CURRENT NEWS

Monday, November 27, 2017

UJIO WA BAADHI YA WAWEKEZAJI KUTOKA CHINA WAVUTIWA NA FURSA ZA UWEKEZAJI PWANI

MKUU wa mkoa wa Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo,akizungumza jambo kuhusu masuala ya uwekezaji baada ya kutembelewa na baadhi ya wawakilishi Wa makampuni ya uwekezaji kutoka nchini China.
Picha ya pamoja baina ya wawakilishi wa makampuni ya uwekezaji kutoka nchini China na viongozi wa mkoa wa Pwani akiwemo mkuu Wa Mkoa huo mhandisi Evarist Ndikilo wa katikatika kati ya walioketi, Na wa kwanza kulia aliekalia kiti ni katibu tawala mkoani hapo Zuberi Samataba na wa kwanza kulia ni mmoja wa wawekezaji hao aitwae Liv Ming .(picha na Mwamvua Mwinyi)

Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha

Wawakilishi wa makampuni ya uwekezaji toka nchini China ,waliofika mkoani Pwani kuangalia fursa za uwekezaji ,wamefurahishwa na kuvutiwa na fursa nyingi walizoziona na kuonyesha nia ya kuwekeza.

Aidha wameeleza watatuma wataalamu wao watakaojua wawekeze kwenye sekta gani kati ya maeneo na sekta waliyoonyeshwa ili kujiletea manufaa.

Wakizungumza baada ya kumtembelea mkuu wa mkoa wa Pwani ,Mhandisi Evarist Ndikilo walieleza, baada ya kuonyeshwa maeneo hayo ya uwekezaji kwa njia ya video ,wameguswa na kufurahishwa kuwekeza mkoani hapo.

Mmoja wa wawakilishi wa wawekezaji hao, Liv Ming aliipongeza nchi ya Tanzania kwa ushirikiano na mahusiano yake na nchi yao ,tangu enzi za marais Julius Nyerere na Mao Tse Sung.

“Tumejionea fursa nyingi za kiuwekezaji na tutatuma wataalamu wetu kuja kuangalia na kutupa ushauri tuwekeze kwenye eneo gani kwani tumeona uwekezaji kwenye sekta ya umeme, vipuri vya magari na uhifadhi wa mazao-kilimo,” alisema Ming.

Ming alieleza kuwa,wameona maeneo mbalimbali kwa njia ya video ambayo wanaweza kuwekeza na wataendelea kufanya mawasiliano na mkoa kwa ajili ya masuala ya uwekezaji wa viwanda kwenye sekta mbalimbali.

“Tumevutiwa na mambo mengi pia kuna baadhi ya makampuni ya wenzetu kutoka China wamewekeza viwanda zaidi ya miaka 20 hivyo tutaendelea kuhamasisha wenzetu nao waje kuwekeza,” alisema Ming.

Nae mkuu wa mkoa wa Pwani ,Mhandisi Evarist Ndikilo alisema ,ujio wa wageni hao ni faraja kwa mkoa huo na Taifa kijumla kwani itasaidia azma ya serikali ya kuwa nchi ya viwanda.
Alielezea ,mkoa utaendelea kuhamasisha wawekezaji wa nje na ndani ya nchi ili wawekeze kwenye sekta mbalimbali zilizopo.

Mhandisi Ndikilo,alisema wamejipanga kuwa ukanda wa viwanda kufikia malengo ya serikali ya awamu ya tano ya nchi ya viwanda na uchumi wa kati.

Ujio wa wawekezaji hao ni kufuatia ziara ya wiki mbili iliyofanywa na timu ya baadhi ya viongozi mkoa wa Pwani wakiwemo viongozi na wataalamu waliokwenda kujifunza uhamasishaji na masuala ya uwekezaji nchini China mwezi Oktoba mwaka huu .

Katika safari hiyo ilikuwa na mafanikio makubwa ambapo waliweza kuzungumza na makampuni 106 huku 30 kukubali kuja mkoani Pwani kwa ajili ya kuangalia maeneo ya uwekezaji na hatimae kuwekeza.

 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania