CURRENT NEWS

Wednesday, December 6, 2017

SERIKALI YASAINI MKATABA WA USHIRIKIANO KATIKA MIRADI YA MAENDELEO YA WANAWAKE.

 Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bibi. Sihaba Nkinga (kushoto) na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake (UN Women) Bibi. Hodan Addou (kulia) wakitia saini Mkataba wa Makubaliano ya Utekelezaji wa Miradi ya Wanawake utakaodumu kwa kipindi cha Mwaka mmoja (2017/2018) katika ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam Desemba 05, 2017.
Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bibi. Sihaba Nkinga (kushoto) na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake (UN Women) Bibi. Hodan Addou (kulia) wakikabidhiana  Mkataba wa Makubaliano ya Utekelezaji wa  Miradi ya Wanawake utakaodumu kwa kipindi cha Mwaka mmoja (2017/2018) katika ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam Desemba 05,2017. 

                  ..........................................................................................
Na Kitengo cha Mawasiliano WAMJW

 Serikali imesaini Mkataba wa makubaliano wa Miradi ya Wanawake Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake (UN Women).

 Akitia saini Mkataba huo kwa niaba ya Serikali Katibu Mkuu wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto Bibi. Sihaba Nkinga amesema kuwa  Mkataba huo unahusu Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo kwa Wanawake  Watanzania.

 Bibi Sihaba Nkinga ameongeza kuwa Mkataba huo  umeainisha maeneo ya ushirikiano ambayo ni  Utekelezaji wa Mkataba wa Kimataifa wa Kuondoa Ubaguzi Dhidi ya Wanawake (CEDAW),Kufanya  Mapitio ya Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia (2000,  Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) na utekelezaji wa Mpango wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (2017/2021).

 Aidha Bibi Sihaba Nkinga amesisitiza  kuwa Mkataba huo utasaidia kuendeleza jitihada za Serikali ya Tanzania na Wadau mbalimbali katika kufikia Usawa wa Jinsia na Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi.

 “ Makubaliano haya yatasaidia sana katika kusaidia juhudi za Serikali na Wadau  kumuwezesha wanawake wa Tanzania kujikwamua  kiuchumi na kufikia usawa wa kijinsia”alisema Bibi. Sihaba.

 Kwa upande wake Mwakilishi wa UN Women - Tanzania, Bibi Hodan Addou amesema kuwa pamoja na jitihada zilizofanyika kati ya Shirika hilo na Serikali katika kuwaletea Maendeleo Wanawake, jitihada zingine zitakazofanyika ni kusaidia juhudi zinazofanywa na Serikali ya Tanzania za kuongeza Ushiriki wa Wanawake katika Uongozi na kutoa maamuzi kwenye  ngazi zote. 

 “Tunaahidi kushirikiana naSerikali katika kumuinua na kumuendeleza mwanamke wa Kitanzania katika kujikwamua kiuchumi” alisema Bibi Hodan.


 Mkataba huo wa Mwaka mmoja (2017/2018) unalenga kumuwezesha mwanamke wa kitanzania kujiajiri, kujitegemea na hivyo kujikwamua kiuchumi kwa  kujiongezea kipato binafsi, familia na taifa kwa ujumla.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania