CURRENT NEWS

Friday, December 22, 2017

RAIS WA ZANZIBAR DKT.ALI MOHAMED SHEIN ATOA PONGEZI KWA TIMU YA ZANZIBAR HEROES RAIS  wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameendelea kutoa pongezi kwa timu ya Taifa ya Zanzibar, ‘Zanzibar Heroes’ kwa kuirudishia Zanzibar heshima yake na sasa imekuwa inasemwa vizuri kutokana na jinsi timu hiyo ilivyoonesha kiwango safi cha kusakata soka.


Dk. Shein aliyasema hayo leo huko katika viwanja vya Ikulu mjini Zanzibar katika chakula maalum cha mchana alichowaandalia wachezaji wa Timu ya Zanzibar Heroes pamoja na viongozi wake wote baada ya kufanya vyema katika mashindano ya mwaka huu ya Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati ‘CECAFA’ yaliofanyika nchini Kenya.

Aliongeza kuwa wachezaji hao wa ‘Zanzibar Heroes’ wamewanawa uso Wazanzibari wote kutokana na uwezo na nguvu ya mpira waliouonesha na hadi kufikia fainali za mashindano hayo ya CECAFA.

Dk. Shein alieleza kuwa watu waliowengi hawakuifikiria timu hiyo ya Zanzibar kama itafika ilipofika na pia baadhi ya watu hawakuwa wakiisema vizuri lakini hatimae imedhihirisha kuwa Zanzibar ina historia nzuri ya soka na kuondosha usemi kuwa ‘Chenga twawala’.

Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa kuwaandalia chakula hicho cha mchana hivi leo ni mwanzo tu wa pongezi zake lakini kuna zawadi tatu kubwa amewaandalia ikianzia taarab maalum ya kikundi cha Taifa cha Zanzibar pamoja na zawadi nyengine mbili kubwa ambazo hazijawahi kutokea na kukataa kuzitaja hii leo na kuahidi kuzitaja hapo kesho.

Nae Kocha Mkuu wa Zanzibar Heroes Hemed Suleiman Moroko alitoa pongezi kwa Rais Dk. Shein pamoja na kwa viongozi wengine wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kocha Abdulkhani Msoma pamoja na Mwalimu Abdalla Mwinyi kutokana na nasaha zake za kutaka wachezaji wawe na silka na hulka za Kizanzibari wakiwa katika mashindano hayo ambazo ndizo zilizowasaidia.

Pamoja na hayo, Kocha mkuu huyo alitoa ombi maalum kwa Rais Dk. Shein kumualika Rais wa Shirikisho la Soka Barani Afrika Ahmad Ahmad kuja Zanzibar ili kufanya mazungumzo nae kwa ajili ya kuzungumza mustakbali wa Zanzibar katika soka kimataifa. 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania