CURRENT NEWS

Friday, December 8, 2017

JAFO AMSIMAMISHA KAZI MKURUGENZI WA NKASI KWA UBADHIRIFU Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Seleman Jafo akitoa taarifa kwa waandishi wa Habari Mkoani Dodoma kuhusu kumsimamisha kazi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, Mkoani Rukwa.
3Baadhi ya Waandishi wa Habari wakimsikiliza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Seleman Jafo wakati akitoa  taarifa kuhusu kumpumzisha kazi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi Mkoani Rukwa.


          ..................................................
Angela Msimbira- OR TAMISEMI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Seleman Jafo amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi Bw. Julios Kaondo, mpaka hapo uchunguzi wa awali wa tuhuma zinazokukabili utakapokamilika.

Akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa Habari Mkoani Dodoma Mhe. Selemani Jafo amesema kuwa amemsimamisha kazi Mkurugenzi huyo kutokana na Mamlaka aliyopewa chini ya kifungu Na. 4 (1-5) cha Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka na Wilaya) sura 287 kwa mujibu wa Kanuni ya 36 ya Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2003.

Mhe. Jafo amesema amechukua hatua hiyo kutokana na tuhuma zinazomkabili za kujihusisha na vitendo vya rushwa katika mchakato wa zabuni ya Miradi ya Maji na kushindwa kusimamia manunuzi katika utekelezaji wa miradi ya maji,  katika kijiji cha Kamwanda Wilayani Nkasi  Mkoani Rukwa akiwa ni afisa Masuhuli wa Halmashauri na kusababisha mradi huo kutokamilika kwa wakati.

Mhe. Jafo amesema mradi huo ulikuwa ukigharimu shilingi  bilioni 7 na wenye lengo la kutatua kero ya Maji katika Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi na kuwaletea maendeleeo wananchi wa wilaya  hiyo. 

Mheshimiwa Jafo amesema hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa watumishi wote waliohusika  kukwamisha Mradi wa Maji katika kijiji cha Kamwanda Wilayani Nkasi Mkoani Rukwa ikiwa ni fundisho kwa watumishi wasiowaaminifu na wasiofanya kazi kwa kuzingatia sheria za utumishi wa umma.

“Jiepusheni na tabia ya baadhi ya watumishi walioko katika Wizara mbalimbali  kufanya vitendo vya udanganyifu, endapo itagundulika hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa wahusika wote”Amesema Jafo

Ametoa wito kwa Wakurugenzi , Wakuu wa Idara, pamoja na watumishi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini  kutojihusisha na vitendo vya rushwa  katika kutekeleza miradi  mbalimbali ya maendeleo.kwa kushindwa  kusimamia  hatua za manunuzi.

Aidha amewataka Watumishi wa umma nchini kufuata kuzingatia sheria,Kanuni  na Taratibu na miongozo iliyopo katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku ili kujiepusha na vitendo vya rushwa katika kuwahudumia wananchi.

 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania