CURRENT NEWS

Sunday, January 7, 2018

MBUNGE UNGANDO KUTATUA KERO YA KITANDA CHA KUJIFUNGULIA HUKO MUYUYU

Mbunge wa jimbo la Kibiti, mkoani Pwani Ally Seif Ungando ,wa kwanza kulia akisafiri na msafara wake ,kwa kutumia njia ya majini kuelekea kwenye visiwa vilivyopo kata ya Kiongoroni, kwenye muendelezo wa ziara yake jimboni humo .(picha na Mwamvua Mwinyi)

Mbunge wa jimbo la Kibiti ,mkoani Pwani ,Ally Ungando ameahidi kuitatua kero ya kitanda cha kujifungulia akinamama wa kijiji cha Muyuyu kata ya Mtunda,kero ambayo imedumu kwa muda mrefu sasa.

Pamoja na hilo amesema atatoa fedha kiasi cha sh.mil.nne ambapo mil.mbili itakuwa kwa ajili ya kujenga choo kwenye nyumba ya mganga wa zahanati ya Muyuyu na milioni mbili nyingine kwa lengo la kumalizia choo katika shule ya msingi Muyuyu.

Ungando alibaini kero hiyo wakati akiwa kwenye muendelezo wa ziara yake ya siku 21 jimboni humo .

Hata hivyo Ungando ,alisema ataendelea kwenda sambamba na kauli mbiu yake yake ya mwendo kasi katika maendeleo ya Kibiti .

Alieleza ,jukumu lake kubwa ni kushirikiana na wananchi kutatua kero mbalimbali zinazowakabili ,kuzisimamia kwenye idara husika na kufuatilia yale yanayoendelea kufanyiwa kazi .

Ungando ,aliwataka wananchi wa Kibiti kushirikiana nae kuchangia pia shughuli za kimaendeleo badala ya kuisubiria serikali pekee ama wafadhili suala ambalo litawachelewesha kupiga hatua na kutoka walipo sasa .

"Ninafanya ziara hii ,sio kujua changamoto zilizojitokeza na kuwaeleza nilipofikia kwenye ufuatiliaji kwa zile nilizoanza nazo " serikali inafanya yale ambayo yapo kwenye taratibu zake hivyo na sie jamii tuiungr mkono kwa kuendeleza yale ambayo yapo kwenye uwezo wetu "alisema Ungando.

Mbunge huyo ,alipokuwa kata ya Kiongoroni alitembelea visiwa vya Pombwe,Jaja,Kiongoroni na Ruma  aliwaasa wazazi na walezi kuwapeleka watoto shule na kuacha tabia ya kuwaacha majumbani jambo ambalo linawakosesha haki ya kielimu.

Ungando alitaka wananchi wa visiwa hivyo ,kuwachunguza watu ambao wana mashaka nao kwakuwa wahalifu wakitokea Gongoni wanaweza kukimbilia visiwani.

Alisema ulinzi na usalama upo mikononi mwa kila mmoja hivyo wachunguzane wao kwa wao kwani wanajuana.

Akiwa visiwani hapo,alipokea changamoto za uchache wa watumishi wa idara ya afya,elimu ikiwemo upungufu wa nyumba za walimu na miundo mbinu ya barabara na kuahidi atazisimamia .

Wananchi wa vijiji hivyo walimshukuru Mbunge wao Kwa juhudi anazozionyesha kwa kuwatumikia na walimuomba akafanyie kazi changamoto walizomueleza ili kuondokana na adha walizonazo.

Katika ziara hiyo ,Ungando alitoa mifuko ya saruji 100 kwenye kata alizopitia ili kusaidia masuala ya maendeleo ambapo ameshatembelea kata ya Mtunda,Mtawanya,Ruaruke na Kiongoroni.

 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania