CURRENT NEWS

Wednesday, November 15, 2017

VIJANA WATAKIWA KUJIKUBALI KUPAMBANA NA UMASIKINI-MWANGANDA

Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Bagamoyo, Fatuma Latu .(picha na Mwamvua Mwinyi)

AFISA maendeleo ya jamii wa halmashauri ya wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani Julius Mwanganda ,alipokuwa akizungumzia utekelezaji wa mfuko wa vijana na wanawake kipindi cha miaka miwili .(picha na Mwamvua Mwinyi)

Na Mwamvua Mwinyi,Bagamoyo

AFISA maendeleo ya jamii katika halmashauri ya wilaya ya Bagamoyo,Julius Mwanganda amesema kundi la wanawake limekuwa na mwamko mkubwa wa kimaendeleo kuliko vijana kutokana na kujikubali na kuunda vikundi vinavyowasaidia kuwezeshwa kirahisi.

Aidha katika kipindi cha mwaka 2017/2018 ,halmashauri hiyo imetenga kiasi cha sh.milioni 369.6 kwa ajili ya kuendesha mfuko wa vijana na wanawake ambapo kati ya kiasi hicho sh.milioni 237.223.516 zimetokana na mapato ya ndani.

Akizungumzia utekelezaji wa mfuko wa kuwezesha vijana na wanawake ndani ya kipindi cha miaka miwili,Mwanganda alieleza kuwa watekeleza kwa asilimia 100 .

Alisema ,kati ya fedha hiyo sh.milioni 131.839.792 ni fedha za marejesho ya kipindi kilichopita 2016/2017.

Mwanganda alielezea ,kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2017/2018 kuanzia July -Septemba ,halmashauri imeweza kuchangia sh.milioni 47.205.795.


Alibainisha katika utoaji wa mikopo awamu ya kwanza tayari imetolewa milioni 162.258.540 huku jumla ya vikundi 18 vya wanawake vikiwa vimepatiwa sh.mil.89.810.381 na vikundi vya vijana 11 milioni 72.448.173.

"Hii ni robo ya kwanza bado robo tatu ,na kikubwa ni kwamba ,makundi haya yananufaika kwani wanaongezea mitaji yao kuinua miradi na biashara ndogondogo wanazozifanya" alifafanua.

Hata hivyo katika mwaka wa fedha 2016/2017 ,halmashauri hiyo ilikopesha zaidi ya sh.milioni 257.5 kati ya hiyo milioni 175.350.7 ni asilimia tano ya fedha kutoka mapato ya ndani na milioni 82.237.140 ni fedha za marejesho .

Alisema kwamba vikundi 32 vya wanawake  na vikundi 26 vya vijana vilinufaika kwa kuwezeshwa mikopo hiyo.

Pamoja na hayo,Mwanganda aliongezea kusema,maendeleo yanaenda vizuri kwani wanapata taarifa za kimaendeleo ya vikundi hivyo kila mwezi.

"Zipo hatua tunazozichukua kama wanakikundi hawarejeshi ipasavyo ,":. Huwa tunafikisha taarifa kwa kata husika,na katika kipindi chote hicho ni vikundi vitatu pekee vilivyowahi kukiuka lakini walifikisha taarifa eneo husika" alisema.

Mwanganda alisema vijana bado hawajajikubali,hawapendi kuunda makundi ,wengi wao wanapenda kufanya shughuli zao kibinafsi/ mmoja mmoja.

Aliwasihi vijana wilayani hapo kujenga tabia ya kuwa makundi ya ujasiriamali ili kuwezeshwa kirahisi tofauti na kuwa peke inakuwa vigumu kukopesheka.

Nae mkurugenzi wa halmashauri ya Bagamoyo Fatuma Latu ,alieleza kuwa wanafanya vizuri kwa kuhakikisha wanatenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya vijana na wanawake  .

Alisema awali urejeshaji ulikuwa mgumu Ila kwasasa wanaendelea kutoa elimu na kuvitembelea vikundi na matokeo yanaonekana kwani urejeshaji unaenda vizuri.

Fatuma alisema ,kabla ya kuvikopesha vikundi,kwa mujibu wa mpango kazi wa idara wanavitembelea vikundi hivyo ili kuvihakiki kama vina sifa pamoja na kupewa mikataba ya kurejesha.

Kwa upande wake ,mwenyekiti wa jukwaa la wanawake Bagamoyo ,Teddy Davis aliwataka wanawake kuendelea kujituma pasipo kujibweteka na kuwa tegemezi.

Alisema suala la mitaji bado ni gumu kwa akinamama wengi lakini haimaanishi kuacha kutumia kidogo wanachokopeshwa kwa manufaa yao.

Teddy aliwaomba wanawake wasikate tamaa ,waendelee kujiinua kimaendeleo na kiuchumi ili kupambana na umaskini.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania