CURRENT NEWS

Tuesday, January 9, 2018

HEKARI 2,737 ZA MAZAO ZALIWA NA KUHARIBIWA NA PANYA HUKO CHALINZE/WAKULIMA WALILIA MAZAO YAO

 Diwani wa kata ya Kibindu ,Ramadhani Mkufya ,akionyesha baadhi ya mashamba ya mahindi ,yaliyoliwa na kuharibiwa na panya walioibuka ,huko Kibindu ,Chalinze, Mkoani Pwani (picha na Mwamvua Mwinyi)


Na Mwamvua Mwinyi,Chalinze 
 Hekari 2,737 za mazao hasa mahindi katika halmashauri ya Chalinze ,mkoani Pwani ,zimeliwa na kuharibiwa na wimbi la panya ambalo limejitokeza tangu mwezi Novemba mwaka 2017 hadi sasa. 
 Kutokana na tatizo hilo ,wakulima wa kata tano za Kibindu,Miono,Mandela ,Pera na Mbwewe wamepata hasara kutokana na kuliwa mazao yao. 
 Akielezea kuhusiana na panya hao wanaoathiri mazao ya wakulima ,afisa kilimo wa halmashauri ya Chalinze ,Jovin Bararata alikiri kuwepo kwa tatizo hilo . 
 Alisema walifikishiwa taarifa hiyo miezi miwili sasa ambapo walienda kwenye mashamba ya wakulima na kujionea athari kubwa iliyopo. 
 Hata hivyo Bararata alisema ,zipo hatua walizozichukua kwani inapotokea tatizo kama hilo ,hulazimika kupeleka taarifa kitengo maalumu cha wizara ya kilimo kinachojishughulikia kuzuia na kudhibiti baa la panya kilichopo Morogoro. 
 Alieleza ameongea na wataalamu wa kitengo hicho na kuelezwa kuwa kinaendelea na jitihada za kupata sumu itakayosaidia kuua na kuondoa panya hao. 
 Afisa kilimo huyo wa halmashauri ya Chalinze ,alisema wakati wakisubiri kupelekwa kwa sumu hiyo ,wamewashauri wakulima kutumia mbinu za asili zitakazowasaidia kupunguza kero hiyo . Bararata alisema ,wanachotakiwa kufanya kwasasa ni kuchimba mashimo makubwa kwenye mashamba yao ,kisha wanaweka ndio na kujazaa maji ,pamoja na mahindi,mpunga ama chakula chochote ambapo panya wakiingia watakufa . 
 "Hiyo ni njia rahisi ya asili ambayo inatumika kusaidia kupambana na baa la panya endapo likijitokeza kama hivi " alifafanua Bararata. 
 Nae Diwani wa kata ya Kibindu Ramadhani Mkufya ,alisema wakulima walio wengi wamelima kwa wingi msimi huu, lakini limejitokeza wimbi la panya ambapo kwa uhakika, baadhi ya wakulima hakuna watakachovuna. 
 Alisema uongozi wa kata umefikisha taarifa ya jambo hilo katika Idara ya kilimo ,halmashauri ya Chalinze ,ambapo wataalamu walifika kujionea hali halisi ya uharibifu uliopo na kusema watapeleka taarifa kitengo husika kinachoshughulika na baa la panya kilichopo Morogoro. 
 Mkufya alisema tangu hapo hawajui kinachoendelea , hivyo wanasubiria kupelekwa sumu ili kuzuia panya wasiharibu maeneo mengine . 
 Baadhi ya wakulima wa kata ya Kibindu ,walishangaa kuona ni kipindi kirefu kimepita tangu kutolewee kwa taarifa hizo na majibu yakiendelewa kutolewa kuwa jitihada zinaendelea za kupeleka sumu. ,
"Lakini hatujaletewa hiyo sumu ,hivyo haijulikani hiyo sumu huwa haipo,kwenye kitengo hicho hadi kutokee tatizo la aina hiyo ndipo wahangaikie kutafuta sumu ilipo"walihoji. 
 Kwa mujibu wa afisa kilimo,sekretarieti ya mkoa wa Pwani ,George Kapilima alipokea taarifa ya tatizo la panya katika maeneo ya Kibiti na Chalinze lakini Kibiti hakuna athari kubwa kama iliyotokea Chalinze. 
 Kutokana na athari iliyojitokeza Chalinze aitaka halmashauri ya Chalinze kufanya tathmini ya tatizo la panya na kuchukua hatua ya kununua sumu hiyo wakati kitengo husika kikiendelea kulifanyia kazi. 
 Kapilima alisema ameshazungumza na afisa kilimo wa halmashauri ya Chalinze na kumtaka aandike barua na kuipelekea kitengo cha kuangamiza panya Morogoro ili waweze kuelekezwa mahali inaponunuliwa sumu ama dawa zinazotumika kuua panya hao. 
 Alisema ,endapo inabuka tatizo la panya ,zige na viwavijeshi jukumu la kutoa dawa huwa ni la wizara ya kilimo hivyo wakati wakiendelea na mchakato ni lazima ichukuliwe hatua mbadala itakayowasaidia kwa sasa.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania