CURRENT NEWS

Wednesday, January 31, 2018

CCM KIBAHA MJINI YAKAMIA KUUZIKA UPINZANI UCHAGUZI 2019/2020

 Mwenyekiti wa Jumuiya wa Wazazi Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kibaha Mjini,Edwin Shunda (mwenye kofia) akishirikiana na wajumbe wa jumuiya hiyo kufyeka katika mazingira ya jengo la chama hicho wakati wa maadhimisho ya kutimiza miaka 41 ya chama hicho wilayani Kibaha leo,yaliyofanya na jumuiya ya wazazi Mjini hapo
 Mwenyekiti wa Jumuiya wa Wazazi Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kibaha Mjini,Edwin Shunda (mwenye kofia) akishirikiana na wajumbe wa jumuiya hiyo kuzoa takataka na kuweka katika vifaa vya kubebea uchafu katika mazingira ya jengo la chama hicho wakati wa maadhimisho ya kutimiza miaka 41 ya chama hicho wilayani Kibaha leo,yaliyofanywa na jumuiya hiyo.(picha na Mwamvua Mwinyi)
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kibaha,Maulid Bundala (katikati) akikabidhi kadi ya CCM kwa Aliyekuwa Mgombea wa udiwani kupitia Chama cha Wananchi (CUF) 2015,kata ya Kongowe ,Mathas Kambi (anaepokea kadi) baada ya jumuiya ya wazazi CCM Wilaya ya Kibaha kufanya usafi katika jengo la chama hicho wakati wa maadhimisho ya kutimiza miaka 41 ya chama hicho wilayani Kibaha leo,Kulia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Kibaha mjini, Edwin Shunda.(Picha na Mwamvua Mwinyi)

Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)Mjini Kibaha, Mkoani Pwani ,Maulid Bundala amezitaka jumuiya zote za CCM na chama kijumla ziungane kuendelea kuisemea serikali na utekelezaji wa ilani ili waliozoea kukosoa wakose ya kusema.

Aidha amewaasa wanachama na viongozi wa chama wilayani hapo,kujipanga ili kuuzika upinzani katika chaguzi zijazo 2019/2020.

Akifungua baraza la jumuiya ya wazazi ya CCM Mjini Kibaha ,wakati jumuiya hiyo ikiadhimisha miaka 41 ya CCM ,Bundala alisema wanaCCM wasiwe watu wakusemewa bali wajifunze kusema wenyewe.

Alisema wawe wamoja na kukiimarisha chama ili ikifika 2019-2020 mitaa na kata zote ziwe mikononi mwa Chama hicho.

"Tembeeni kifua mbele ,macho mita 100 bila kuogopa ,elezeni anayofanya mwenyekiti wetu wa CCM Taifa na rais Dk.John Magufuli"

"Msisubiri kusemewe na watu  wasiolitakia mema taifa letu,tusingojee wapinzani wazushe hoja zinazopotosha kwa wananchi na kuikosoa serikali" alisema Bundala.

Bundala aliwaasa viongozi wa chama kila mmoja kwa nafasi yake kumsaidia Mh.Rais kusimamia utekelezaji wa ilani katika ngazi za chini .

Aliwataka kuondoa uoga kwa kuwasimamia na kuwakosoa pale wanapokosea watendaji ,madiwani na halmashauri .

"Tusimwachie Rais pekee asimamie mambo yote peke yake ,tukikaa nyuma nyuma ndio maana tunauziwa mbuzi kwenye gunia ,tuhakikishe halmashauri zinatimiza miradi pia huduma stahiki kwa wananchi" alisema Bundala.

Bundala aliomba vijana waache kukaa vijiweni,kucheza pool wajitume ili kujikomboa na umasikini.

Hata hivyo ,alieleza viongozi wa chama nao wasiwe wababaishaji wafanyekazi ama biashara na kazi kwani wao ni mfano wa kuigwa.

Nae mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi Kibaha Mjini ,Edwin Shunda alisema wamejipanga kurejesha mitaa na kata 2019-2020 .

Shunda alisema ,pia wanatarajia kuondokana na hali ya kuwa tegemezi kwa kuanzisha miradi ya jumuiya hiyo .

Katika maadhimisho hayo ,jumuiya hiyo ilifanya usafi eneo la chama Mjini Kibaha ambapo pia aliyekuwa mgombea wa udiwani kupitia CUF ,kata ya Kongowe ,2015,Mathas Kambi alijiunga na CCM.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania