CURRENT NEWS

Monday, December 11, 2017

BALOZI WA KUWAIT NCHINI AL-NAJEM AMKABIDHI DIWANI WA VIGWAZA VIFAA VYA WENYE ULEMAVU NA MABESENI YA AKINAMAMA WAJAWAZITO

 Balozi wa Kuwait nchini ,Mhe.Jasem Al- Najem wa kwanza kushoto akikabidhi vifaa vya watu wenye ulemavu na mabeseni 100 yenye vifaa vya uzazi vyote vikiwa na thamani ya mil.17.5,
  Kwa  diwani wa kata ya Vigwaza Mohsin Bharwani wa pili kutoka kulia. ( 
picha na Mwamvua Mwinyi)
Balozi wa Kuwait nchini ,Mhe.Jasem Al- Najem akizungumza na baadhi ya wananchi wa Vigwaza kwenye zahanati ya Vigwaza Chalinze Bagamoyo Mkoani Pwani baada ya kumkabidhi diwani wa kata ya Vigwaza Mohsin Bharwani vifaa vya watu wenye ulemavu na mabeseni 100 yenye vifaa vya uzazi vyote vikiwa na thamani ya mil.17.5.(picha na Mwamvua Mwinyi)

11,Des
Na Mwamvua Mwinyi,Vigwaza
Balozi wa Kuwait nchini ,Mhe.Jasem Al- Najem amemkabidhi diwani wa kata ya Vigwaza ,jimbo la Chalinze Bagamoyo mkoani Pwani ,Mohsin Bharwani vifaa vya watu wenye ulemavu na mabeseni 100 yenye vifaa vya uzazi vyote vikiwa na thamani ya mil.17.5.

Kati ya fedha hiyo kiasi cha sh.mil .13 ni gharama ya vifaa vya watu wenye ulemavu ikiwemo magongo 20,fimbo za wenye ulemavu 10,fimbo za walemavu wa macho 10,miwani 20 ,mafuta ya wenye ulemavu wa ngozi na viti vya kubebea wagonjwa kwa watu wazima 20 na kwa watoto kumi.

Pamoja na hilo ,sh mil.4.5 ni gharama ya mabeseni 100 yenye vifaa vya akinamama wajawazito kabla na baada ya kujifungua  .

Akipokea vifaa hivyo,kwenye zahanati ya Vigwaza ,diwani wa kata ya Vigwaza Bharwani alimshukuru balozi wa Kuwait nchini Al-Najem na kusema ni balozi wa mfano na anastahili kuigwa .

Alieleza wamekuwa wakishuhudia misaada mingi ikielekezwa mijini lakini balozi huyo amefika kijijini kwa watu wenye shida na wanaohitaji misaada kama hiyo.
Aidha aliwaomba mabalozi wengine waende kwenye kata hiyo ,kuwezesha na kusaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili
"Nilionana na mdau Muntazir Hussein ambae alikuwa kiungo wa kunisaidia kunikutanisha na balozi Al-Najem " alisema Bharwani.
Hata hivyo ,Bharwani alimshukuru balozi huyo kwa jitihada zake za kuwaunga mkono ,kwa niaba ya serikali ya Kuwait na Red Cross Society ya Kuwait kwa msaada huo ambao utawasaidia akina mama wajawazito na wenye ulemavu.
Akikabidhi vifaa hivyo,balozi wa Kuwait nchini Al-Najem alisema amekabidhi vifaa Kwa ajili ya watu wenye ulemavu vyenye thamani zaidi ya dola 6,000 sawa na sh.mil.13 na vifaa vya uzazi mil.4.5.
Alisema mpango huo ulianza kwa kumkabidhi Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Samia Suluhu Hassan vifaa tiba vya uzazi ambavyo vitasambazwa katika hospitali mbalimbali kwa Tanzania Bara na Zanzibar.
Alisema Serikali ya nchi hiyo kwa ushirikiano na Red Cross Society ya Kuwait imetoa vifaa hivyo kama hatua ya kuendelea kudumisha na kuendeleza mahusiano mazuri kati ya nchi hiyo na Tanzania.
 Al- Najem alielezea serikali ya Kuwait itaendelea kusaidia Serikali ya Tanzania katika uimarishaji wa sekta ya afya na elimu nchini .
Alisisitiza vifaa hivyo vifikishwe kwa walengwa ili vilete tija kwa maslahi ya jamii.
Akimshukuru balozi wa Kuwait nchini Tanzania kwa niaba ya wananchi, mwenyekiti wa kijiji cha Vigwaza ,Ramadhani Kirumbi alimpongeza pia diwani kwa kujitoa kutafuta wadau Kwa ajili ya wakazi wa Vigwaza.
Alisema licha ya kupokea vifaa hivyo lakini zahanati ya Vigwaza bado inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maabara,jengo la watoto na wodi ya akina baba.
Kirumbi alisema endapo changamoto hizo zitatatuliwa itawezesha zahanati hiyo kuwa kituo cha afya.

Alimuomba balozi wa Kuwait asichoke kuwashika mkono na kuendelea kuwaunga mkono kwa changamoto nyingine zinazowagusa.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania