya Sera ya Elimu ya Ujamaa na Kujitegemea”.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri Mkuu Mhe. Jafo alisema makusudio na msingi wa Sera ya Msingi ya Elimu ya Ujamaa na Kujitegemea bado yapo vilevile lakini inapaswa kuangalia katika zama za sasa ni kwa namna gani sera hiyo iboreshwe ili iweze kuakisi uhalisia wa kipindi cha sasa.

“Tujitathimini kwa ufupi, tuangalie wahitimu wanaotoka katika vyuo vyetu hasa vijana wanaomaliza katika hatua ya shahada, stashahada na astashahada; kwa elimu waliyoipata tukiuliza maswali kuhusu uchumi wa viwanda, je maswali yanajibika? Je ni wangapi wanategemea kuajiriwa balada ya kujiajiri wenyewe?” Alisema Mhe. Jafo

Mhe. Jafo aliongeza kuwa ni lazima vijana wanaohitimu wapate elimu bora itakayowawezeshe kushindana katika soka la ajira na kujiajiri katika Jumuia ya Africa Mashariki na hata duniani kote.

“Tusipojenga misingi bora ya elimu tutapata vijana wasindikizaji siyo washiriki katika ajenda pana ya maendeleo na hasa katika ajenda hii ya uchumi wa viwanda”.

Aliendelea kueleza Sera ya elimu tuliyonayo yawezekana kuna jambo linapaswa kufanyika katika kuboresha Sera hiyo, hivyo  wanazuoni inabidi kujadili kwa kina na kwa uwazi ili kuja na maazimio yenye mashiko yatakayoisaidia Nchi katika kuelekea kwenye uchumi wa viwanda.

“Nimatumaini yangu na matumaini ya Serikali kuwa katika kazi hii tutakayoifanya kwa siku hizi mbili tutapata mawazo ya ubunifu kutoka kwa wataalamu wote mliopo hapa ambapo itasaidia kuweka maazimio mahususi, ambayo sisi kama Serikali tutayachukua kwa ujumla wake na kuangalia ni kwa jinsi gani tutayafanyia kazi kuboresha elimu yetu ili kusaidia vijana wahitimu kupambana na maeendeleo katika kujenga uchumi wa viwanda”.

Aidha Mhe. Jafo alieleza kuwa ajenda ya Taifa ya elimu imezungumzia kwa uwazi namna itakavyotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano kuboresha ajenda ya elimu na hasa namna ambavyo ajenda ya elimu itakuwa shindani zaidi kwa kuwekeza kiasi kikubwa cha fedha katika bajeti ya elimu.

“Niwaambie tu ndugu zangu, Serikali imeamua kuwekeza shilingi bilioni 600 na zaidi kwa mwaka kwenye elimu peke yake ukiachilia mbali miundombinu. Hii ni kwa ajili ya kuwapatia vijana mikopo lakini pia kugharamia elimu kwa kutoa takribani shilingi bilioni 20.7 kila mwezi ambapo kwa tathmini ya haraka zingeweza kujenga barabara yenye urefu wa km 600 ambayo ingeweza kuanzia Dar es Salaam hadi Singida”. 
Alisema Mhe. Jafo.

Waziri Jafo alisema kuwa makusudio ya Serikali ni kuifanya elimu iwe rafiki zaidi kwa kujenga mazingira bora ya kujifunza na ndiyo makusudio ya mdahalo huo utakaofanyika kwa siku mbili. 

Aliwasihi wanazoni wote kujadili kwa uwazi na kutumia elimu yao vizuri ili ikajibu matatizo ya wananchi na hasa katika swala zima la uchumi wa viwanda ili kwa pamoja kusaidia katika kujenga nchi yetu.

“Mheshimiwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli amefarijika sana kusikia kuwa wasomi mmekutanika hapa kujadili ajenda hii muhimu aliyoianzisha ya uchumi wa viwanda lakini hasa kuangalia ni jinsi gani tutaboresha elimu yetu. Naomba niwahakikishie kuwa kwa dhamira ya dhati aliyonayo Mheshimiwa Rais, haya maoni mazuri yatakayotoka hapa atayachukua kwa utetekelezaji ili kulisaidia Taifa letu”.


Kongamano hilo la “Uchumi wa Viwanda: Kufikiria Upya Sera ya Elimu ya Ujamaa na Kujitegemea,” limeandaliwa na Wanazuoni Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaamu kwa kushirikiana na Shirika la Haki Elimu, ambapo linalofanyika kwa siku mbili katika Ukumbi wa Nkuruma, Chuo Kikuu cha Dar es Salaamu kuanzia tarehe 20 -21 Novemba, 2017.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania