CURRENT NEWS

Friday, January 26, 2018

JSI YAMKABIDHI RIDHIWANI BAISKELI 9 NA MAKABATI 11 KWA NIABA YA HALMASHAURI YA CHALINZEWa nne kutoka kulia ni mkurugenzi wa mradi wa CHSSP kutoka JSI ,Dk.Tulli Tuhuma ,Wa tatu kushoto Mbunge wa jimbo la Chalinze ,Ridhiwani Kikwete akikabidhiwa baiakeli 9 na makabati 11 kutoka JSI chini ya ufadhili wa PEPFAR/USAID ,Wa tatu kutoka kulia ni mganga mkuu wa halmashauri ya Chalinze,Dk. Rahim Hangai (picha na Mwamvua Mwinyi)

Na Mwamvua Mwinyi,Chalinze

TAASISI ya utafiti na mafunzo ya JSI, chini ya ufadhili wa PEPFAR na msaada wa watu wa Marekani (USAID), imemkabidhi mbunge wa jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete,msaada wa baiskeli  Tisa na makabati 11 yakuhifadhia nyaraka na kumbukumbu.

Baiskeli na makabati hayo, zitaelekezwa kwa wasimamizi wa kamati za ukimwi na kamati za ulinzi wa watoto wanaoishi kwenye mazingira hatarishi ili waweze kutekeleza majukumu yao kirahisi.

Akimkabidhi vifaa hivyo Ridhiwani,mkurugenzi wa mradi wa CHSSP kutoka JSI ,Dk.Tulli Tuhuma ,alisema wametoa msaada huo kutokana na kutambua Chalinze ina maeneo ambayo hayafikiki kirahisi.

Alisema makabati yatasaidia kuhifadhi nyaraka na takwimu halisi ya watoto hao na kuweka taarifa na kumbukumbu sza changamoto zao.

"Takwimu ni muhimu ,taarifa bila kumbukumbu hupotea kama hazijahifadhiwa kwenye sehemu zisizo salama" alisema dk.Tulli.

Aidha,Tulli alieleza pia wametoa mafunzo kwa
wasimamizi wa watoto wanaoishi kwenye mazingira hatarishi 161 kuanzia ngazi za vijiji na kata pamoja na wasimamizi wa wasimamizi 16 huko Chalinze ili waweze kupata uwezo na ufahamu wa mradi huo.

Akielezea mradi kijumla ,alisema lengo ni kuwezesha upatikanaji bora zaidi wa huduma bora za afya na ustawi wa jamii kwa watu walioathirika na maambukizi ya virusi vya ukimwi na walio kwenye mazingira hatarishi.

Alielezea malengo makuu ni kujenga uwezo kwa raslimali watu kwa kusaidia watu walioathirika na virusi vya ukimwi na watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu kwenye ngazi ya jamii.

"Kamati za ukimwi na kamati za ulinzi wa wanawake na watoto na kufanya kazi kwa karibu na serikali na wizara ya afya kwa kutengeneza mfumo jumuishi kwa kutambua watoto walio kwenye mazingira hatarishi na kumwezesha kumpeleka ,kwenye maeneo ya afya,ulinzi ama ustawi wa jamii"alifafanua.

Dk.Tulli alisema mradi ni wa miaka mitano ulianza 2014 ili kuiwezesha serikali ya Tanzania katika halmashauri za  wilaya 84 kudhibiti maambukizi ya Ukimwi na kufikia watoto walio kwenye mazingira hatarishi 384,000 ifikapo 2020.

Alisema wameshafikia halmashauri 68 kati yake 67 za Tanzania Bara na moja Visiwani Zanzibar na wameshatoa mafunzo kwa wasimamizi wa halmashauri 15,560 hadi sasa .

Nae Ridhiwani akiikabidhi halmashauri ya Chalinze vifaa hivyo,aliishukuru taasisi hiyo na wafadhili PEPFAR/USAID kwa msaada walioutoa .

Alisema utarahisisha kufikiwa maeneo yenye mahitaji makubwa ambayo yalikuwa hayafikiki kirahisi.

Ridhiwani alisema wasimamizi wa kamati hizo vijijini na kwenye kata watumie fursa hiyo kufika na mashuleni kujua takwimu halisi za watoto katika makundi mbalimbali ,takwimu ambazo zitasaidia katika mipango ya serikali kwenye jamii.

Aliomba ,wahusika wakatunze vifaa na usafiri huo ili kuleta manufaa .

" Wafadhili hawa wanahitaji kuona matokeo badala ya kwenda tofauti na malengo yao,Nendeni mkahudumie watoto kwenye eneo husika analostahili ikiwemo ulinzi ,ustawi wa jamii na kumfuatilia kujua kama amepata huduma"alisisitiza Ridhiwani.

Mganga mkuu wa halmashauri ya Chalinze,Dk. Rahim Hangai alisema wanakabiliwa na changamoto ya jiografia ,ambapo maeneo mengi yapo mbali na Mji.

Alisema vitendea kazi vya aina hivyo vitasaidia kutekeleza majukumu ipasavyo ambayo serikali inayasimamia.

Dk.Hangai alisema elimu waliyopatiwa wasimamizi 161 na wengine 16 ni hatua tosha ya kufanikisha kazi zao inavyostahili .

Mwisho

 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania