CURRENT NEWS

Monday, January 8, 2018

JAFO AKEMEA UTATU USIO MTAKATIFU KATIKA MANUNUZI YA UMMA TARURA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Selemani Jafo(kulia) akiteta jambo na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe.Amos Makala wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya wataalaamu wa Wakala wa Barabara mijini na Vijijini(TARURA) yaliyofanyika Jijini Mbeya.

Mkurugenzi wa barabara Vijijini Mhandisi Abdul R.Digaga akitoa taaarifa ya awali kwa mgeni rasmi kuhusiana na mafunzo ya masuala ya Ununuzi wa Umma na Usimamizi wa Mikataba ya Ujenzi na matengenezo ya barabara na Maadili katika kazi za TARURA yaliyofunguliwa leo Jijini Mbeya.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Selemani Jafo akizungumza na wahandishi, wajumbe wa bodi ya zabuni na wataalamu wengine wa TARURA wa mikoa saba ya Nyanda za juu kusini wakati wa mafunzo ya Ununuzi na maadili yanayofanyika Jijini Mbeya.

Baadhi ya wataalamu wa TARURA wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Nchi,OR-TAMISEMI Mhe.Selemani Jafo wakati akifungua mafunzo ya Manunuzi na Maadili Jijini Mbeya.

Katika Picha ya pamoja ni ni Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI Mhe.Selemani Jafo(Aliyekaa katikati) pamoja na viongozi wa Mkoa pamoja na TARURA na washiriki wa mafunzo kutoka Mkoa wa Njombe.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Selemani Jafo(kushoto) akiteta jambo na Mkurugenzi wa barabara Vijijini Mhandisi Abdul R.Digaga baada ya ufungzuzi wa mafunzo ya TARURA jijini Mbeya.

    .............................................................
Nteghenjwa Hosseah, Mbeya

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo amewataka watumishi wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijiji(Tarura) kuvunja utatu usio mtakatifu katika kazi za ujenzi na matengenezo ya barabara zinazoendelea kutangazwa katika maeneo mbalimbali Nchini.

Waziri Jafo ameyasema hayo wakati wa kufungua mafunzo ya Siku Sita ya watalaam wa Tarura kutoka katika Mikoa saba ya Nyanda za Juu kusini kuhusiana na masuala ya Ununuzi wa Umma na Usimamizi wa Mikataba ya Ujenzi na matengenezo ya barabara na Maadili katika kazi za TARURA yenye   takribani miezi sita sasa tangu kuanzishwa kwake.

Waziri Jafo amesema "Ninaposema Utatu mtakatifu namaanisha Afisa Manunuzi, Mhasibu na Mhandishi wa Tarura katika eneo husika hawa ndio huwa wanaamua nani apewe kandarasi kwa mujibu wa mahusiano na makubaliano wanayoyajua wao.

" Huu Utatu usio mtakatifu katika kazi za Umma ufe kuanzia leo na Mkandarasi apewe kazi kwa kuzingatia uwezo wake wa kitaalam na kifedha katika kukamilisha kazi hiyo na sio mahusiano na makubaliano nje ya vigezo vilivyowekwa".

Amesema kuna mahusiano ya karibu sana na Rushwa na inafahamika wazi kuwa Rushwa hupofusha wataaalam kuona na kutathmini uwezo wa Mzabuni, huzorotesha kazi iliyopangwa kufanyika na kuwanyima wananchi haki yao ya Msingi ya huduma bora za barabara na amebaini wakiendeleza kasumba hiyo  watachukuliwa  hatua za kisheria na kinidhamu.

Akimkaribisha Waziri Jafo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Amos Makala amesema wamejiandaa kikamilifu kusimamia kazi za Tarura na baada ya uzinduzi wa kitaifa walizindua tena Kimkoa ili kuwafahamisha wananchi wa Mkoa huu umuhimu wa Taasisi hii, ili waweze kumiliki Kazi zinazofanywa na Tarura na kuwaeleweshe lengo la kutoka kazi za barabara kutoka Halmashauri na kusimamiwa na Tarura.

“Tarura imekuja kuboresha kazi nzuri iliyokuwa ikifanywa na Baraza la Madiwani, Kamati za kudumu pamoja na Ofisi ya Mkurugenzi sasa TARURA  wamekuja kutekeleza kitaalam zaidi, namna ya usimamizi, manunuzi, mikataba ili tuweze kupata matokea bora na ya haraka.

Naye Mkurugenzi wa Tarura Eng. Abdul R. Digaga  amesema Mafunzo haya ni mpango wa Kimakakati wa  Tarura katika kupambana na Rushwa katika utekelezaji wa miradi ya Ujenzi na matengenezo ya barabara, mgongano wa maslahi, matumizi mabaya  ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara na ukosefu wa Uadilifu miongoni mwa watendaji. 

Mafunzo hayo ambayo yalianza kufanyika katika kanda mbalimbali Nchini na kanda hii ya Nyanda za juu kusini ni ya mwisho kufanyika kwa wataalam wa Tarura wa kada mbalimbali na imejumuisha Mikoa ya Mbeya, Songwe, Ruvuma,Rukwa,Katavi na Iringa na Njombe. 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania