CURRENT NEWS

Wednesday, December 6, 2017

NAIBU WAZIRI AWESO AZITAKA TAASISI KULIPA MADENI YA ANKARA ZA MAJI


 Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso akizungumza na watumishi
wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira mjini Moshi (MUWSA) alipotembelea
mamlaka hiyo mkoani Kilimanjaro.

Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso akiwa kwenye picha ya pa
moja na menejimenti ya Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira mjini Moshi
(MUWSA) alipotembelea mamlaka hiyo mkoani Kilimanjaro. 

Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso (mbele kulia) akiwa na
Msimamizi wa Mradi, Mhandisi Richard Magwizi (kulia) wakipita kwenye moja
sehemu ya mradi wa Same-Mwanga, mkoani Kilimanjaro.
        ......................................................................................................................
Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso amezitaka taasisi za Serikali kulipa
madeni ya ankara za maji kwa mamlaka za maji nchi nzima, ili ziweze kutoa huduma
bora ya maji inayokidhi mahitaji ya wananchi.

Aweso alitoa rai hiyo alipokuwa akizungumza na watumishi wa Mamlaka ya Maji na
Usafi wa Mazingira mjini Moshi (MUWSA), alipotembelea mamlaka hiyo kwa dhumuni la
kujionea utendaji wa mamlaka hiyo mkoani Kilimanjaro.

‘‘Mamlaka za Maji nchini zimeendelea kukabiliwa na changamoto ya malimbikizi
makubwa ya madeni ya ankara za matumizi ya maji kwa taasisi za Serikali, ambazo
zimekuwa zikipata huduma ya maji na kushindwa kulipa kwa wakati, ambapo hadi
kufikia Machi 2017 deni lilikuwa limefika Sh. bilioni 39.94’’, alisema Naibu Waziri.

‘‘Kuna haja taasisi za Serikali kulipa madeni yao yote kwa kuwa wamekuwa kikwazo
katika maendeleo ya Sekta ya Maji, kwani mamlaka nyingi zimekuwa zikikosa fedha za
kutosha kwa ajili ya kujiendesha na kupeleka maji kwa wananchi. Wakilipa madeni hayo
itaziwezesha mamlaka zetu kujiendesha kwa ufanisi na kufikia lengo la kuwapa
wanachi huduma bora ya maji iliyo endelevu,’’ alisema Aweso.

Aweso alisema wizara itaangalia jinsi ya kufanikisha ulipwaji wa madeni hayo, ili
kuimarisha huduma ya maji mijini kufikia asilimia 86 mwezi Juni, 2017 na 95 ifikapo
mwaka 2020 kulingana na Ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Aidha, Naibu Waziri Aweso ametembelea mradi wa maji wa Same-Mwanga ambao
unatekelezwa katika Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro kwa nia ya kuhakikisha
unatekelezwa vya ubora na kukamilika kwa wakati.

Mradi huo mkubwa unategemea kuhudumia zaidi wa watu 400,000 wa vijiji 38 katika
Wilaya za Same, Mwanga na Korogwe, unatarajiwa kugharimu zaidi ya Dola za

kimarekani milioni 300 na kukamilika Mei, 2019.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania