CURRENT NEWS

Saturday, December 16, 2017

SAMAKI WACHANGA NA WAZAZI WAKAMATWA KATIKA SOKO LA SAMAKI LA KIMATAIFA MWALONI KIRUMBA MWANZA.


Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Mhe.Abdalla Ulega leo amekamata samaki aina ya sangara wachanga na wazazi tani 11 waliokuwa wakitoroshwa kwenda nchi jirani ya DRC kwa kukwepa kulipa kodi.

Samaki hao tani 11 walitakiwa kulipiwa ushuru wenye thamani ya Tsh.99,000,000 badala yake wafanyabiashara hao wa kikongo walikwepa kulipa ushuru huo kwa kuchukua kibali kinachoonyesha samaki hao wanaenda kuuzwa Tunduru mkoani Ruvuma

Akiongea na uongozi wa halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Mhe Ulega amesema kuwa watumishi wa serikali watangulize Uzalendo katika nafasi zao wanazozitumikia kuliko kuendekeza rushwa.

"Jamani naombeni sana msimamieni sheria Ili kulinda Rasilimali zetu zisitoroshwe kwenda nje bila kulipiwa Kodi,tumungeni Mkono Rais wetu John Pombe Magufuli katika kuhakikisha Rasilimali hizi zinawanufaisha wananchi na sio watu wachache"alisema.

Ulega amesema kuwa  ni kinyume cha sheria kuvua samaki wachanga na wazazi, na ameuagiza uongozi wa Manispaa ya Ilemela kwa kupitia Mkurugenzi wake kuhakikisha wanasimia sheria ipasavyo na hakuna samaki wachanga na Wazazi kuvuliwa.

"Ikitokea wakati wa ukaguzi wenu mmekamata samaki wachanga au wazazi taifisheni na sheria ichukue mkondo wake kwa yoyote anayehusika au anayevunja sheria kwa kujua au kutokujua"alisema Ulega.

Katika hatua nyingine Mhe. Naibu Waziri Abdalla Ulega alipata fursa ya kuhutubia wafanyabishara katika soko hilo,mara nyingi Naibu Waziri alikatishwa hotuba yake kwa kushingiliwa na umati mkubwa wa wafanyabiashara waliokusanyika sokoni hapo.

Aidha wafanyabiashara hao walimweleza Naibu Waziri changamoto wanazokumbana nazo hapo sokoni ikiwa ni pamoja na ukosefu wa maji safi na salama na ubovu wa miundombinu ya vyoo katika soko hilo.

Mhe.Ulega amempa siku tatu Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela Bw.John Wanga kuhakikisha maji na miundombinu ya vyoo sokoni hapo inashugulikiwa ndani ya siku tatu.

"Mkurugenzi nakuagiza kufikia Jumatatu Decemba 18 changamoto ya maji safi na Salama na Miundombinu yote ya vyoo vya soko hili viwe vimepatiwa Ufumbuzi".Alisema Ulega.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania