CURRENT NEWS

Sunday, November 26, 2017

WAZIRI WA HABARI Dkt. HARRISON MWAKYEMBE AMEFUNGUA MASHINDANO YA LIGI KUU YA WANAWAKE TZ.


Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison G. Mwakyembe  leo tarehe 26 Novemba, 2017 amekuwa mgeni rasmi  kwenye ufunguzi wa Ligi Kuu ya Wanawake ya Tanzania uliofanyika mkoani Arusha. 
Katika ufunguzi huo kumechezwa mechi kati ya vilabu vya Panama FC na Alliance School FC ambapo timu ya Alliance iliibuka kidedea kwa kuifunga Panama FC 2-1. 
Akiifungua ligi hiyo, Waziri Mwakyembe ameshukuru TFF na Chama cha Mpira wa Miguu cha Wanawake (TWFA) kwa maandalizi thabiti ya ligi hiyo msimu huu na kuvitaka vilabu vinazoshiriki kuweka mkazo kwenye maandalizi na kuzingatia sheria na kanuni zinazoungoza mpira mpira wa miguu. 
Aidha, Waziri Mwakyembe aliwahakikishia washiriki dhamira ya Serikali katika kujenga mazingira bora ya sekta ya michezo nchini kwa kuwawezesha watoto na vijana kupata mafunzo ya michezo ili kuvitambua na kuvilea vipaji mapema. 
"Michezo kwa sasa ni chanzo kikubwa na cha kuaminika cha ajira duniani, hivyo Serikali ya Awamu ya tano itaendelea kuboresha mazingira ya michezo, na ninyi wanamichezo muweke juhudi binafsi katika kuhakikisha mnafikia viwango vya juu katika michezo yenu". 
Katika ufunguzi huo Waziri Mwakyembe aliambatana na Rais wa TFF, Bw. Wallace Karia na Katibu Mkuu wa TFF, Bw. Wilfred Kidau na Mwenyekiti wa TWFA, Bi. Amina Karuma.

 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania