CURRENT NEWS

Wednesday, January 10, 2018

MJUMBE WA NEC PWANI AZIPAMBA KAMPENI ZA UDIWANI KATA YA KURUI KISARAWE


 Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM(NEC) Taifa Hajji Abuu Jumaa akipokea mwanachama mpya kutoka upinzani kwenye kampeni za uchaguzi kata ya Kurui.
 Mbunge wa Kisarawe Selemani Jafo akimnadi mgombea udiwani kata ya Kurui Mussa Kunikuni
 Viongozi wa CCM mkoani Pwani wakimuombea kura mgombea udiwani kata ya Kurui Mussa Kunikuni

 Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Kisarawe Khalfan Sika akimuonesha jambo Mbunge wa Kisarawe Selemani Jafo
Wanachama wa CCM wakiserebuka kwenye kampeni za udiwani kata ya Kurui
.....................................................................................
Zikiwa zimesalia siku chache kabla uchaguzi mdogo wa Ubunge na Udiwani kufanyika kwenye maeneo mbalimbali nchini Januari 13, mwaka huu, Mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa (NEC) kutoka mkoa wa Pwani Hajji Abuu Jumaa ameongoza kampeni za Udiwani wa kata ya Kurui wilayani Kisarawe na kumnadi mgombea udiwani kupitia CCM Mussa Kunikuni.

Katika kampeni hizo, Jumaa amemwagia sifa za uzalendo na uchapakazi mgombea huyo na kuwaomba wananchi wa kata ya Kurui kutofanya makosa siku ya uchaguzi huo mdogo januari 13, 2018.

Akizungumza katika kampeni hizo zilizofanyika kijiji cha Zegero, Jumaa amewaeleza wananchi kuwa "Kisarawe mmepata bahati kwa kuwa na mbunge wa Jimbo mchapakazi na mzalendo sana kwa taifa letu ndugu yetu Selemani Jafo ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi. Mnapaswa kumchagulia Diwani mzuri wa kushirikiana naye katika kata hii ili Ilani ya CCM iweze kutekelezwa vyema. Diwani huyo si mwingine bali Mussa Kunikuni"

Kwa upande wake, Jafo amewaomba wananchi wa kata ya Kurui kumchagua ndugu Mussa Kunikuni ili aweze kushirikiana naye katika kuwaletea wananchi maendeleo.

Jafo ametumia nafasi hiyo kuwaeleza wananchi mafanikio yaliyopatikana na yanayoendeleo kupatikana kupitia sekta ya Afya, Elimu, Barabara, Umeme, maji na mambo mbalimbali ya kijamii. 

Kadhalika, Katibu wa CCM mkoa wa Pwani amewatahadharisha wananchi kutokukubali kukurubuniwa na kauli za wanasiasa wa upinzani kwani hawana jipya isipokuwa wanatafuta maneno ya kuwalaghai wananchi ili wawapigie kura.

Kampeni hizo zinaendelea katika vijiji mbalimbali na zinatarajiwa kuhitimishwa Januari 12 mwaka huu katika kijiji cha Kidugalo kata ya Kurui wilayani Kisarawe.


 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania