CURRENT NEWS

Thursday, December 7, 2017

JAFO ATANGAZA WALIOCHAGULIWA KUJIUNGA KIDATO CHA KWANZA 2018


  
       
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Seleman Jafo akiongea na Waaandishi wa habari kuhusu matokeo ya uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2018 katika ukumbi wa Mikutano wa Tamisemi Mjini Dodoma.

 
 Baadhi ya waandishi wa Habari wakifuatilia taarifa ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Seleman Jafo kwenye mkutano i kuhusu  matokeo ya uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2018 katika ukumbi wa Mikutano wa Tamisemi Mjini Dodoma.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Seleman Jafo akifafanua jambo wakati akiongea na Waaandishi wa habari kuhusu  matokeo ya uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2018 katika ukumbi wa Mikutano wa Tamisemi Mjini Dodoma.

......................................................................................................................
Angela Msimbira – OR-TAMISEMI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Seleman Jafo amesema  kati ya wanafunzi 662,035 waliofaulu mtihani wa kumaliza elimu ya msingi  wanafunzi  650,862 sawa na asilimia 98.31 wamechaguliwa  kujiunga na  masomo ya kidato cha  kwanza katika awamu ya kwanza  mwaka 2018

Akitangaza matokeo ya uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2018 Tanzania Bara kwenye kikao na waandishi wa habari leo katika ofisi za Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe Jafo amesema kuwa idadi wa wanafunzi   mwaka huu imeongezeka  kwa wanafunzi 124,209 ambapo ni sawa na asilimia  23.58 ikilinganishwa na wanafunzi 526,653 waliochaguliwa awamu ya kwanza kuingia kidato cha kwanza mwaka 2016.

Amesema kuwa wanafunzi 1912 wenye uhitaji maalum (pupils with special needs) waliofaulu mitihani ya darasa la saba  wamechaguliwa  kujiunga  na masomo ya kidato cha kwanza mwaka 2018 kwenye shule za sekondari za Serikali.

Mhe. Jafo amefafanua kuwa wanafunzi  11,173 sawa na asilimia 1.69 ya waliofaulu hawakupata nafasi ya kuchaguliwa  kujiunga  na kidato cha kwanza katika awamu ya kwanza  ya uchaguzi  kutokana na uhaba  wa miundombinu ya elimu hususani  vyumba vya madarasa kwenye baadhi ya Halmashauri ya  Mikoa ya Lindi (170), Mbeya (3,092), Rukwa (4,091), Manyara (1,268), Katavi (976) na Simiyu (1,576).

Amesema kuwa Halmashauri ambazo zimeshindwa kuwapangia wanafunzi wote waliofaulu nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza ni Halmashauri za Lindi wanafunzi (80) Mbeya (207),Halmashauri ya  Jiji la Mbeya  ( 1,227), Mbarali (1,578),  Kalambo (166), Nkasi (1,318), Halmashauri ya Wilaya ya  Sumbawanga (1,054), Halmashauri ya Manispaa  ya Sumbawanga (1,553), Babati (581). Hanang (687), Mpanda (262), Nsimbo (714), Halmashauri ya Mji wa Bariadi (369) na Halmashauri ya Wilaya ya Busega (1,207).

Mhe. Jafo amewaagiza Wakuu wa Mikoa ambayo haijakamilisha ujenzi wa miundombinu hasa ya vyumba vya madarasa  kuhakikisha wanakamilisha hadi kufikia mwezi februari, 2018 ili wanafunzi watakaochaguliwa kwenye awamu ya pili wapate nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2018.

“Lengo la Serikali  ni kuhakikisha kuwa wanafunzi wote waliofaulu mtihani wa darasa la saba wanapata nafasi  ya kujiunga  na masomo ya kidato cha kwanza  nimeshatoa maelekezo  kwa wakuu wa mikoa kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wanapata nafasi  ya kujiunga na kidato cha kwanza kwa mwaka 2018” Amesema Jafo

Mhe. Jafo amesisitiza kuwa  walezi na wanafunzi ambao watakosa nafasi  katika awamu ya kwanza ya uchaguzi  kuwa wavumilivu wakati mikoa inajiandaa kwa ajili ya kuwapokea wanafunzi wote kuanza na masomo ya kidato cha kwanza.

Amewaagiza  waalimu  na watendaji wa elimu  katika ngazi zote nchini kuongeza  bidii katika usimamiaji na ufuatiliaji wa utoaji wa elimu nchini na kushirikiana na wadau wa elimu  kukamilisha majengo na kuandaa mazingira  ya kuwapokea wanafunzi  wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza  2018 bila vikwanzao vikiwemo michango na ada ili  kutekeleza sera ya utoaji wa elimu  msingi bila malipo.

Aidha amewaomba Wazazi, Walezi na jamii kwa ujumla kushirikiana na Wilaya, Halmashauri na shule, kuhakikisha kwamba wanafunzi  wote waliochaguliwa wanaandikishwa , wanahudhuria na kubaki shuleni  hadi watakapohitimu  elimu ya Sekondari.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania