CURRENT NEWS

Tuesday, November 14, 2017

ZAHANATI TATU ZAFUNGWA CHALINZE KUTOKANA NA UKOSEFU WA WATUMISHI -DKT.HANGAI

 Mganga Mkuu wa  halmashauri ya Chalinze ,Dkt.Rahim Hangai akizungumzia changamoto wanazokabiliana nazo kwenye sekta ya afya  (Picha na Mwamvua Mwinyi)

Mwenyekiti wa  halmashauri ya Chalinze, Saidi Zikatimu akiongea jambo kuhusiana na masuala ya afya  .(Picha na Mwamvua Mwinyi)

Na Mwamvua Mwinyi,Chalinze
Zahanati za Msolwa,Tukamisasa na Mihuga katika halmashauri ya Chalinze Mkoani Pwani ,zimefungwa kwa muda kutokana na ukosefu wa watumishi ,unaodaiwa kusababishwa na zoezi la uhakiki wa vyeti kwa watumishi.
Aidha kati ya  zahanati 39 zilizopo kwenye halmashauri hiyo zahanati 11 zina watumishi mmoja mmoja na nyingine 28 zina watumishi wawili wawili.
Hali hiyo inaathiri utoaji wa huduma za afya katika maeneo zilizopo zahanati hizo na kusababisha wananchi kufuata huduma maeneo mengine .
Mganga mkuu wa halmashauri ya Chalinze ,Dkt.Rahim Hangai alipoulizwa kuhusiana na changamoto hizo alikiri ,na kudai wana upungufu wa watumishi 282 kwasasa,sawa na asilimia 72 .
Alisema awali kabla ya zoezi la uhakiki wa watumishi hao kulikuwa na watumishi 162 na upungufu ni 236 lakini uhakiki ulipofanyika ulibaini mapungufu ya vyeti kwa watumishi 46 ambao waliondolewa hivyo ongezeko la uhaba huo umefikia watumishi 282 .
Dkt.Hangai alieleza kwamba kuhusiana na zahanati kufungwa ,suala hilo nalo limetokana na zoezi hilo kwani ilikuwa ikifanyakazi lakini baada ya hayo ndipo kukawepo pengo hilo .
Alizitaja zahanati zilizokuwa zimefungwa kuwa ni pamoja na Msolwa,Tukamisasa,Mihuga na Visezi ambapo zahanati ya Visezi imeshaanza kazi baada ya kurekebisha taratibu za ndani ya halmashauri .
Dkt.Hangai alielezea,zipo hatua walizozichukua kwa kuingiza taarifa katika vikao husika vya halmashauri na TAMISEMI na wanashukuru wanatarajia kupelekwa watumishi Tisa ambao watasaidia kupangwa kwenye zahanati hizo ili ziendelee kutoa huduma.
Wengine kati ya hao Tisa watasambazwa kwenye zahanati zenye mahitaji makubwa kwa sasa .
"Ikama inatakiwa kila zahanati iwe na watumishi watano hadi saba lakini zahanati zetu 11 hapa Chalinze zina mtumishi mmoja mmoja na nyingine zilizobakia kati ya 39 tulizonazo zina watumishi wawili wawili"
"Baada ya zoezi lile tuliamua kufanya zoezi ili kujua zahanati zetu zimebakiwa na watumishi wangapi wangapi na kujua hali halisi ya watumishi tulionao na ndipo tulibaini hayo" alifafanua Dkt.Hangai.
Nae mwenyekiti wa halmashauri hiyo ,Saidi Zikatimu aliishukuru serikali kwa kuwapangia watumishi Tisa katika Idara ya afya .
Alieleza tatizo la upungufu wa watumishi bado lipo hivyo wanaiomba serikali kuongeza watumishi hao pale kunapotokea mgawanyo ili kupunguza changamoto iliyopo.
Zikatimu alisema zoezi la uhakiki wa vyeti liliathiri kwani licha ya kuwepo kwa uhaba wa watumishi kwenye sekta hasa ya afya na elimu lakini kwasasa umezidi kuwa mkubwa.
Mwenyekiti huyo aliipongeza serikali kwa kubaini watumishi waliokuwa wakila mshahara kinyume na taratibu .
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania