CURRENT NEWS

Friday, December 29, 2017

KHERI JAMES: "VIJANA TUJITOLEE, TUSHIRIKIANE PAMOJA"Mwenyekiti UVCCM Taifa Kheri James amewataka Vijana kujitolea na kushirikiana pamoja katika ujenzi wa Jumuiya na Chama ili kumsaidia Rais Magufuli katika kutimiza majukumu yake.
Maneno Hayo yamesemwa  leo na Mwenyekiti wa UVCCM Taifa Kheri James katika mwendelezo wa ziara yake ya mapokezi iyofanyika Kongowe, Kibaha Mjini mkoani Pwani Leo Alhamis Desemba 28, 2017.
"Vijana tuna wajibu wa kujitolea. Mambo ya posho, nauli, chakula yatatucheleweshea maendeleo. Tujitolee katika ujenzi wa chama na jumuiya. Viongozi wa Chama naomba mshirikiane na Vijana. Bila ya ushirikiano hakuna ujenzi imara wa Jumuiya na chama" amesema Kheri James.
Kheri alitumia muda mwingi kueleza majukumu ya Vijana kwa Chama na Serikali na kuhimiza viongozi wa Serikali kuacha majivuno na kushirikiana na Vijana. Kwa wale watakaogoma kutoa ushirikiano kwa Vijana basi watajwe hadharani.
"Vijana pazeni sauti, semeni na muwataje viongozi wanao jitenga na kuwabagua Vijana" alisema Kheri James.
Pia  aliwataka Vijana kutokulewa madaraka,  kwa kutafuta umaarufu usio na tija na kutambua cheo ni dhamana.
"Viongozi Vijana msilewe  madaraka. Tutambue cheo ni dhamana. Kama kuna umaarufu  mzuri ni ule wa kujipambanua kuwa msaada wa Vijana wenzetu." alisema Mwenyekiti UVCCM Taifa Kheri James.
Mwenyekiti hakuchoka kuwaeleza Vijana namna wanapaswa kuenenda kwa kufanya kazi site kwa kufanya hivyo UVCCM itakuwa kimbilio kwa Vijana wengi nchini.
"Matarajio ya Chama na Vijana ni kuona Jumuiya ya Umoja wa Vijana ikiwa kimbilio la vijana wanaokimbizwa na Mgambo, wasio na Ajira, wanaonyanyaswa na wote wanaoonewa kimbilio lao ni UVCCM.
Hatutaki vijana wa Instagram, Twitter na Facebook Tunataka vijana walioko site, vijiweni, shambani huko vijana waporipori wanatuhitaji", alisema Mwenyekiti UVCCM Taifa Kheri James.
Katika ziara ya mapokezi hayo ilihudhuliwa na viongozi mbalimbali wa Chama, Serikali mkoa wa pwani.
Mwenyekiti Kheri alionyesha kuchukizwa vilivyo na kitendo cha Vijana kutumiwa na kisha kutelekezwa na badala yake akasisitiza Vijana wapewe ajira na fursa mbalimbali waweze kujikimu kiuchumi.
"Viongozi sisi tunaumizwa sana na Vijana kutumiwa nyakati za uchaguzi, kwenye fursa na  kwenye neema wanawekwa pembeni. Ni lazima tujenge mazingira ya kuwasaidia Vijana nyakati zote. Mkoa wa Pwani unaongoza sana kwa kasi ya Tanzania ya Viwanda. Ni wajibu viwanda hivi viende sambasamba na kuwajali, kuajili na kuwasaidia Vijana." alisema Kheri James.
Katika hatua nyingine Mwenyekiti Kheri James aliwasisitiza Vijana wa mkoa wa Pwani na kote Nchini kumpa ushirikiano wa kutosha Rais Magufuli ambaye ameonyesha kuwajali sana Vijana nyakati zote.
"Watu wa Pwani Tuungane kuunga mkono Serikali yetu na Rais wetu kwa kufanya kazi. Mhe. Rais Magufuli anawapenda Vijana. Anahitaji kuona mkimpa ushirikiano, mkieleza mema anayoyafanya yeye pamoja na Serikali yake" alisema Kheri James.
Katika ziara hiyo Mkoa wa Pwani Mwenyekiti UVCCM Taifa Kheri James alilakiwa na viongozi mbalimbali wa jumuiya, Chama na Serikali Mkoa wa pwani huku msafara wake akifuatana na  Kaimu Katibu Mkuu UVCCM TAIFA Shaka H. Shaka, Kaimu Katibu Idara ya Siasa, Organaizesheni na mahusiano ya kimataifa Ndugu Mohammed Abdallah, Wajumbe wa Halmashauri Kuu Taifa, Wajumbe wa Baraza kuu la Taifa na Maafisa toka UVCCM Makao Makuu.
#TukutaneKazini
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania