CURRENT NEWS

Monday, December 25, 2017

MGALU AWATAKA MAAFISA MAENDELEO NA WAJASIRIAMALI KUKIMBIZANA NA MAHITAJI YA VIWANDA ILI KUPATA SOKO LA NDANI

 Naibu waziri wa nishati ambae pia ni Mbunge wa viti maalumu mkoani Pwani ,Subira Mgalu Teddy akitembelea mabanda ya biashara mbalimbali za wajasiriamali wakati alipokwenda kufunga maonyesho ya bidhaa za wajasiriamali wilayani Bagamoyo.

Naibu waziri wa nishati ambae pia ni Mbunge wa viti maalumu Mkoani Pwani ,Subira Mgalu akipokea zawadi kutoka kwa Mwenyekit wa jukwaa la uwezeshaji wanawake wilayani Bagamoyo, Teddy Davis wakati alipokwenda kufunga maonyesho ya bidhaa mbalimbali za wajasiriamali wilayani humo .(picha na Mwamvua Mwinyi)

Na Mwamvua Mwinyi,Bagamoyo
NAIBU Waziri wa Nishati ambae pia ni mbunge wa viti maalumu mkoani Pwani,Subira Mgalu ,amewataka wataalamu na maafisa maendeleo ya jamii , washuke viwandani kujua masharti na taratibu ili kuwaandaa wajasiriamali kuzalisha malighafi zinazohitajika viwandani humo .
Aidha ametoa rai kwa wanawake wajasiriamali kukimbizana na fursa za viwanda ili kupata soko na kuondokana na umaskini .
Subira aliyasema hayo wakati akifunga maonyesho ya bidhaa za wajasiriamali yaliyofanyika wilayani Bagamoyo kuanzia desemba 20 hadi 24 mwaka huu.
Alieleza ,wilaya ya Bagamoyo na mkoa wa Pwani kuna viwanda vya kusindika mbogamboga na matunda lakini wanashindwa kuvitumia kuchangamkia soko la ndani.
Alisema maafisa maendeleo waangalie namna watakavyowaandaa wajasiariamali mbalimbali kuzalisha malighafi zinazotakiwa ili kutoa nguvu kazi ,kuviwezesha vikundi na wajasiriamali hao.
"Viwanda tunavyo vingi,tunajivunia uwepo wa viwanda vya matunda na mbogamboga lakini tumewahi kupiga hodi na kuwaeleza utayari wa wajasiriamali wa wilaya na mkoa wetu ili soko la ndani likue?????
" Hatuzuii kuagizwa malighafi nje lakini ,wapo wafanyabiashara wenye bidhaa nzuri ,zenye viwango hapa hapa ,tujitathmini sisi kwanza ili kujikomboa"alisisitiza Subira.
Subira alisema,biashara ni ushindani hivyo aliwataka wanawake kuwa wabunifu wa kutengeneza vitu vyenye ubora na kujitangaza pasipo kufanyabiashara kizamani .
Alimuagiza pia mwenyekiti wa jukwaa la uwezeshaji wilayani hapo kufuatilia kujua taratibu na masharti yanayotakiwa kwenye viwanda hivyo ili wanufaike na viwanda hivyo. 
Akizungumzia suala la asilimia kumi ya kundi la vijana na wanawake kupitia halmashauri ,alisema anajivunia kuwa na halmashauri ya Bagamoyo na Chalinze ,zinajali wanawake na vijana.
Subira alisema kuwa ,amekuwa akilisemea suala hilo na halmashauri hizo kuwa za mfano kwani mwaka huu wa fedha zimetumia takribani mil.400 kwa ajili hiyo.
Aliviasa vikundi vinavyonufaika na mikopo ya halmashauri kuzalisha badala ya kufanyia ufahari mitaani na kurejesha kwa wakati.
"Kuna fursa nyingi za kuwezeshwa mzitumie ,twendeni mbali zaidi ,tuambatane tukazitafute fursa huko zilipo ikiwemo bank ya posta,bank ya wanawake (TWB)na taasisi ya uwezeshaji chini ya serikali , inatoa udhamini kwa umoja wa vikundi."alisema Subira.
Nae mwenyekiti wa jukwaa la uwezeshaji wanawake wilayani Bagamoyo ,Teddy Davis alisema lengo la kuandaa maonyesho hayo ni kukutana wajasiriamali.
Lengo jingine ni kutafuta masoko na kukutana wajasiriamali na majukwaa 11 ya kata wilayani hapo na wadau wa maendeleo na kupata mafunzo .
Teddy alisema wanakabiliwa na changamoto ya uhitaji wa mitaji,ukosefu wa masoko,ukosefu wa ujuzi na elimu na masharti magumu kwa taasisi zinazotoa mikopo .
Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Bagamoyo ,dk.Shukuru Kawambwa alisema vikundi vya ujasiriamali pamoja na taasisi vipatavyo 26 katika jimbo la hilo vimewezeshwa sh.milioni 15.400 kupitia mfuko wa jimbo hilo .

Dk.Kawambwa alisema,fedha za mfuko wa jimbo ni ndogo lakini zina manufaa kwa wale wanaozipangia mipango yenye tija .

Mkurugenzi wa halmashauri ya Bagamoyo ,Fatuma Latu ,alisema mwaka 2016-2017 halmashauri hiyo ilitoa mapato yake ya ndani kwa asilimia 100 na kuwezesha asilimia 5 kwa wanawake na asilimia 5 vijana.

 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania