CURRENT NEWS

Friday, January 19, 2018

DC MTATURU ARIDHISHWA NA UKARABATI NA UPANUZI WA MRADI WA MAJI WA NTEWA.

             Miundombinu ya kuvunia maji ya mvua iliyopo katika shule ya msingi ya  Ntewa.

 Mhandisi wa kampuni ya Sumaco Bakari Luanda akitoa maelezo mbele ya mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu aliyekuwa anakagua malambo ya kunyweshea maji ikiwa ni sehemu ya ukarabati na upanuzi wa mradi wa huo.
Mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu akisikiliza maelezo ya moja ya miundombinu ya mradi huo.

 Mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu akizungumza na wananchi wa Kata ya Ntuntu katika mkutano wa hadhara mara baada ya kukagua mradi huo.
Mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu akisikiliza maelezo  kutoka kwa mwenyekiti wa kamati ya watumia maji.

 Wananchi wa kijiji cha Kata ya Ntuntu wakiwa katika mkutano wa hadhara  wakimsikikiza mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu hayupo pichani aliyeenda kukagua ukarabati na upanuzi wa mradi wa maji wa Ntewa na kuzungumza na wananchi.
Mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu akisalimiana na  walimu wa shule ya msingi ya Ntewa alipokuwa kwenye ziara ya kukagua mradi wa maji wa Ntewa na kuzungumza na wananchi.
   .............................................................................................................................

MKUU wa wilaya ya Ikungi mkoani Singida mheshimiwa  Miraji Mtaturu amekagua ukarabati na upanuzi wa mradi wa maji wa Ntewa uliopo kata ya Ntuntu na kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi huo.
Mradi huo unaofanyiwa ukarabati na upanuzi kwa thamani ya shilingi milioni 339 na mkandarasi  Sumaco Company LTD ni Utekelezaji wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji(WSDP )inayolenga kusogeza maji karibu na wananchi. 

Akizungumza mbele ya mkuu wa wilaya huyo,mhandisi wa kampuni hiyo Bakari Luanda amesema mradi huo umekamilika kwa asilimia 96 na  wanatarajia kuukamilisha na kuukabidhi tarehe 26 January baada ya marekebisho waliyoagizwa na Mhandisi wa halmashauri kukamilika.

Kwa upande wake kaimu Mhandisi wa maji wilaya Marycela Hagila akisoma taarifa ya mradi huo amesema kazi hiyo imelenga kuongeza vituo vya kuchotea maji 16,malambo mawili ya kunyweshea mifugo,choo matundu 6 na Miundombinu ya kuvunia maji ya mvua katika shule ya msingi ya Ntewa.

“Mradi huu wa maji wa Ntewa unategemea kisima kirefu kama chanzo cha maji,pampu maji zinazoendeshwa kwa kutumia mafuta ya dizeli,vituo viwili vya kuchotea maji na tanki la kuhifadhia maji lenye ujazo wa lita elfu 50,000,”alisema Hagila.

Akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara mara baada ya kukagua mradi huo mh Mtaturu amesema serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Pombe Magufuli imedhamiria kutatua changamoto ya maji mijini na vijijini kupitia kampeni maarufu ya kumtua mama ndoo ya maji kichwani kwani lengo likiwa wananchi wapate maji si zaidi mita 400.

“Ndugu wananchi nimekuja kutembelea mradi huu uliokuwa ukabidhiwe mwezi novemba mwaka jana,nimeona na nimeridhishwa na hatua iliyofikiwa,tumeona kupitia mradi huu kutakuwa na ongezeko la vituo vya kuchotea maji 16 toka vituo viwili vilivyokuwepo awali,wananchi watachota maji kwenye vitongoji vyao hii ni dhamira ya dhati ya serikali katika kutekeleza ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM)kama  iliyoahidi,naomba muutunze”alisema Mtaturu.

Alizielekeza jumuiya za watumia maji KIDINDI kusimamia mradi huo ili huduma itolewe kwa tija kwa wananchi  kama ilivyolengwa huku akiahidi kuchangia shilingi laki 5 katika ujenzi wa maabara ya shule ya sekondari ya Ntuntu.

Diwani wa kata ya Ntuntu Omari Toto ameishukuru serikali kwa hatua hiyo kubwa ya kuboresha upatikanaji wa maji kwa kuwa awali hali ilikuwa mbaya sana na kumpongeza mkuu wa wilaya hiyo kwa kusimamia shughuli za maendeleo.


“Ndugu zangu wananchi wa Ntuntu serikali imetuletea mradi huu ambao ni faida kwetu,tuutunze,tunaona chini ya mkuu wa wilaya yetu hii usimamizi wa shughuli za maendeleo upo,na leo hii ni mara yake ya pili kuja kututembelea katika muda mfupi nimefarijika sana,”alisema diwani huyo.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania